RAIS Dk. John Pombe Magufuli, amezindua rasmi Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (Agricultural Sector Development Programme, Phase Two – ASDP II).
Mpango huo wa miaka mitano utatekelezwa hadi mwaka 2023 kwa gharama ya Sh. Trilioni 13.8 ambapo Serikali na washirika wa maendeleo watatoa asilimia 40 ya fedha hizo, na sekta binafsi itatoa asilimia 60.
Katika uzinduzi wa mpango huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Rais Magufuli alisema hakuna budi viongozi kusimamia kwa dhati mpango huo ili kuleta tija kwenye kilimo.
“Ninataka viongozi wawe sehemu ya mpango huu wa kilimo, tunao wataalamu muwatumie vizuri katika ushauri na utekelezaji wa maazimio mtakayoyaweka kwenye vikao vyenu vya kila siku,” alisema Rais Magufuli.
Viongoni waliohudhuria ni pamoja na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, , Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu Mstaafu, , Mizengo Peter Pinda, Mawaziri, Wabunge, Mabalozi, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, wadau wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, wadau wa sekta binafsi, viongozi wa dini na viongozi wa siasa.
Alisema lengo la mpango huo, kuleta mageuzi katika sekta ndogo za kilimo, mifugo na uvuvi ili kuongeza uzalishaji na tija, kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara zaidi badala ya kujikimu pekee, kuongeza mapato ya wakulima, uhakika wa usalama wa chakula na lishe na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi kwa ujumla.
Vilevile amewahakikishia wakulima, wafugaji na wavuvi kuwa Serikali itashirikiana nao kwa karibu katika utekelezaji wa mpango huu, lakini ameelezea kutoridhishwa kwake na utendaji wa benki ya maendeleo ya kilimo ambayo amesema licha ya kuwezeshwa na Serikali mtaji wa takribani Shilingi Bilioni 300 kwa ajili ya kuwakopesha wakulima, imekuwa haiwakopeshi wakulima.
Hata hivyo, ameonyesha kutoridhishwa na mwenendo wa benki ya kuwasaidia wakulima ambapo alibainisha kuwa ipo haja ya kuisaidia serikali kutimiza malengo yake katika sekta ya kilimo.
“Naomba niwe mkweli, bado sijaridhika na utendaji kazi wa benki hii, benki ipo pale kwa ajili ya kuwakopesha wakulima, Serikali inakopa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya kuwakopesha wakulima, lakini yenyewe inachukua hizo hela na kwenda kuzikopesha benki zingine” alisema.
Aliongeza “Kwa hiyo tumekopa pesa kutoka AfDB Sh. Bilioni 207, mtaji umewekwa na Serikali Sh. Bilioni 60 tangu mwaka 2014, lakini hakuna fedha iliyokwenda kwa mkulima na wakati mwingine benki hii inapotaka kukopesha huwatafuta matajiri wakubwa ambao baadhi yao wameshindwa kulipa mikopo yao kwenye benki zingine, sasa nikisema siridhiki na utendaji wa benki hii mtanikatalia ndugu zangu?”
Aidha, Rais amewataka viongozi wa Serikali kutoa taarifa juu ya juhudi za Serikali kuimarisha sekta ya kilimo ikiwemo utekelezaji wa Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo Ukanda wa Kusini (SAGCOT) ambao mwaka 2016 ulipatiwa Sh Bilioni 150 za mkopo kutoka Benki ya Dunia na mradi wa kuunganisha matrekta uliopatiwa mkopo wa takribani Sh. Bilioni 248.
Rais Magufuli amemtaka Waziri wa Kilimo Mhe. Dk. Charles Tizeba kuchukua hatua dhidi ya mzigo wa tozo zinatozwa na bodi mbalimbali za mazao nchini, ambazo zimekuwa zikiwaumiza wakulima ilihali bodi hizo hazichangii katika gharama za uzalishaji wa mazao.
Awali kabla ya hotuba ya Rais Magufuli, Waziri Tizeba alieleza kuwa katika utekelezaji wa mpango wa ASDP II Serikali imetenga Sh. Bilioni 943 kupitia wizara mbalimbali katika bajeti ijayo na washirika wa maendeleo wameahidi kutoa sh. Trilioni 1 na Bilioni 900.
“Tofauti na awamu ya kwanza ya mpango huu, awamu hii ya pili itajielekeza katika mazao machache ya kipaumbele katika kilimo, mifugo na uvuvi yenye kugusa watu wengi na yaliyochaguliwa kwa kuzingatia mnyororo wa thamani na ikolojia ya kanda za kilomo”.
Dk. Tizeba amebainisha kuwa ASDP II inatekelezwa wakati kukiwa na maendeleo mazuri katika sekta ya kilimo ikiwemo kutosheleza mahitaji ya chakula kwa asilimia 123, kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara kutoka tani 796,502 mwaka 2015/16 hadi tani 881,583 mwaka 2016/17 huku kukiwa na uzalishaji mkubwa wa zao la pamba msimu uliopita ambapo umeongezeka kutoka tani 133,000 hadi kufikia tani 600,000.
Nao wawakilishi kutoka kwa wakulima, wafugaji, wavuvi, sekta binafsi, Kamati ya Kudumu ya Bunge na washirika wa maendeleo ya sekta ya kilimo wamemuahidi Rais Magufuli kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa ASDP II ili malengo yaliyokusudiwa yafanikiwe.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment