Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, amesema Maelekezo ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu utoaji wa habari za Serikali kwa umma yanatekelezwa kwa kasi na ofisi au mtendaji yeyote wa ofisi ya umma atakayekaidi asitafute wa kumlaumu.
“Waziri wa Habari Mhe Innocent Bashungwa, hivi ninavyoongea hapa ameshasaini barua yenye maelekezo hayo na zaidi kuzijulisha taasisi zote za umma nchini kuhusu tathmini itakayofanyika,” alisema.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo leo mkoani Morogoro wakati akitoa mada kwenye semina ya wahariri kuhusu Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere.
Amesema utoaji wa habari kwa umma ni jambo la kisheria na kikatiba hivyo hata maelekezo ya Rais yako sahihi na atakayekaidi “amekaidi mamlaka, amekaidi sheria na amekaidi katiba.”
Katika hatua nyingine, Dkt. Abbasi amewataka wahariri na waandishi nchini kuenzi misingi ya weledi na uzalendo katika kazi zao ikiwemo kufanya utafiti kwanza kuliko “kufakamia” mawazo na maoni ya watu wasioitakia nchi mema.
“Baadhi ya waandishi hawafanyi utafiti wala kutaka kujua mambo kwa kina na huishi wakifakamia tu kila kinachosemwa na mabeberu kupinga maendeleo yetu. We mwandishi gani sisi ndio Serikali na ndio wenye hela na ndio wenye mradi tunakwambia tunakwenda kujenga mradi Rufiji, anatokea wakala wa mabeberu mmoja kashiba mivyakula ya kwenye kopo huko anakofadhiliwa kuishi anakwambia huo mradi hautajengwa, hawana hela hao, mwandishi unatoka unamwamini wakala wa beberu unaandika na kusambaza uongo, we vipi mbona hatukuelewi na wewe ni wa moto au wa baridi?” alihoji Dkt. Abbasi akisisitiza tangu utekelezaji wa mradi wa Umeme JNHPP Rufiji uanze hakuna malipo ambayo Serikali imechelewesha au kushindwa kuwalipa wakandarasi.
0 comments:
Post a Comment