Naibu Waziri wa Nishati,Wakili Stephen Byabato (aliyenyoosha mkono) akiwaonyesha kitu wasimamizi wa ujenzi wa kituo wakiwemo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wakati wa ziara ya kukagua eneo litakalojengwa Kituo cha Kupoza Umeme kilichopo Kijiji cha Imalilo wilayani Bariadi mkoani Simiyu, Februari 24,2021.
Naibu Waziri wa Nishati,Wakili
Stephen Byabato, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukamilisha haraka
zoezi la kuwalipa fidia wananchi waliobaki ambao wamepisha Mradi wa Ujenzi wa Kituo
cha Kupoza Umeme kilichopo Kijiji cha
Imalilo wilayani Bariadi mkoani Simiyu, kabla ya mwezi Machi mwaka huu.
Wakili Byabato alitoa
maagizo hayo, Februari 24, 2021 baaada ya kufanya ziara ya kutembelea eneo hilo
linalotarajiwa kuanza kujengwa kituo hicho mwezi Julai mwaka huu, na kuzungumza
na baadhi ya wananchi ambao bado hawajalipwa fidia kutokana na changamoto
mbalimbali kujitokeza.
Alitaja baadhi ya
changamoto hizo kuwa ni pamoja na kutofautiana kwa majina yaliyoandikwa katika
vitambulisho vyao, nyaraka na hundi, zilizokuwa zikitumika kuwalipa fedha za
fidia.
Aliweka wazi kuwa ni
wananchi watano (5) tu kati ya Arobaini na Watano (45) waliopaswa kulipwa fidia
bado hawajalipwa, Arobaini (40) tayari wamekwishalipwa na kuondoka kupisha
mradi.
Kwa mantiki hiyo aliwaelekeza
TANESCO kushirikiana na Idara na Taasisi husika ili kushughulikia na kumaliza
changamoto hizo zinazokwamisha malipo ya wananchi hao, na kuhakikisha
wanawalipa wote kabla ya mwezi machi mwaka huu, ambapo kunatarajiwa kuwekwa
jiwe la msingi la kuanza ujenzi wa mradi huo.
Sambasamba na hilo,
alitaka kuhamishwa kwa makaburi yaliyopo katika eneo hilo kwa kufuata utaratibu
na sheria za nchi, kuzingatia haki ya kila alieyepisha mradi huo, kuepuka
malalamiko kutoka kwa wananchi.
“TANESCO kamilisheni
ulipaji wa fidia kwa waliobaki, hizi changamoto zao zinatatulika shirikianeni
na mamlaka husika pitieni nyaraka na kufuata sheria zinazotakiwa muwalipe fedha
zao hawa wananchi, ili waendelee na maisha yao na mradi uanze kujengwa hapa,
hatutaki mradi huu ulete malalamiko kwa wananchi tunataka haki itendeke kwa
kila aliyepisha mradi huu na afurahie uwepo wake hapa, mapema mwezi Machi tutaweka
jiwe la msingi, sitaki kusikia malalamiko siku hiyo”, alisema Wakili Byabato.
Aidha katika ziara
hiyo Wakili Byabato alitoa msisitizo kwa TANESCO, kuendelea kukata umeme kwa
wadaiwa sugu ambao bado hawajalipa madeni ya Ankara zao na bado wanaendelea
kutumia umeme.
Alisema ukataji wa
umeme unawahusu wadaiwa wote bila kujali Taasisi, Mashirika ya Umma, Binafsi wala
Dini.
Hata hivyo
aliwasisitiza TANESCO kukata umeme kwa kuzingatia faida kwa maana kuwa mteja
akilipa fedha kidogo atarejeshewa umeme kwa siku kadhaa, baadaye wakate tena
hivyohivyo hadi pale atakapomaliza deni lake.
Vilevile wasikatae
kupokea fedha ya mteja atakayoona anaweza kulipa kwa kipindi husika, wapokee
wamuwashie baada siku kadhaa wakate tena.
Pia wawe na tabia ya
kuwatembelea wadaiwa wao ili kuwakumbusha juu ya ulipaji wa madeni yao na kufanya
ukaguzi ili kujiridhisha kama mteja aliyekatiwa umeme kwa muda mrefu anatumia nishati gani, hiyo itasaidia kubaini
wateja wasiowaaminifu wanaoiba umeme.
0 comments:
Post a Comment