METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, December 5, 2020

WAHITIMU VETA WAASWA KUJIUNGA KATIKA VIKUNDI

Wahitimu wa chuo cha ufundi stadi na huduma VETA Mwanza wametakiwa kujiunga katika vikundi ili waweze kujiajiri na kukopesheka.

Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa sherehe za mahafali ya arobaini ya wahitimu wa mwaka wa pili kwa mwaka huu ambapo amewataka kujiunga katika vikundi ili iwe rahisi kukopesheka kupitia mikopo ya halmashauri au taasisi binafsi kulingana na mradi wanaokusudia kuufanya jambo ambalo litasaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira katika soko

'.. Kwa watakaoingia katika ajira isiyo rasmi, Ni vema niwashauri kuunda au kujiunga na vikundi vidogo vidogo ili kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali za fedha na mie nitakuwa mstari wa mbele kuwakingia kifua mpate hata zile kazi za zabuni zinazotangazwa na manispaa ..' Alisema

Aidha Dkt Mabula akawasisitiza wahitimu hao kuziishi ndoto zao sanjari na kuchukua tahadhari dhidi ya makundi mabaya  ili  kuepuka kutumbukia kwenye majanga kama ukimwi na matumizi ya dawa za kulevya.

Kwa upande wake mkuu wa chuo Cha VETA Mwanza Ndugu John Mathias Kengese akasema kuwa zaidi ya wanafunzi 105 wa fani za useremala, ushonaji, ujenzi, upakaji rangi na uchomeleaji vyuma wamehitimu katika Mahafali hayo sambamba na kutaja changamoto zinazokabili chuo hicho ikiwemo upungufu wa walimu, uchakavu na uhaba wa vifaa vya kisasa vya kufundishia

Akihitimisha moja ya wahitimu wa Mahafali hayo Bi Janeth Francis mbali na kushukuru Serikali kwa jitihada zake katika kutoa fursa kwa vijana kujifunza ujuzi tofauti tofauti chuoni hapo akawataka wahitimu wenzake kuyaishi yale yote waliyofundishwa wakati wakiwa chuoni hapo na kujiepusha dhidi ya matendo yasiyofaa katika jamii
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com