METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, December 21, 2020

MUSOMA YAPEWA JUKUMU ZITO

Katibu Tawala Mkoa wa Mara Karolina Mthapula akizungumza na wajumbe wa Kamati ya ulinzi kwa Mwanamke na Mtoto kwa Manispaa ya Musoma katika ukumbni wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Katibu Tawala Mkoa wa Mara Karolina Mthapula amezitaka Kamati za ulinzi kwa Mwanamke na Mtoto mkoani humo kuwajibika katika kuhakikisha inasaidiana na jamii kutokomeza vitendo vya ukatili hasa katika maeneo ya vijijini.

 

Karolina Mthapula ameyasema hayo mkoani Mara wakati akifungua Mafunzo na uwezeshaji kwa Kamati za ulinzi kwa Mwanamke na Mtoto ya Wilaya Musoma yaliyoratibiwa na Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na Shirika la UNFPA.

 

Karolina amesema kuwa ili kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto ni lazima vyombo mbalimbali kuunganisha nguvu pamoja.

 

Ameongeza kuwa suala la mila na desturi katika jamii zetu lizingatie kuendeleza mila na desturi zilizo nzuri na zenye manufaa katika jamii ili ziweze kusaidia mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.

 

 “Tuongeze nguvu katika ngazi za vijijini ma mitaani kwani huko kuna changamoto kubwa ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto” alisema

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Grace Mwangwa amesema Serikali inatambua kwamba utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) unafanyika hasa katika ngazi za mitaa hivyo ni muhimu kwa Kamati za Wilaya kushuka chini kuwapa mafunzo na kuwezeshwa kuwafikia wananchi na kuwapa elimu juu ya kutokomeza vitendo vya ukatili.

 

Ameongeza kuwa viongozi wa Halmashauri na Manispaa zilipo Kamati hizo kuwasaidia kuziwezesha Kamati hizo vitendea kazi kwa ajili ya kuwasaidia katika kutekeleza majukumu yao pale inapotokea kitendo cha kikatili katika maeneo mbalimbali.

 

Aidha Mstahiki Meya wa Manispaa ya Musoma, William Gumbo amesema jamii inapaswa kuwa wazi na kuvunja ukimya kwa kuyazungumza masuala haya ya vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto hasa kwa viongozi wa kisiasa kuwa kipaumbele katika kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomea.

 

“Sisi Viongozi wa kisiasa tunawajibu mkubwa wa kuibebea agenda hii ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika maeneo yetu hivyo tuwajibike katika hili” alisema

 

Kwa upande wake Mzee maarufu Obadia Bulenga amesema elimu aliyoipata kuhusu kupambana na vitendo vya uaktili dhidi ya Wanawake na Watoto atahakikisha inafika kwa jamii inayomzunguka hasa katika vikao vya mitaa na hata katika maongezi na watu mbalimbali.

 

Naye Kiongozi wa Dini kutoka Kanisa la EAGT Musoma Mchungaji Msaidizi Nicobili Mfanyi amesema kuwa atatumia ibada kutoa elimu jinsi ya kupambana na kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ili jamii ijue na ichukue hatua ya kuondokana na vitendo hivyo.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com