Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, Ernest
Mangu ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Rwanda (kushoto) na Meja
Jenerali Mstaafu, Simon Marco Mumwi ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini
Urusi, kabla ya mazungumzo, ofisini kwa Waziri Mkuu mjini Dodoma, Aprili 8,
2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa akizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, Ernest Mangu
ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Rwanda (kushoto) na Meja Jenerali Mstaafu,
Simon Marco Mumwi ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Urusi ofisini kwa
Waziri Mkuu mjini Dodoma Aprili 8, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka mabalozi wanaoiwakilisha
Tanzania nchini Urusi na Rwanda kutumia fursa hiyo kwa kutangaza vivutio vilivyopo
nchini ili kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo
ya utalii.
Pia amewataka Mabalozi kila mwisho wa mwaka wajifanyie
tathmini ya mafanikio waliyoyapata kutokana na uwakilishi wao katika Mataifa
ambayo ni kwa kiasi gani wamechangia
kwenye uboreshaji wa maendeleo ya Taifa.
Ametoa maagizo hayo leo (Jumapili, Aprili 8, 2018)
wakati akizungumza na Balozi Ernest Mangu anayewakilisha Tanzania nchini Rwanda
na Balozi Simon Mumwi anayewakilisha Tazania nchini Urusi, katika ofisi ya Waziri Mkuu
mjini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema Tanzania ina vivutio vingi vya
utalii ikiwa ni pamoja na uwepo wa mbunga za wanyama, hivyo ni vyema wanapoondoka
wachukue nyaraka zote zitakazowasaidia katika kutangaza vivutio vya utalii ili
kuongeza idadi ya watalii nchini.
Amesema mbali na kutangaza sekta ya utalii, pia
watafute wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta nyingine kama vile
madini, viwanda na kutafuta masoko ili wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania
waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi.
“Pia mkajifunze mbinu ambazo wenzetu wanazitumia
katika kuboresha sekta mbalimbali ambazo na sisi tunazo hapa nchini kama za
viwanda na kisha mje mtueleze namna ya kuziboresha. Kujifunza ni jambo zuri
hivyo msisite kufanya hivyo huko muendako.”
Pia
Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao wakawatambue na kuwaunganisha Watanzania
waishio kwenye nchi wanazoiwakilisha ili nao washiriki kwenye ujenzi wa uchumi
wa viwanda na wawasisitize wafuate sheria za nchi wanazoishi na wakumbuke
nyumbani.
Waziri
Mkuu amewasisitiza mabalozi hao kwenda kupunguza gharama za uendeshaji wa
Balozi kwa kuzuia matumizi katika mambo yasiyo ya lazima. “Pia maslahi ya nchi
lazima mkayasimamie huko muendako hasa katika masuala ya kiuchumi.
Kwa upande wao mabalozi hao wamesema watahakikisha
wanayafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa ikiwa ni pamoja na kuimarisha
ushirikiano baina ya Tanzania na nchi wanazoziwakilisha.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI,
NOVEMBA 16, 2017.
0 comments:
Post a Comment