Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), Bw. Joseph Haule, akiwa na Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Julius Ngusa, pamoja na wajumbe wengine wakikagua athari za miundombinu ya barabara katika eneo la Jangwani ambapo bodi hiyo imeridhia kutoa bilioni nne kukarabati eneo hilo.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Dar es
Salaam, Mhandisi Julius Ngusa, akitoa taarifa kwa wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa
Barabara katika ziara yao ya kukagua hali ya mtandao wa barabara kwa mkoa huo
na kutembelea kujionea athari za miundombinu katika eneo la Jangwani.
Serikali kupitia Mfuko wa Barabara (Road fund) imesema ipo
tayari kupitisha kiasi cha shilingi bilioni nne kwa ajili ya kumlipa mkandarasi
atakaepatikana ili kuboresha miundombinu ya jangwani mara baada ya uhakiki wa
makisio hayo kukamilika na kujiridhisha.
Akizungumza kwa niaba ya
wajumbe wa Bodi ya mfuko huo,
Mwenyekiti wa Bodi Bw. Joseph Haule, amesema kuwa nia ya Serikali ni
kuhakikisha inatatua changamoto hiyo haraka kabla ya mvua za masika kuanza.
"Bodi imeona tatizo hili
na tumeliona kama suala la dharura, ndio maana tumekuja hapa kujionea hali
halisi ili kutafuta njia sahihi ya kutatua tatizo hili ambalo limekuwa kero kwa
muda mrefu", amesema Mwenyekiti wa Bodi.
Aidha, Bw. Haule amefafanua
kuwa kweli tatizo ni kubwa, mfereji una kina kifupi na makalvati mawili makubwa
yaliyopo hapo yameziba kabisa.
Ameongeza kuwa nia ya Bodi ni
kuona wananchi na wasafirishaji wanatumia muindombinu hiyo wakati wote wa mvua
na kiangazi
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia
Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, amesema kuwa Serikali kupitia Wizara
yake imeandaa mkakati wa muda mrefu kuhusu miundombinu hiyo ambapo amesema kuwa
kwa sasa wataalamu wanafanya usanifu wa kina kwa ajili ya kuja na suluhisho la
kudumu ikiwemo ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 300.
Mwakalinga amefafanua kuwa
aliagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuhakikisha wanatafuta
ufumbuzi wa haraka ikiwemo kutoa mchanga ambao umetuama katika eneo hilo ili
kuinusuru miundombinu hiyo.
Naye, Meneja wa TANROADS mkoa
wa Dar es salaam, Mhandisi Julius Ngusa, amethibitisha kuwa ofisi yake
inaendelea kuhakikisha kuwa michanga inayotuama katika eneo hilo inatolewa kwa
wakati ili kuruhusu magari kuweza kupita mara baada ya mvua kunyesha.
Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wametembelea eneo la Jangwani kujionea hali halisi ya miundombinu katika eneo hilo ambayo imekuwa ikiathiriwa na mvua na kusababisha kufunga mawasiliano ya watumiaji wa barabara ya Morogoro hususani eneo hilo kila mwaka.
0 comments:
Post a Comment