METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, December 17, 2020

Baraza la Madiwani Makete lagomea kupokea taarifa

BARAZA la madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Makete Mkoani Njombe wamegoma kupokea taarifa ya utendaji kazi wa halmashauri hiyo kwa kile walichodai ni kutokana na kucheleweshewa kupewa taarifa hiyo .

Miongoni mwa madiwani hao pia yumo Mbunge wa Makete Festo Sanga ambao kwa kauli moja wamesema hawawezi kuipitisha taarifa hiyo kwani kuna baadhi ya miradi wanaitilia shaka hasa katika matumizi yake ya fedha ikilinganishwa na uhalisia wa miradi husika.

Wamesema,lazima wapate muda wa kuipitia taarifa hiyo kifungu kwa kifungu ili wajiridhishe  kama fedha zilizotumika ni sawa na miradi inayoonekana kwenye taarifa hiyo.

Mgomo huo umetokea leo katika kikao cha kwanza cha baraza la madiwani tangu ufanyike uchaguzi Mkuu ambapo baada ya kula kiapo ndipo wakapewa ripoti hiyo kutoka kwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ili waipokee na na  kupitisha .

Kwa mujibu wa madiwani hao,kutokana  na Mwongozo uliotolewa na Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI ) wanapaswa wapatiwe taarifa  kabla ya siku saba ili waisome vizuri na kujiridhisha katika kazi ambazo zimefanyika.

Akizungumza katika kikao hicho Sanga amesema kuwa serikali imetoa mwongozo kwamba   diwani anatakiwa apate taarifa siku saba  kabla ya kikao ili kumwezesha kupata muda wa kusoma na kujiridhisha kama yale yaliyomo kwenye taarifa husika yana uhalisia.

 Ameshauri kikao hicho kiahirishwe na badalanyake kifanyike kesho ili leo wajumbe wakaipitie taarifa hiyo na kisha wafanye maamuzi sahihi ya kuipitisha ama kutoipitisha taarifa hiyo.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Francis Chaula amepokea ushauri huo na kuahitisha kikao hicho hadi kesho.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com