Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii), Dkt. John Jingu amewataka Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini kubuni mbinu zitakazowawezesha kufanya kazi wa ufanisi na kuchochea maendeleo ya Nchi.
Katibu Mkuu Dkt. Jingu amesema hayo Mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu na Makamu Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kutoka Vyuo vinane na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru vilivyo chini ya Wizara hiyo.
Amesema baadhi ya viongozi wakiwemo Wakuu wa Vyuo wamekuwa na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na hivyo kushindwa kuleta maendeleo yaliyokusudiwa.
Amesema Wakuu wa Vyuo wanatakiwa kuwa na maono yatakayowezesha utoaji wa mafunzo kwa wanafunzi kuajiriwa, kujiari na kuwaajiri wengine na hivyo kuleta mabadiliko chanya kutokana na kuhamasisha maendeleo kwa jamii husika.
“Wanafunzi wapatiwe mafunzo ambayo yatawawezesha kutumia maarifa wanayoyapata vyuoni na kuyatafsiri kwa matendo katika jamii zao na hivyo kuharakisha maendeleo ya Taifa” alisema
Aidha amesema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii imeanza kushirikiana na wadau wengine kubuni kuanzishwa vituo vya ubunifu vya kidigitali ambavyo vinatumika kuwanoa wanavyuo ili waweze kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Patrick Golwike amesema mafunzo hayo kwa wakuu wa Vyuo va Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, ni kuwawezesha kupata ujuzi katika masuala ya uongozi na hivyo kuongeza tija.
Amesema viongozi hao wanawajibika kupata uelewa katika uongozi na mbinu za kutafuta ufumbuzi na masuala mbalimbali sambamba na kubuni mbinu za kuboresha elimu inayotolewa katika vyuo wanavyoviongoza.
Akizungumzia mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mlale, Luciana Mvula amesema mafunzo hayo ya uongozi ni muafaka kutokana na mabadiliko yanayotokea katika nyanja mbalimbali za maisha.
Ameogeza kuwa mbinu za uongozi ni muhimu katika kuwaandaa wanafunzi watakaoweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Wakuu na Makamu Wakuu wa vyuo wanaopata mafunzo wanatoka katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (Arusha), vyuo vya Maendeleo ya Jamii Ufundi Mabughai (Tanga) na Misungwi (Mwanza), Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, Mlale (Ruvuma), Uyole (Mbeya), Rungemba (Iringa), Ruaha (Iringa), Buhare(Mara) na Monduli(Arusha).
0 comments:
Post a Comment