Katibu wa Machinga Network mkoa wa Iringa Joseph Kilienyi akizungumza na wafanyabiashara wadogo wadogo wakati akieleza kuridhishwa kwa mwenendo wa biashara kwa wafanyabiasha hao wa soko la mashine tatu manispaa ya Iringa.
Na Fredy Mgunda,Iringa.
Wafanyabiashara wadogo wadogo wa mkoa wa Iringa(MACHINGA NETWORK)wameridhishwa na hali ya kibiashara inavyoendelea hivi sasa baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona ambao ulisababisha hasara kwa wafanyabiashara hao.
Wakizungumza na blog hii wafanyabiashara wa soko la mashine tatu walisema kuwa biashara zimerejea katika hali ya kawaida kama ilivyokuwa awali na wameanza kupata faida na kurudisha mitaji yao iliyokuwa imeyumba kipindi cha ugonjwa wa Corona.
Antony mashaka alieleza kuwa kipindi cha Corona alikuwa anashindwa kuuza biashara yake ya mitumba katika soko hilo kwa wingi kutokana na mashariti yaliyokuwa yamewekwa kutokana na uwepo wa ugonjwa wa Corona lakini kwa sasa anauza kwa faida kwa kuwa hakuna yale mashariti tena.
"Ndugu mwandishi angalia hapa kuna wateja wengi ambao wanachagua nguo za mitumba bila mashariti kama ilivyokuwa kipindi cha Corona ndio maana saizi tunasema biashara imerudi kama ilivyokuwa awali kabla ya Corona na faida tunapata kubwa ndio maana tupo hapa"alisema Mashaka.
Mashaka aliongeza kwa kuwaomba wateja wa nguo za mitumba kwenda katika soko hilo kununua nguo hizo zinazouzwa kwa bei nafuu na wasiogope msongamano mkubwa kwa kuwa saizi hakuna tena ugonjwa wa Corona kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli ambavyo amekuwa akisisitiza kuwa hakuna tena ugonjwa huo hapa nchini.
Bi Amina Salum ambaye ni mfanyabiashara wa viazi mviringo alisema kuwa ulikuwa wakati mgumu sana kufanya biashara kipindi cha Corona kutokana na hofu iliyokuwa imetanda kwa miongoni mwa watanzania na dunia kwa ujumla juu ya ugonjwa huo ambao ulikuwa tishio kubwa kwa dunia na bado tishio kwa baadhi ya nchi ambazo bado ugonjwa huo upo.
"Kwa kweli tunamshukuru Mungu kwa kutuepusha na Corona kwa sababu saizi tunafanya kazi zetu za kibiashara kama mwanzo na wateja wanakuja kununua bidhaa zetu bila ya kuwa na hofu yoyote ile ya ugonjwa huo" alisema Salum .
Nao baadhi ya wanunuzi katika soko la mashine tatu walisema kuwa walikuwa wanahofu kubwa ya kwenda sokoni hasa katika soko hilo kutokana na mashariti yaliyokuwepo kipindi cha ugonjwa wa Corona hivyo kusababisha kushindwa kufika katika soko hilo.
Lakini walieleza kwamba baada ya ugonjwa wa Corona sasa wanaendelea kwenda kupata huduma kwenye soko hilo ambalo bidhaa zake zinapatikana kwa bei nafuu kuliko maeneo mengine na kuongeza mzunguko wa biashara katika soko hilo.
"Saizi tunakuja sokoni bila shaka yoyote ile kununua bidhaa zetu tunazozitaka kutokana na mahitaji yetu ambayo tunahitaji katika soko hilo la mashine tatu"walisema.
Kwa upande wake katibu wa Machinga Network mkoa wa Iringa Joseph Kilienyi alisema kuwa baada ya ugonjwa wa Corona biashara zimerejea katika hali ya kawaida na wafanyabiashara wadogo wadogo wanaendelea kufanya biashara kama kawaida.
"Ukiangalia saizi maeneo yote ya kibiashara yanaendelea na biashara kama kawaida kutokana na kuondolewa na mashariti ya ugonjwa wa Corona hivyo wafanyabiashara na wanunuzi wapo huru" alisema kilenyi.
0 comments:
Post a Comment