Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Yusuph Singo (kulia) akipokea kombe la michuano Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika, (COSAFA) kwa mwaka 2020/2021 kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi wakati wa hafla iliyoandaliwa na Serikali ya kuwapongeza wachezaji wa Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake wenye umri wa chini ya miaka 17 (U-17) baada ya kuwa mabingwa wa michuano hiyo iliyofanyika Afrika Kusini hivi karibuni.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Yusuph Singo (kulia) akipokea mkanda wa WBF Intercontinental Super Welter Weight kutoka kwa Hassan Mwakinyo (kushoto) ambao ameutetea baada ya kumtwanga Jose Carlos Paz wa Argentina kwa TKO raundi ya nne mchezo uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya mpira wa
miguu ya wanawake wenye umri wa chini ya miaka 17 (U-17) wakiwa katika hafla
iliyoandaliwa na Serikali kuwapongeza mabingwa wa michuano ya Baraza la Vyama
vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika, (COSAFA) yaliyofanyika Afrika Kusini hivi
karibuni.
Serikali ipo mstari wa mbele na itaendelea kutenga
fedha na kutoa mchango katika kuziandaa timu za taifa kwa hali na mali hatua
ambayo ni kichocheo cha kukuza michezo nchini pamoja na ufadhili unatolewa kwa
timu hizo na wadau mbalimbali ndani na nje ya na nchi.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini
Yusuph Singo amebainisha hayo leo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Katibu Mkuu
wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi wakati wa
hafla ya kuwapongeza wachezaji wa Timu ya mpira wa miguu ya wanawake wenye umri
wa chini ya miaka 17 (U-17) ambao ni mabingwa wa michuano Baraza la Vyama vya
Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika, (COSAFA) kwa mwaka 2020/2021.
“Kuanzia sasa kamati zote zitakazokuwa zinahusisha
timu za taifa katika michezo yote, wahakikishe Serikali na Baraza zinashiriki
tangu mipango ya awali ili kuhakikisha nia ya kusaidia kikamilifu timu za taifa
inafanyika hatua itakayosaidia Serikali kufahamu kila kitu kinachoendelea
katika michezo yote nchini” Alisema Singo.
Singo ameongeza kuwa ili taifa liweze kufanya vizuri
katika michezo ni lazima kuwekeza katika michezo kwa vijana wa chini ya miaka
15, 17, 20 na 23 hatua itakayosaidia taifa kupata timu bora na hatimaye kufanya
vizuri katika mashindano mbalimbali kwa vijana ambao ni uwekezaji wenye tija
katika kuandaa timu bora za taifa.
Katika hatua nyingine, Singo amelisisistiza Baraza la
Michezo la Taifa (BMT) kuendelea kushirikiana na vyama vya michezo nchini
kuhakikisha michezo husika inakuwa na mchango na kulisaidia taifa kufanya
vizuri kitaifa na kimataifa.
Timu ya ya Taifa ya wanawake ya U-17 wamechukua
ubingwa wa michuano Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika,
(COSAFA) baada ya kuwafunga Zambia kwenye fainali za mashindano hayo kwa
mikwaju ya penati 3-4 kufuatia sare ya 1-1 iliyofanyika uwanja wa Nelson
Mandela Bay, Afrika Kusini.
Akiwapokea washindi hao wa COSAFA, Rais waShirikisho
la Soka nchini (TFF) Walles Karia amesema ushindi walioupata Timu ya ya Taifa ya wanawake ya U-17 ni
zawadi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na
kwa mlezi wao ambaye pia ni Mkamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mama Samia Suluhu Hassan katika kuliongoza taifa.
“Hii imekuwa ni timu ya kwanza kutoa zawadi viongozi
wetu, Mhe. Rais na Makamu wa Rais tangu wachaguliwe kuliongoza taifa kwa
kipindi kingine cha miaka mitano” alisema Karia
Pia Rais wa TFF amesisitiza kuimarishwa kwa
ushirikiano katika programu za soka zinazotolewa na Shirikisho kwa vijana wa
kike na wa kiume kwa kuwa huo ndiyo msingi mzuri wa timu za Taifa kwa miaka
ijayo.
Kwa upande wa wachezaji wakiongozwa na Aisha Masaka
katika safu ya ufungaji ambaye amekuwa na mchango katika ushindi huo kwa
kufunga magoli 10 katika mechi tano ambayo ni wastani wa kufunga magoli mawili
kila mechi amesema wameridhishwa na ushirikiano walioupata kutoka Serikalini na
viongozi wa TFF hatua iliyowasaidia kufikia kuwa mabingwa wa COSAFA.
Tanzania imekuwa mgeni mwalikwa nchini Afrika Kusini
ambaye mara mbili imetwaa kumbe katika ukanda wa COSAFA ambapo mwaka 2019 timu
ya U-20 ya wanawake “The Tanzanite” ilialikwa kwenye mashindano hayo ambayo
yalifanyika Afrika Kusini ambapo nao walifanikiwa kubeba ubingwa pia.
Wakati huo huo, pia wachezaji wa mchezo wa ngumi za
kulipwa Hassan Mwakinyo na Zulfa Yusufu Macho wamepongezwa kwa kupeperusha vema
bendera ya taifa kwa kushinda katika mashindano yao yaliyofanyika hivi karibuni
jijini Dar es Salaam.
Zulfa Yusufu Macho alimshinda kwa kwa points Alice Mbewe wa Zambia kwa uzito wa Super Fly weather weight wakati Bondia Mtanzania Hassan Mwakinyo ametetea mkanda wake wa WBF Intercontinental Super Welter Weight baada ya kumtwanga Jose Carlos Paz wa Argentina kwa TKO raundi ya nne.
0 comments:
Post a Comment