METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, October 8, 2020

NAWAPONGEZA KACU KWA KUUNGA MKONO DHANA YA RAIS MAGUFULI YA UCHUMI WA VIWANDA KWA VITENDO – KATIBU MKUU KUSAYA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akiwahutubia Wageni waalikwa wakiwemo Wakulima na Wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (KACU) katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata pamba kilichozinduliwa leo na Naibu Waziri Kilimo, Mhe. Hussein Bashe Mjini Kahama.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akiwahutubia Wageni waalikwa wakiwemo Wakulima na Wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (KACU) katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata pamba kilichozinduliwa leo na Naibu Waziri Kilimo, Mhe. Hussein Bashe Mjini Kahama.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akiteta jambo na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack wakati wa hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata pamba mjini Kahama leo.


Sehemu ya Wakulima na Wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha KACU wakifuatilia matukio katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda hicho leo mchana tarehe 8 Oktoba, 2020 mjini Kahama.

Naibu Waziri Wizara ya Kilimo Mhe. Hussein Bashe mwenye mkasi, akiwa pamoja na Viongozi wa mkoa wa Shinyanga, Wizara ya Kilimo na Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali akikata utepe kuashiria kuzindulia rasmi kwa kiwanda cha kuchakata pamba kinachomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (KACU) leo mchana, tarehe 8 Oktoba, 2020 mjini Kahama; Kiwanda hicho kilisimama uchakati wa zao la pamba tangu msimu wa kilimo wa 2013/2014.

Naibu Waziri Wizara ya Kilimo Mhe. Hussein Bashe mwenye shati nyeusi akipata maelezo kutoka kwa fundi mitambo mara baada ya mashine za kiwanda cha kuchakata pamba kuzinduliwa leo  mjini Kahama wengine ni Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya amewapongeza Wananchama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (Kahama Cooperative Union Ltd – KACU) kwa kuzindua rasmi kiwanda cha kuchakata pamba, hafla iliyoongozwa na Mhe. Hussein Bashe, Naibu Waziri Kilimo, mchana wa leo tarehe 8 Oktoba, 2020 katika mji wa Kahama.

Katibu Mkuu Kilimo Bwana Gerald Kusaya amesema Wanachama wa Chama Kikuu cha KACU Ltd wanastahili pongezi nyingi kwa kuwa mazingira hayakuwa rahisi kufufua kiwanda hicho na kuongeza kuwa Vyama Vikuu vingine vinastahili kuiga mfano huo.

Chama Kikuu cha Ushirika cha KACU Ltd kimefanikisha jambo hili baada ya kuandaa mpango biashara kwa ajili ya kufanya shughuli za uchakataji wa pamba ambapo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kupitia mpango huo; Iliridhia kukikopesha Chama hicho, mkopo wa jumla ya shilingi Billioni 4 ili kufanya ukarabati wa kiwanda, ununuzi wa pamba mbegu na uchakataji wa pamba mbegu ili kuzalisha pamba nyuzi na pamba mbegu.

Aidha, Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa Chama Kikuu cha Ushirika cha KACU Ltd kilisajiliwa mwaka 1994 kwa hati ya usajili namba 5,493 ambapo wakati hadi sasa kina jumla ya vyama Wanachama 116 na kwamba kufufua mashine hizo ambazo zilisimama tangu msimu wa kilimo wa mwaka 2013/2014 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uzalishaji mdogo wa pamba pamoja na kushindwa kuhimili ushindani wa makapuni binafsi.

Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa uanzishwaji wa kiwanda hicho; Uende sambamba na ongezeko la uzalishaji wa pamba na tija.

“Ndugu zangu Wanaushirika na Wakulima, ili kiwanda kiendelee kijiendeshe kwa tija ni lazima tuzalishe malighafi za kutosha, maana yake ongezeni uzalishaji wa pamba mara mbili ya uzalishaji wa mwaka huu, na anzeni kwa kutumia mbegu bora, tumieni mbolea na Watumieni Wataalam wote, wakiwepo Maafisa Ugani”.

Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa ili kiwanda kiendelee vizuri ni lazima pamba izalishwe kwa wingi ili kukifanya kiwanda kijiendeshe kwa kipindi cha mwaka mzima.

“Ninyi wote ni mashahidi kuwa baada ya mavuno ya pamba kuisha, viwanda vyetu wa vinafanya kazi kwa kipindi kifupi cha miezi miwili hadi mitatu; Hii si sahihi ni vizuri viwanda vikaongeza usindikaji kwa kipindi kirefu cha mwaka mzima; kuwa na kiwanda kama hiki cha Kahama chenye uwezo mkubwa wa kusindika pamba nyingi zaidi ya kilo elfu 71 kwa siku.” Amekaririwa Katibu Mkuu Kusaya.

Kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata pamba mbegu kilo 68,825 hadi 71,693 kwa siku na kuzalisha robota 144 hadi 150 za pamba nyuzi. Uwezo huo ni mkubwa na ambao unaweza kuchakata pamba zote zinazozalishwa katika mkoa wa Shinyana kwa zaidi ya kilo 6,100,000 kwa msimu mzima.

Katibu Mkuu kusaya ameongeza kuwa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuanzisha, kuendeleza na kufufua viwanda ambavyo vilikua havifanyi kazi kwa muda mrefu na kwamba kuanza kufanyakazi kwa kiwanda hicho ni juhudi ya Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na Benki ya Kilimo (TADB) baada ya kuja na mpango wa kuanza kufufua viwanda vilinavyomilikiwa na Vyama vya Ushirika katika zao la pamba vilivyopo katika Mikoa ya Geita na Shinyanga.

Wakati huo huo Katibu Mkuu ametumia muda huo kutoa onyo kwa Wabadhilifu wote wa mali za ushirika popote nchini kuhakikisha wanarejesha mali za Wanachama wa Ushirika mapema kabla Serikali haijachukua hatua.

Katibu Mkuu Kusaya amesema mali zote zilizoibwa na kuporwa na Viongozi wachache wasio waaminifu, zitarejeshwa kama ambavyo zimeendelea kurejeshwa maeneo mbalimbali kote nchini.

“Nataka niwahakikishie kuwa, kama kuna mali ya ushirika ilichukuliwe isivyo halali; Mali hizo zitarudishwa tu. Nitoe wito kwa Mwananchi yeyote aliyechukua mali ya ushirika isivyo halali popote nchi, atumie wakati huu kurudisha kabla hatujaanza kuchukua hatua kali na katika jambo hili Serikali haitakuwa na huruma.” Amemalizia Katibu Mkuu Kusaya.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com