METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, October 6, 2020

DARASA LA SABA SIMIYU WAAHIDI KUONGOZA MTIHANI WA TAIFA MWAKA 2020

Wanafunzi wa Darasa la Saba katika Shule ya Msingi Somanda A na Somanda B Mjini Bariadi wakipokea mkono wa heri kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakati alipowatembelea shuleni hapo kwa ajili ya kujiridhisha na maandalizi na kuwatakia heri wakati wakielekea katika  Mtihani wa Taifa wanaotarajia kuufanya Oktoba 7-8, 2020.

Mmoja wa Wanafunzi wa Darasa la Saba katika Shule ya Sima A Mjini  akiwaongoza wanafunzi wenzake kwa dua maalum kwa ajili ya kuombe Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba unaotarajiwa kufanyika tarehe 7-8 Oktoba, 2020; (kulia)  waliosimama juu ya meza ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe. Anthony Mtaka akiungana nao katika dua wakati alipowatembelea shuleni hapo Oktoba 05, 2020 kujionea maandalizi na kuwatakia heri katika mtihani huo.

Edina Meshaki mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Sima B Mjini Bariadi, akizungumza namna walivyojiandaa na mtihani wa Taifa unatarajiwa kufanyika Oktoba 07-08, 2020 wakati wa ziara ya viongozi wa mkoa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka iliyolenga kujionea maandalizi yaliyofanyika na kutakia kila la heri katika mtihani huo.

Ikiwa imebaki siku moja kwa wanafunzi wa darasa la saba nchini  kufanya mtihani wa Taifa, wanafunzi wa darasa la saba mkoani Simiyu wamesema wamedhamiria kushika nafasi ya kwanza Kitaifa  katika mtihani huo kutokana na mikakati ya taaluma iliyopo na maandalizi yaliyofanyika, huku wakiahidi pia kutoa wanafunzi kumi bora Kitaifa.

 

Hayo yamebainishwa Oktoba 05, 2020 na baadhi ya wanafunzi wa Shule za msingi Somanda A, Somanda B, Sima A na Sima B za mjini Bariadi wakati wa ziara ya Viongozi wa Mkoa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka katika shule hizo iliyokuwa na lengo la kujiridhisha na maandalizi na kuwatakia heri wanafunzi watakaofanya mtihani huo.

“Tumejiandaa vizuri na mtihani wa Taifa utakaofanyika tarehe 07 na 08 mwezi huu, walimu wetu wametuandaa vizuri tunawashukuru sana walimu kwa kutufundisha vizuri, tulifanya vizuri mtihani wa Mock na tumejipanga kufanya vizuri zaidi mtihani wa Taifa, tunaahidi kutoa wanafunzi watano katika  kumi bora Kitaifa,” Kija Masunga mwanafunzi wa darasa la Saba Somanda B.

“Nawashukuru walimu kwa kutufundisha kutoka chekechea mpaka darasa la saba pia tunashukuru uwepo wa kambi za kitaaluma zimetusaidia sana, baadhi ya wanafunzi katika shule za serikali wanadanganywa na wazazi wao wakaandike majibu yasiyo sahihi ili wakaozeshwe lakini kupitia kambi wanafunzi tunalindwa na tunajiamini,”Edina Meshaki kutoka Sima A.

Aidha, wanafunzi hao wameomba Serikali iendelee kuboresha miundombinu ya kujifunzia ikiwa ni pamoja na uwekaji wa nishati ya umeme katika vyumba vyote vya madarasa ili waweze kujisomea nyakati zote hususani wakati wa kambi za kitaaluma.

Mwalimu Monica Silayo kutoka Shule ya Msingi Somanda B amesema wamewaandaa wanafunzi vizuri ambapo amebainisha kuwa wanafunzi hao wako tayari  kufanya mtihani huo wa Taifa bila wasiwasi wowote.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Sima A, Hamza Hamis amesema “sisi si watu wa maneno ni watu wa vitendo hatuzungumzi mambo mengi lakini tunaahidi kuwa tumejipanga; hili suala la kuwa namba moja tumeliwekea mikakati toka mwaka jana  sasa hivi tunafanya mwendelezo wa mikakati yetu na mwaka huu Simiyu hatukamatiki”.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewashukuru walimu wote wa mkoa wa  Simiyu kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwataka viongozi na watumishi wengine kutoa kipaumbele kwa walimu katika maeneo ya huduma ili wapata nafasi ya kuwafundisha wanafunzi wao .

Kuhusu zawadi kwa wanafunzi na walimu watakaofanya vizuri katika mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka 2020 Mtaka amesema, “wanafunzi watakaoingia 10 Bora kitaifa kila mmoja atapewa shilingi 500,000/= mwalimu atakayeongoza kwa ufaulu wa A nyingi kimkoa katika kila somo atapewa shilingi 500,000/=, shule itakayoingia 10 bora Kitaifa itapewa shilingi milioni tatu, wilaya itakayoingia 10 bora walimu wake wataenda kufanya utalii wa ndani katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.”

Mtaka ameongeza kuwa katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la saba mwaka 2019 wanafunzi mkoa wa Simiyu ulitoa wanafunzi wanne walioingia katika 10 bora Kitaifa kwa shule za Serikali na kila mwanafunzi aliepwa zawadi ya shilingi 300,000/=

Kwa mujibu wa Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju jumla ya wanafunzi 30,779 wanatarajia kufanya mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba, huku akibainisha kuwa maandalizi yako vizuri ambayo yamechangiwa na walimu, wazazi, viongozi na wadau wote wa elimu kwa lengo la kufikia azma ya mkoa ya kushika nambari moja Kitaifa.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com