Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akifungua Mafunzo ya Mfumo Mpya wa HCMIS kwa kundi la kwanza linalojumuisha Maafisa Utumishi Utawala kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro yaliyofanyika leo kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya Mfumo Mpya wa HCMIS kwa kundi la kwanza linalojumuisha Maafisa Utumishi Utawala kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael wakati akifungua Mafunzo hayo leo kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini Dodoma.
Mfumo
mpya wa Taarifa Shirikishi za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) uliotengenezwa na
wataalam wa ndani una uwezo wa kuhifadhi taarifa muhimu za Watumishi wa Umma
tangu kuajiriwa kwao na utatatua changamoto nyingi za kiutumishi ikiwamo ya
madai ya muda mrefu ya malimbikizo ya mishahara.
Hayo
yamesemwa leo na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael wakati akifungua Mafunzo ya Mfumo
Mpya wa HCMIS kwa kundi la kwanza linalojumuisha Maafisa Utumishi Utawala
kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro yaliyofanyika kwenye ukumbi wa
mikutano wa VETA Jijini Dodoma.
Dkt.
Michael amesema Mfumo huo pamoja na kujumuisha taarifa zote muhimu zinazohusu
maendeleo ya Mtumishi wa Umma tangu aajiriwe hadi anapofikia ukomo wa ajira
yake, pia unajumuisha taratibu zote muhimu za kiutendaji katika Utumishi wa
Umma.
“Tofauti
na Mfumo wa Lawson unaotumika hivi sasa,
Mfumo huu mpya unahifadhi taarifa za Miundo ya Taasisi za Umma, Miundo ya
Maendeleo ya Utumishi, Miundo ya Mishahara ya Watumishi, Ikama na Bajeti,
taarifa za Ajira za Watumishi na matukio yote yanayowahusu, malipo ya mishahara
yao, makato ya marupurupu yao kwa kila mwezi na upandishwaji vyeo,” Dkt.
Michael amefafanua.
Dkt.
Michael ameainisha kuwa, Mfumo mpya utaondoa changamoto ya madai ya malimbikizo
ya mshahara ya muda mrefu pindi Mtumishi anapopandishwa cheo, kwani mara baada
ya kupanda cheo, taarifa zake zitabadilishwa kwa wakati ikiwa ni pamoja na
kupata mshahara mpya.
Naibu
Katibu Mkuu huyo amesisitiza kuwa, Mfumo huo uliotengenezwa na wataalam wa
ndani wa Serikali, unaakisi mahitaji ya ndani ya Serikali, utaimarisha usalama
wa taarifa na nyaraka pamoja na kupunguza gharama za matengenezo na ulipiaji
leseni ambapo Serikali ilikuwa ikitumia dola 217,000 kwa mwaka ambazo hivi sasa zitatumika katika miradi ya
maendeleo nchini.
Akizungumza
kwa niaba ya Washiriki wa mafunzo hayo, Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala,
Wilaya ya Kondoa, Bw. Archanus Kilaja, ameipongeza Serikali kutengeneza Mfumo
kwa kutumia wataalam wa ndani, kitendo kinachoashiria nchi yetu imeanza
kujitegemea kwenye eneo la mifumo.
Bw.
Kilaja ameahidi kuyafanyia kazi mafunzo watakayoyapata ili watakaporejea kwenye
maeneo yao ya kazi waweze kuutumia mfumo vizuri kama Serikali ilivyokusudia.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Priscus Kiwango amesema, Mafunzo
yatakayotolewa kwa kundi la kwanza la Maafisa Utumishi na Utawala, yamepewa
muda mrefu wa wiki mbili kwani ndio walengwa wakuu na watumiaji wa mfumo, muda
huo utawawezesha kufahamu vizuri namna mfumo unavyofanya kazi.
Bw,
Kiwango ameongeza kuwa, Mfumo mpya ambao utatumika badala ya Mfumo wa Lawson unaotumika hivi sasa,
umeshafanyiwa majaribio, na Serikali imejiridhisha kwamba uko tayari kwa ajili
ya kuanza kufanya kazi rasmi na utakuwa bora zaidi ya unaotumika sasa.
Maandalizi ya Mfumo Mpya wa HCMIS ulianza mwaka 2018 kwa kukusanya mahitaji ya wadau kutoka kwenye taasisi mbalimbali za Serikali, usanifu na ujenzi wa Mfumo ulianza mwaka 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2020.
0 comments:
Post a Comment