Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel akizungumza jambo mbele ya waandishi wa habari kwenye maonesho ya Tatu ya Teknolojia na Uwekezaji Katika Sekta ya Madini Septemba 17 mkoani Geita.
Baadhi ya Mashine zinazotumika katika shughuli za uchimbaji wa madini zikiwa zimeegeshwa kwa ajili ya Maonesho ya Tatu ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini.
Imeelezwa kwamba ukusanyaji wa mapato yatokanayo na wachimbaji wadogo mkoani Geita umepanda kutoka Tsh. 1,154,192,861.76 Mwaka 2016 na kufikia shilingi 13,948,186,684.80 mwaka 2020 ambayo ni mafanikio yaliyojitokeza mara baada ya kuanzishwa kwa masoko ya madini nchini.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Tatu ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini mkoani Geita yaliyoanza leo tarehe 17 Septemba 2020.
“Tunajivunia kuongezeka kwa mapato na uzalishaji wa dhahabu katika Mkoa wetu wa Geita ambapo mwaka 2016 uzalishaji wa madini ya dhahabu ulikuwa kilo 327, 2017 kilo 832, mwaka 2018 kilo 1634, na baada ya kuanzishwa kwa masoko ya madini mwezi Aprili, 2019 dhahabu ya kilo 4656 ilizalishwa na mwaka huu 2020 zimezalishwa kilo 5591”. Mkuu wa Mkoa Gabriel alisisitiza.
Aliendelea
kusema kuwa, hayo ni mapinduzi makubwa yaliyotokea ndani ya muda mfupi ikiwa ni
ishara ya kuboreka kwa Sekta hii ya Madini nchini katika suala zima la
usimamizi wa rasilimali hii adhimu.
Aidha, Mhandisi Gabriel alieleza kuwa, Maonesho ya mwaka yanayoanza leo tarehe 17 mpaka tarehe 27 Septemba mwaka 2020 ni maalumu kwa ajili ya kusherekea mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye Sekta ya Madini ambapo mapato yatokanayo na madini yamepanda kwa kiwango cha juu.
Ameongeza kuwa, pamoja na kusherehekea mchango wa sekta ya madini kwenye mapato ya mkoa maonesho haya yatasaidia katika kukuza teknolojia ya uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wadogo na kutangaza fursa mbalimbali zilizopo katika mkoa wa Geita.
Akizungumzia juu ya uanzishwaji wa masoko ya Madini, Mhandisi Gabriel amesema kuwa mpaka leo Geita ina masoko 9 ya dhahabu ambayo masoko hayo yameleta matokeo chanya huku nidhamu ya watanzania katika kusimamia na kutumia masoko ikiwa imeongezeka.
Akielezea mafanikio ya Soko la madini la mkoa wa Geita tangu kuanzishwa kwake, Mhandisi Gabriel amesema kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa dhahabu kutoka takribani kilo 100 hadi kilo 200 na zaidi kwa mwezi na kusisitiza kuwa, mwezi wa nane soko la Geita liliuza dhahabu ya kiasi cha shilling Bilioni 58.9.
Wakati
huo huo, Mhandisi Gabriel ametoa pongezi kwa Wizara na Tume ya Madini kwa
kuboresha shughuli na usimamizi makini kwenye Madini na kutoa ushirikiano mzuri
na ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Aidha,Mhandisi
Gabriel amewataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini mkoani Geita
kuyatumia vyema masoko yaliyopo mkoani humo na kuwahakikishia ulinzi katika
masoko yote kwa mkoa wa Geita.
Ameongeza kuwa mji wa Geita uko salama katika mazingira ya aina yoyote na kuwataka wananchi kushiriki katika maonesho hayo bila hofu ya usalama wao, wafike na kutembelea mabanda hayo ili kupata uelewa wa vitu mbalimbali kwani maonesho yameandaliwa kwa ajili ya watu wote.
0 comments:
Post a Comment