Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Philip Chitaunga akizungumza na Wadau wa Utalii wanaotoa huduma za malazi kwa Wageni katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wakati wa mafunzo ya usajili wa Wageni wanaolala kwenye huduma za malazi kupitia mfumo wa MNRT PORTAL yaliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam
Baadhi ya Wadau wa Utalii kati ya 200 wanaotoa huduma za malazi kwa Wageni walioshiriki katika mafunzo kutoka katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wakifuatilia mafunzo ya usajili Wageni wanaolala kwenye Huduma za Malazi zilizosajiliwa na Wizara ya Maliasili kupitia mfumo wa MNRT PORTAL yaliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Wageni wa ndani na nje ya nchi watakaolala kwenye Huduma za Malazi zilizosajiliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mujibu wa sheria kuanzia Oktoba 1, 2020 watatakiwa kuanza kusajiliwa kwenye mfumo wa kielektoniki wa MNRT PORTAL.
Wageni hao watatakiwa kuwa na Vitambulisho vya Taifa( NIDA) au Hati za Kusafiria na wale ambao hawatakuwa na vitambulisho hivyo watasajiliwa kupitia namba za simu au Vitambulisho vya Udereva
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Philip Chitaunga wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja ya Usajili Wageni wanaolala kwenye Huduma za Malazi kupitia mfumo wa kielektoniki wa MNRT PORTAL kwa Wamiliki wa Malazi wapatao 200 wa Kanda ya Pwani.
Amesema lengo kuu la kusajili Wageni hao katika huduma hizo ni kupata taarifa zitakazosaidia Serikali kupata takwimu sahihi kwa ajili ya kuboresha sekta ya Utalii nchini.
Amesema taarifa hizo zitatumika kama nyezo katika kuandaa sera,mikakati na mbinu katika kuboresha sekta ya utalii hasa utalii wa ndani ambao mwamko wake umekuwa mdogo kwa Wananchi
Amesema mfumo huo wa kusajili wageni utatumika katika Mahoteli, Kambi pamoja Loji pekee zinazotambulika na Wizara hiyo
Amesema utaratibu huo wa kusajili Wageni ni takwa la kisheria, Hivyo amewataka Wamiliki wa Malazi hao kuhakikisha kuanzia tarehe 1, Oktoba mwaka huu wanaanza kutekeleza agizo hilo kwa kusajili Wageni wanaofika katika Huduma za malazi kwa kutumia vitambulisho hivyo.
Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi, Chitaunga amewatoa hofu Wamiliki wa malazi kuwa taarifa hizo za Wageni zitatumika kwa ajili ya matumizi ya serikali pekee na zitatunzwa kwa usiri wa hali ya juu.
Kwa upande wake, Samson Nelsa ambaye ni mmiliki wa Huduma za Malazi katika mkoa wa Pwani, amesema mfumo huo utasaidia serikali kuandaa takwimu za idadi ya watalii
Amesema mfumo huo mbali ya kuisaidia Serikali kupata takwimu za utalii wa ndani na wa nje pia utasaidia Wamiliki wa Hoteli kuwa na sehemu salama ya kuhifadhia taarifa zao.
Naye Mohamed Juma ambaye ni mmiliki wa Hoteli ya Rainbow licha ya kuipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutaka kuwa na takwimu halisi za watalii kupitia mfumo huo utakaoanza kutumika mwezi ujao ameitaka Wizara hiyo kuwa ihakikishe hakuna taarifa za wateja wao zinatumika kwa ajili ya maslahi binafsi
Aidha, Ameitahadhalisha Wizara kuwa makini katika kuulinda mfumo huo ili usiweze kushambuliwa na baadhi ya watu kwa ajili ya maslahi yao binafsi.
0 comments:
Post a Comment