Viongozi mbalimbali mkoani Rukwa wamejitokeza kuwahamasisha wananchi mkoani humo kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa mkoa huo itakayochezwa katika Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga kati ya timu ya Tanzania Prison iliyohamishia makazi yake mjini Sumbawanga dhidi ya timu ya Namungo yenye makazi yake Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi.
Wakiongea katika nyakati mbali mbali pindi walipotembelea kuona maandalizi ya uwanja huo kwaajili ya mechi hiyo wamesema kuwa hakika mechi hiyo itakuwa ni ya kihistoria katika mkoa wa Rukwa ambao hakuna timu hata moja ambayo imeshawahi kushiriki ligi kuu kwa Zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Akiongea kwa niaba ya kamati maalum ya Mkoa inayoshughulika na kuilea timu katika Mkoa huo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Chrisant Mzindakaya aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo ambayo kwa sasa ndio timu ya nyumbani kwa watu wa mkoa huo.
“Timu hii ni mali yetu, si ya magereza tena, kwa jina timu ya magereza lakini kwa vitendo ni timu ya mkoa huu wa Rukwa itakuwa hapa siku zote, tutakuwa nao siku zote, mpira ambao utacheza keshi ni na Namungo, Namungo haiwezi kuwashinda magereza, lakini kubwa kuliko yote ni ninyi wananchi wa Sumbawanga hap ana vitongoji vyote mfike mshuhudie mchezo mzuri utaofanyika hapo kesho, tunaamini kiwango kilichowekwa cha kuingia hapa uwanjani ni cha kusaidia watu wengi muingie,” Alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Rukwa Blasi Kiondo aliwaalika wadau wote wa mpira wa ndani ya mkoa na wilaya zake pamoja na mikoa ya jirani ikiwemo Mkoa wa Songwe na Katavi kufika katika Uwanja wa Nelson Mandela kushuhudia mpamabano huo na kuongeza kuwa kutakuwa na mechi ya utangulizi ya vijana chini ya miaka 17 itakayoanza saa 5 mchana kabla ya mechi hiyo ya ligi kuu.
“Kiingilio chetu ni rahisi sana, tumeweka kiingilio cha Shilingi Elfu tatu kwa mzunguko wa uwanja mzima na tumeweka shilingi elfu saba kwa VIP, na nitangazie wanachi wote kuwa kuingia mapema ni vizuri Zaidi kwasababu kutakuwa na mechi chini ya umri wa miaka 17 itakayoanza saa tano mpaka saa sita mchana,” Alisema.
Kwa upande wake Katibu mkuu wa Tanzania Prisons Jabu Adam Kifukwe aliwahakikishia wadau wote wa mpira mkoani humo kuwa timu yao imejiandaa vyema kwaajili ya mechi hiyo ya nyumbani na wasiwe na shaka juu ya wachezaji kwamba wote wapo katika afya njema na hakuna mwenye majeraha na kuomba wananchi wajitokeze kwa wingi katika kuishangilia timu hiyo.
“Waje watupe support, kwamba bila ya wao sisi tunajua kwamba wao ndio wachezaji namba 12 wanaipa Support kubwa waje waiunge mkono timu yao, tupo nyuma yao watuongoze tuweze kushinda mechi hii,” Alimalizia.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa ACP Justin Masejo amewahakikishia wananchi ulinzi na usalama kuanzia maandalizi ya mechi hiyo, kuanza kwa mechi hadi kumalizika kwake.
0 comments:
Post a Comment