Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na wazee wa Kijiji cha Likarangilo alipotembela katika zahanati na kukagua shughuli za masuala ya Lishe wakati wa kuadhimisha siku ya lishe kijijini hapo, Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma Agosti 20, 2020.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akimpima uzito mmoja wa watoto waliohudhuria katika maadhimisho ya siku ya lishe katika kijiji cha Likarangilo kilichopo Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, wakati wa kukagua utekelezaji wa afua za lishe katika mkoa huo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akimkabidhi cheti cha kuzaliwa mkazi wa kijiji cha Likarangilo mama Taufiq Hashim wakati wa zoezi la kukagua utekelazaji wa shughuli za afua za lishe katika jijini hicho kilichopo Wilaya ya Madaba Mkoani Songea.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameiasa jamii kuendelea kutumia vyakula vya asili ili kuwa na afya bora na kuondokana na magonjwa yatokanayo na lishe duni.
Ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Lishe unaoratibiwa na Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali chini ya ofisi yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya lishe.Ziara hiyo iliyofanyika tarehe 20 Agosti, 2020 katika Halmashari ya Wilaya ya Songea pamoja na kutembelea zahanati ya Likarangilo iliyopo Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma katika kuadhimisha siku ya lishe kijijini hapo.
Waziri Mhagama amesema kuwa, uwepo wa vyakula vya asili ni muhimu sana katika jamii zetu kwa kuzingatia vina virutubisho muhimu vya kuimarisha afya kwani hupatikana katika mazingira yanayozunguka na ni vyakula visivyo na madhara kwa wengi.
Alieleza uwepo wa lishe bora unachangia kuchagiza maendeleo kwa jamii zetu kwa kuzingatia kuwa kila kundi linahitaji kula chakula bora katika kuhakikisha afya zinaimarika ili kushiriki katika shughuli za maendeleo.
“Makundi yote ikiwemo, watoto, vijana na wazee yanahitaji kula mlo kamili na kwa wakati kwani changamoto za ukosefu wa lishe bora husababisha kudhorotesha shughuli za maendeleo,”
Waziri aliongezea kuwa, miongoni mwa changamoto zinakabili utekelezaji wa masuala ya lishe nchini ni mitazamo hasi juu ya baadhi ya vyakula na kuona vimepitwa na wakati pamoja na ukosefu wa elimu ya afya kwa wanajamii na kuona masuala hayo ni ya makundi na matabaka Fulani.
“Tupambane kuhakikisha kila mwananchi anawajibika katika kubadili mtazamo juu ya utumiaji wa vyakula vya asili na kuondokana na hali ya kubeza vyakula hivyo na hii ianze na mtu binafsi, familia, jamii kisha taifa kwa ujumla, “alisema Waziri Mhagama
Waziri aliiasa jamii kuwa na bidii na kuendelea kudumisha desturi zililopo katika jamii na kuwakumbusha kushiriki katika shughuli za kilimo na ufugaji wa wanyama, ndege, samaki ili kujipatia vyakula vitokanavyo na uzalishaji huo.
“Ni muhimu kudumisha mila na desturi zetu kwa kuhakikisha tunakula vyakula vya asili na tuondokane na vyakula vya kisasa vyenye kutumia kemikali nyingi, hebu tuanze kula vyakula vyetu vya asili ikiwemo wadudu na vyakula vya mbogamboga vinavyopatikana katika jamii zetu kwa mfano hapa Songea kuna viyenje, senene, mangatungu, liderere, kisamvu, nyeng’enya, chikandi, uyoga, mahungu, pulika na simbilisi tuvitumie bila kuvipuuza, ”alisema Waziri Mhagama
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Mhe. Pilolet Kamando alieleza furaha yake kwa kutembelewa na Waziri, na kuendelea kuahidi kushughulikia maelekezo na maagizo ya kuhakikisha elimu ya masuala ya afua za lishe yanatolewa kwa jamii ili kuondokana na changamoto ya udumavu kwa watoto na magonjwa mengine yatokanayo na ukosefu wa lishe bora.
Alieleza pia Mkoa umeendelea kupambana na masuala ya lishe kwa kutoa elimu kwa Watendaji wa Vijiji, Kata na wahudumu wa afya, kuhakikisha elimu ya kubadili tabia inatolewa ili jamii iwe katika hali nzuri katika masuala ya lisha.
“kumekuwa na mikakati mingi ya kuhakikisha jamii zinaendelea kula vyakula vyenye tija, na hili lipo ndani ya uwezo wetu na tutaendelea kuvitumia vyombo vya habari kwa kuhakikisha masuala ya lishe yanakuwa ni ajenda ya kila siku,”alisema Mhe. Kamando.
Aliongeea kuwa, Mkoa umeendelea kusimamia na kutenga bajeti ya kusaidia usimamizi wa afua za lishe na hii imesaidia kupiga hatua na kupungua kwa hali ya udumavu kutoka asilimia 44 hadi 41.
0 comments:
Post a Comment