Hayo yamebainika Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya uboreshaji makazi uliofanywa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. John Jingu.
Akizungumza katika Uzinduzi huo, Katibu Mkuu Dkt. Jingu amesema baada ya kutembelea makazi ya watu walioboresha makazi na kushuhudia uboreshaji wa makazi hayo ambapo wananchi kwa asilimia kubwa wameweza kuchukua hatua ya kuboresha makazi yao.
Aidha amewataka watanzania katika maeneo mengine nchini kuiga wanavikundi wa Kata ya Koromije kutumia mfano huo kuleta mabadiliko katika maisha yao ikiwa ni namna bora zaidi ya kuweza kujikwamua kutoka katika hali duni.
“Katika maeneo yote tumeshuhudia dhana ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na hali hii imeimarisha familia Ustawi na maendeleo na katika kuratibu mwongozo wa makazi bora hapa maafisa Maendeleo ya Jamii wafanye kazi kuhamasisha jamii, kuboresha makazi yao”
Dkt. Jingu amesisitiza kuwa mchango wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali ni muhimu sana katika Kampeni hiyo kwa kushirikiana na Serikali kuleta maendeleo ya wananchi hivyo Asasi za kiraia zione umuhimu wa kuunga Mkono juhudi za Serikali katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda amewahimiza viongozi katika ngazi mbalimbali kuhamasisha Kampeni ya ujenzi wa makazi bora ili kuchochea maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Naye mmoja ya wafaidika wa Kampeni ya Kuboresha Makazi Bi Joyce Lupemba amesema mwanzo walikua wakiishi katika mazingira duni wakilala pamoja mifugo pamoja ila baada ya kuboresha makazi wamekuwa wakiishi na kulala sehemu salama.
“Tulikuwa tukisumbuliwa na wadudu wakiwemo chawa na kunguni, lakini kwa sasa wamejenga nyumba zinazowezesha kuishi kwa raha lakini pia nyumba bora zinasaidia katika malezi ya watoto”alisisitiza
“Mimi na familia tulikuwa tukilala katika nyumba ya tembe iliyoezekwa kwa nyasi huku nyumba hiyo hiyo ikitumika kama zizi la Mifugo, jambo lililochagia maambukizi ya magonjwa mbalimbali hasa kwa watoto” alisema
Aidha Shuhuda mwingine Bw. Tano Kakunga ameiomba Serikali kuboresha utoaji wa mikopo kwa vikundi ili waweze kuendelea kuboresha makazi zaidi hasa kwa kuwa na maji na umeme wa uhakika.
“Tulikuwa tukiishi katika nyumba za nyasi na udongo ilitulazimu kutolala nyakati za usiku mvua inaponyesha tukihofia nyumba zetu kubomoka na kujaa maji ndani” alibainisha
Kampeni ya kuboresha makazi inaenda na Kauli Mbiu Piga Kazi, Boresha Makazi, inayoenda sambamba na kauli mbiu ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi tu hivyo kauli ikiakisi mwelekeo wa kubadilisha hali duni na kuwa na maisha mazuri.
0 comments:
Post a Comment