Katika kuendeleza na kukuza amani, upendo, mshikamano na kudumisha umoja kwa wasanii wanaoigiza maarufu kama “Bongo Movie” pamoja na wasanii waimbaji maarufu kama “Bongo Fleva”, Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa Kiheka Charles amezikutanisha timu za makundi hayo mawili katika mechi ya mpira wa miguu iliyopigwa katika viwanja vya shule ya sekondari Mazwi mjini Sumbawanga.
Kiheka alisema kuwa miongoni mwa malengo ya kufanya hivyo ni kuendelea kuhamasisha michezo ndani ya mji wa Sumbawanga kwani wasanii ni kioo cha jamii na kupitia wao huenda wananchi wakahamasika kuishiriki kwenye mazoezi mbalimbali na hatimae kupelekea kuimarika kwa afya zao.
Aidha, aliwaomba wadau mbalimbali wa michezo na sanaa ndani ya mkoa wa Rukwa kujitokeza na kuendelea kuwasaidia wasanii ili waweze kufanikiwa katika malengo yao na hatimae vijana hao kuweza kujiajiri na kupunguza utegemezi katika familia zao na kuongeza kuwa kazi ya serikali ni kuendelea kuihamasisha jamii ili iweze kujitoa kwenye michezo.
“Michezo ni Afya, Sanaa ina kazi ya kuelimisha na kuburudisha, sanaa huifanya jamii kuwa kitu kimoja, na michezo pia huifanya jamii kuwa kitu kimoja na tunashirikiana katika mambo mbalimbali hasa katika kutangaza kampeni zetu mbalimbali za kimaendeleo, kutangaza fursa zinazopatikana ndani ya manispaa yetu ya Sumbawanga na tukifanya vizuri, unajua ile sumbawanga iliyokuwa inasifika zamani ile sifa itapotea, nadhani wenye mnaona watu wakija kutoka mbali wanaona tofauti na walivyokuwa wanafikiria,” Alisema.
Kwa upande wao washiriki wa mchezo huo waliishukuru Ofisi ya Mkurugenzi Manispaa ya Sumbawanga kwa uratibu wa mchezo huo uliofanywa na afisa utamaduni wa manispaa hiyo huku wakiendelea kusisitiza wadau wengine wajitokeze katika kukuza michezo kwani michezo huleta furaha katika jamii.
Pia kapteni wa timu ya Bongo fleva Steven Stanley a.k.a Young Steve alimpongeza Afisa utamaduni huyo kwa juhudi za kuwakutanisha wasanii pamoja, “Michezo inakutanisha watu, inaleta furaha, amani, tunakutana watu mbalimbali tunajuana na labda nimpongeze Afisa utamaduni kwa hii ishu aliyoianzisha kwasababu ni ishu moja nzuri sana, kwasababu tumeanza na hii hapa tumecheza bongo fleva na bongo movie kesho nadhani kutakuwa na ishu nyingine tena,” Alisema.
Nae kocha wa Bongo Movie Juvenile Mwananjela aliwaomba wadau mbalimbali wanaotafuta vipaji vya wacheza mpira wa miguu wajisogeze kwenye mechi za mitaani ili kuweza kuona vipaji kwani wenye vipaji ni wengi na pia aliendelea kumuomba Afisa utamaduni kupitia ofisi ya Mkurugenzi kuendelea kuunga mkono vipaji vilivyopo mitaani.
Hadi mechi hiyo inakwisha timu ya bongo fleva walipewa ushindi dakika 15 kabla ya mpira kuisha baada ya timu ya bongo movie kukataa penati waliyodai hayakuwa maamuzi sahihi na hatimae kutoka nje ya uwanja wakati wakiwa sare ya mabao 3 kwa 3 na mshindi wa mechi hiyo alipewa mbuzi.
0 comments:
Post a Comment