METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, July 28, 2020

‘TUSHIKAMANE HATA BAADA YA KURA ZA MAONI’ KATIBU CCM MKOA MWANZA



Wagombea wa nafasi za uchaguzi wa udiwani wa viti maalum wilaya ya Ilemela mkoa wa Mwanza (UWT) wametakiwa kudumisha mshikamano, upendo na umoja katika kipindi cha mchakato wa kura za maoni ili kupata wawakilishi watakaopeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu na wale watakaokosa nafasi waaswa kuwaunga mkono watakaoteuliwa na vikao vya chama hicho.

Rai hiyo imetolewa na katibu wa CCM mkoa wa Mwanza, Comred Julius Peter wakati akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi huo uliofanyika katika viwanja vya CCM Kirumba ili kuchagua wawakilishi Saba watakaoungana na madiwani wa kata 19 za manispaa ya Ilemela ili kuchuana na vyama vyengine kabla ya kupata fursa ya kuwa wajumbe wa baraza la madiwani ambapo amesema kuwa hakuna mwenye hati miliki na chama hicho na kuwa wanachama wote wana fursa sawa ya kugombea na kuchaguliwa huku akiwasisitiza kuvunja makundi na kuepuka mpasuko baada ya uchaguzi huo

‘.. Wagombea tuendelee kudumisha umoja, upendo na mshikamano, Hiki chama ni cha kila mwana chama, Mnaogombea mpo 87 nafasi ni moja ..’ Alisema

Aidha Katibu huyo amesisitiza juu ya kuwepo kwa uwazi wakati wa zoezi la uchaguzi na kuzingatia haki ili kuepusha changamoto zisizo za msingi zinazoweza kujitokeza ikiwemo vurugu na mpasuko.

Akimkaribisha mgeni huyo, katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Bi Aziza Isimbula akasema kuwa wilaya yake inaendelea vizuri na taratibu za uchaguzi huku akimhakikishia ushindi kwa chama hicho mara baada ya kuisha kwa mchakato wa kura za maoni na kuwapata wagombea watakaoteuliwa na vikao kuwakilisha chama hicho.

Nae katibu wa jumuiya ya wanawake (UWT) wilaya ya Ilemela Bi Salama Mhapi akasema kuwa katika uchaguzi huo,  Idadi ya wapiga kura ni 329 na idadi ya wagombea ni 89 huku wajumbe 3 wakishindwa kuhudhuria mkutano huo ambapo mgombea aliyepata kura nyingi ni Bi  Sarah Lisso alipata kura 205, Bi Kuruthumu Ramadhan alipata kura 146, Bi Safia Mkama alipata kura 152, Bi Rahma Hilal alipata kura 139, Bi Leah Kisandu alipata kura 61, Bi Sarah Manyama alipata kura 86 na  Bi Marietha Masenhelo aliepata kura 77.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com