Serikali
kupitia Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), kwa kushirikiana na halmashauri
mbalimbali nchini ambako zao la mkonge linalimwa imesema itaanzisha vitalu vya
zao hilo ili kuwawezesha wananchi kupata mbegu baada ya kuwepo na mwamko wa
wananchi kutaka kulima zao hilo.
Akizungumza
katika Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA),
Afisa Maendeleo ya Masoko wa Bodi ya Mkonge Tanzania, David Maghali alisema
kuwa mwamko wa wakulima kulima zao hilo sasa ni mkubwa ndiyo maana Serikali
imefikia uamuzi wa kuzalisha miche mingi ili kuwawezesha wananchi kupata fursa
katika kilimo cha zao hilo.
“Mwamko
wa kuongezeka kwa wakulima wa zao la Mkonge kumekuja baada ya kuongezeka kwa
matumizi ya zao hilo hasa kwenye sekta ya ujenzi, kwani mkonge hutumika
kutengeneza gypsam na vifaa vya Magari kwa hiyo mahitaji yake yamekuwa
yakiongezeka siku hadi siku”, Alisema Maghali.
Alisema
kuwa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam(SABASABA), yameleta
mwamko mkubwa wa wananchi wengi kujua na kujifunza fursa zilizoko kwenye zao la
mkonge, ikiwemo kupata elimu juu ya kulima zao hilo, uvunaji wa zao hilo, ajira
zinazoweza kutengenezwa katika zao hilo na matumizi ya zao hilo ambayo kwa sasa
ni makubwa duniani, lakini pia wameweza kujifunza bidhaa mpya, matumizi mapya
na fursa za uwekezaji viwanda katika eneo hilo.
Aidha Maghali
aliongeza kuwa Bodi ya Mkonge Tanzania iko tayari kuwahudumia wananchi katika
maeneo mbalimbali ambako zao la mkonge linalimwa, kwa kushirikiana na
Halmashauri TSB inaendesha zoezi ya kutengeneza vitalu ili kurahisisha
upatikanaji wa miche kwa wananchi wenye
uhitaji kupata miche hiyo kwa urahisi.
Kwa
Upande wake Afisa Mipango wa TSB, Fredrick Sospeter alisema kuwa zao la Mkonge
lina fursa nyingi na linadumu kwa muda mrefu ambapo linamuwezesha mkulima
kuvuna kwa miaka 12 mara mbili kwa mwaka baada ya kupanda na kuanza mavuno
baada ya miaka mitatu.
“Ulimaji
mkonge ni mzuri kwa sababu zao hili linakomaa kwa muda wa miaka mitatu na baada
ya hapo mavuno yake yanachukua hadi muda wa miaka 12 kwa mkulima akiwa anavuna
mara mbili kwa mwaka, maana yake akiwa anavuna baada ya miezi sita”,
Alieleza
kuwa zao hilo lina faida nyingi sana ikiwemo
mizizi yake ambayo hutumika kutengenezea madawa ya binadamu, mifugo na
mimea, shina ambalo hutumika kutenegeneza juisi yenye sukari (asali) ambayo
hutumiwa kwa wingi na wagonjwa wenye matatizo ya kisukari.
Vilevile
majani ya mkonge hutumika kutengenezea nyuzi, Kamba, mazulia, magunia, Gypsam,
karatasi za kutengenezea fedha(noti), gesi, mbolea pamoja na chakula cha
wanyama.
“Zao la
Mkonge lina fursa nyingi kwa hiyo wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi
karibuni muwekeze katika viwanda vya kutengeneza madawa ya binadamu, mifugo,
mimea, juisi yenye sukari (asali), nyuzi, Kamba, mazulia, magunia, Gypsam,
karatasi za kutengenezea fedha(noti), gesi, mbolea pamoja na chakula cha
wanyama ili kujenga uchumi mzuri kwa wananchi kupata ajira na wengine kulima
zao hili”, Alisema Sospeter.
0 comments:
Post a Comment