METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, November 6, 2018

Mongella apokea magari kutoka AGPAHI, asisitiza matumizi sahihi

Na George Binagi-GB Pazzo
Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe. John Mongella amepokea magari mawili aina ya Nissan Patrol yenye thamani ya shilingi Milioni 186, kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za afya hususani mapambano vya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi katika Halmashauri za Misungwi na Buchosa.
 
Magari hayo yametolewa na shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Health Initiative (AGPAHI) linalosaidia mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, kwa ufadhili wa watu wa Marekani kupitia Mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana na Ukimwi (PEPFAR) chini ya vituo vya kudhibiti magonjwa na kinga (CDC).

Akipokea magari hayo jana kwenye kikao cha wadau wa afya na ustawi wa jamii mkoani Mwanza, Mongella alisisitiza kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa na kuonya kwamba watakaothubutu kuyatumia kwa matumisi yasiyo sahihi hatua zitachukuliwa dhidi yao.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa alisema shirika hilo limekuwa likifanya kazi kwa karibu na halmashauri ili kuboresha huduma za afya na kwamba katika kipindi cha kuanzia mwezi Oktoba 2017 hadi Septemba 2018, shirika hilo limefanya ukarabati wa Vituo 146 vya kutolea huduma vikiwemo 36 mkoani Mwanza huku Vituo 40 vikiwekewa mfumo wa umeme jua (Solar).

Katika kuboresha huduma za afya, alisema shirika hilo limenunua vyombo vya usafiri ikiwemo magari, pikipiki na baiskeli vyenye thamani ya shilingi Milioni 900.2 kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za VVU/ UKIMWI katika mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga pamoja na Mara.
Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe. John Mongella (wa pili kulia) akikata utepe kuashiria makabidhiano ya magari hayo. Wengine ni Mkurugenzi Halmashauri ya Misungwi, Kisena Mabuba (kushoto), Mkuu wa Wilaya Misungwi, Mhe. Juma Sweda (wa pili kushoto) pamoja na Mwenyekiti Halmashauri ya Misungwi, Antony Bahebe (kulia).
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhe. John Mongella akizungumza kwenye kikao cha wadau wa afya mkoani Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji shirika la AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa afya mkoani Mwanza.
Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza, Dkt. Thomas Rutachunzibwa akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa afya mkoani Mwanza.
Mkuu wa Wilaya Nyamagana Mhe. Dkt. Philis Nyimbi (kushoto), Mkurugenzi Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba pamoja na Kaimu Meya Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha wakipokea Microscope kusaidia utoaji huduma za afya.
Mkurugenzi Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, John Wanga akionesha "Microscope" aliyopokea kwa ajili ya kusaidia utoaji wa huduma za afya katika Manispaa hiyo.
Tazama Video hapa chini
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com