Muonekano
wa Kituo cha kuuza mafuta ya Petroli na Dizeli cha serikali (TANOIL)kitakachosimamiwa
na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC) kupitia Kampuni ya Mafuta
ya TANOIL, kilichofunguliwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Juni 06, 2020
wilayani Musoma mkoani Mara.
Waziri wa
Nishati, Dkt Medard Kalemani( wa tatu kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Nishati,
Mhandisi Zena Said( kushoto), Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu( pili
kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima( katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika la Mendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC) Dkt. James Mataragio (wa tatu
kulia) na Viongozi wa Waandamizi wa Wizara ya Nishati na taasisi zake, Viongozi
wa Serikali ya Mkoa wa Mara wakikata utepe kuashiria ufunguzi wa kituo cha
kuuza mafuta ya Dizeli na Petroli cha serikali( TANOIL) kitakachosimamiwa na Shirika
la Maendeleo ya Petroli Tanzania( TPDC) kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANCOIL,
kilichofunguliwa na Waziri huyo , Juni 06, 2020
wilayani Musoma mkoani Mara.
Waziri wa
Nishati, Dkt Medard Kalemani akikata sili katika gari iliyobeba mafuta, ili
kufungua koki kuruhusu mafuta kuingia katika matanki ya kuhifadhi mafuta ya
kituo cha kuuza mafuta ya Petroli na Dizeli cha TANCOIL,alipozindua rasmi
biashara ya mafuta katika kituo hicho kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo
ya Petroli Tanzania( TPDC) kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANCOIL,
kilichofunguliwa na Waziri huyo , Juni 06, 2020
wilayani Musoma mkoani Mara.
Waziri wa
Nishati, Dkt Medard Kalemani( katikati) akiwa katika picha ya pamoja na
Viongozi wa Waandamizi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake, Viongozi wa
Serikali ya Mkoa wa Mara baada ya ufunguzi wa kituo cha kuuza mafuta ya Dizeli
na Petroli cha serikali( TANOIL) kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania( TPDC) kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANCOIL, kilichofunguliwa
na Waziri huyo , Juni 06, 2020 wilayani
Musoma mkoani Mara.
Waziri wa
Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Mara
wakati akifungua rasmi biashara ya
mafuta katika kituo cha kuuza mafuta ya Dizeli na Petroli cha serikali(TANOIL)
kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania( TPDC) kupitia
Kampuni ya Mafuta ya TANOIL, Juni 06, 2020,
wilayani Musoma mkoani Mara.
Waziri wa
Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua rasmi biashara ya kuuza na kusambaza
mafuta nchini kwa kufungua kituo cha kwanza kuuza mafuta ya Petroli na
Dizeli cha Serikali kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini
(TPDC) kupitia Kampuni yake Tanzu ya Mafuta ( TANCOIL).
Aidha Dkt.
Kalemani alisema kuwa kuzinduliwa na kufunguliwa kwa biashara hiyo ni kutimiza
azma na nia njema ya Serikali ya kuboresha shirika lake la TPDC,kuwapatia na
kuwasogezea karibu wananchi wake huduma ya kupata mafuta yenye viwango vya
ubora unaotakiwa, bei nafuu, na yatakayopatikana kwa wingi muda wote.
Dkt.
Kalemani alifanya Uzinduzi huo pamoja na kufungua kituo hicho wilayani Musoma,
mkoani Mara Juni 6, 2020, wakati wa
ziara yake ya kikazi katika Mkoa huo,
akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa
Nishati Subira Mgalu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said
pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Wizara hiyo na Taasisi zilizochini
yake.
Alisema
baada ya kuanza rasmi kwa biashara hiyo, TPDC kupitia TANCOIL itashirikiana na
Halmashauri zote nchini kuhakikisha inafanikisha azma ya Serikali ya kufungua
na kuweka vituo vya kuuza na kusambaza mafuta katika kila halmashauri nchini
pamoja na miundombinu ya kuhifadhi na kusafirisha mafuta.
“Tumeshaanza
biashara ya kuwauzia wananchi wetu mafuta, sitegemei kusikia mafuta yanauzwa
kwa bei aghali katika vituo vya serikali, TPDC na TANCOIL mnielewe vizuri
hapa! hii haipo na haitakuwepo, lengo
letu sisi serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wapata bidhaa bora za mafuta
kwa kiwango kinachotakiwa, kwa bei nafuu
na yatapatikana kwa wingi wakati wote na huduma hii inapatikani jirani na maeneo yao!,”Alisema Dkt. Kalemani.
Dkt.
Kalemani aliwaeleza watanzania kuwa TPDC na TANOIL watashiriki katika biashara
ya uagizaji na usambazaji mafuta kama zinavyofanya kampuni zingine za mafuta
nchini ili kuongeza ushindani na kutanua wigo wa kampuni za kizalendo
kushiriki katika biashara ya mafuta,
ambayo kwa sasa inafanywa na makampuni
kutoka nje ya nchi tu.
Alisema
kuwa serikali kupitia TPDC itajenga vituo 100 kwa kipindi cha miaka 5 ijayo,
tayari baadhi ya Halmashauri zimeanza kutenga maeneo yatakayojengwa vituo
hivyo: Aidha itahakikisha kuwa nusu ya mafuta yote yanayoingizwa nchini
yanasimamiwa TPDC.
“Watanzania
tutembee kufua mbele na kujivunia vilivyo vya kwetu! Uzinduzi wa biashara hii
ya mafuta hapa Musoma leo unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, ya Uongozi
wa Rais Dkt. John Magufuli, ni kutambua juhudi na mchango mkubwa wa Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kuimarisha sekta ya Umma ya
kukuza uchumi, pia hatuna budi kutambua mchango wake wa kuanzisha TPDC mwaka
1969 pamoja na kiwanda cha kusafisha mafuta cha TIPER mwaka huohuo, ambapo TPDC
ilimiliki kiwanda hicho kwa asilimia 50%, mwalimu aliona na kuwaza mbali sana,
hii yote ni katika dhana ya kujitegemea kiuchumi,”. Alisisitiza Dkt. Kalemani.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi wa Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini, (TPDC),
Dkt. James Mataragio alisema kuwa katika kutekeleza azma hiyo ya serikali,
kuanzia mwaka huu wa fedha 2020/2021, TPDC imetenga fedha za kutosha kwa ajili
ya mtaji wa kugharamia shughuli za uagizaji, usambazaji na usimamizi wa mauzo
ya mafuta nchini kote.
Dkt.
Matagio, alisema kwamba TANOIL imejipanga kuhakikisha kuwa, kunakua na usalama
wa usambazaji mafuta nchini yaani (security of supply), kunapatikana
takwimu sahihi za mafuta, bei na viwango stahiki vya ubora, pamoja na uelewa
mzuri na mpana wa biashara ya mafuta nchini.
“Ninafuraha
sana leo TPDC inaandika historia mpya na kubwa sana katika nchi yetu,
tunaungana na wakazi wa Mkoa wa Mara, kwa niaba ya watanzania wote kuonyesha
furaha yetu katika kuandika historia hii mpya ya kwamba shirika letu na
maendeleo ya Mafuta, (TPDC) linarudi kwa kishindo katika biashara ya kuuza na
kusambaza wa mafuta ya Petroli, Dizeli na bidhaa zake kwa maslahi yetu sote na
taifa kwa ujumla”, Alisema Dkt. Mataragio.
Alieleza
zaidi kuwa Mwaka 2000, Serikali ilifanya maamuzi ya kuendesha biashara ya
mafuta nchini kwa mfumo wa soko huria, hivyo TPDC ikaunda kampuni tanzu ya
COPEC kuweza kuingia katika mfumo huo na kushiriki katika soko la ushindani
katika biashara hiyo.
TPDC ilinunua
na kujenga vituo mbali mbali nchini vikiwemo Segera na Muheza Mkoani Tanga,
Makuyuni na Makumira Mkoani Arusha, Singida, Geita, pamoja Mkoani Mara ambapo
vilinunuliwa vituo viwili tu cha Musoma na Tarime, vituo vyote hivyo
vinamilikiwa na TPDC kwa asilimia mia moja(100% ).
Dkt.
alisema kuwa TPDC ilishiriki katika biashara hiyo kupitia katika vituo
hivyo,hata hivyo kukosekana kwa Sheria madhubuti ya Mafuta/Petroli, kulififisha
ushiriki wa TPDC katika soko lenye ushindani mkubwa.
Aliweka
wazi kuwa baada ya kufanyika kwa michakato na mapitio ya rejea , maboresho
mbalimbali ya shirika hilo pamoja na mambo mengine, kumewezesha Uwepo wa Sheria
madhubuti, pamoja na usimamizi wa kanuni mbalimbali, ambazo sasa unaiwezesha
TPDC kuingia katika soko kwa ufanisi zaidi.
Sheria ya
Mafuta ya Mwaka 2015 imeipa TPDC hadhi ya kuwa Shirika la Mafuta la Taifa (NOC)
ili kujiendesha kibiashara, kupitia Sheria hiyo, TPDC imeimarisha kampuni zake
Tanzu za GASCO na TANOIL. Awali, TANOIL ilikuwa COPEC. Kampuni ya GASCO inajishughulisha
na biashara ya gesi na TANOIL inajishughulisha na biashara ya mafuta, ambayo
ndiyo biashara tunayoizindua leo Kitaifa.
Katika
mwaka huu wa fedha, TPDC itakamilisha ujenzi wa vituo viwili katika Mkoa wa
Singida na Mkoa wa Geita. Aidha, TPDC inaendelea na mkakati wa kutwaa ardhi
katika mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Dodoma na Morogoro. Hatua za utwaaji
ardhi katika mikoa ya Dodoma na Tanga zipo katika hatua za ukamilishaji.
“Natumia
fursa hii kwa niaba ya TPDC kutoa shukrani zetu za dhati kwa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Nishati unayoiongoza wewe
Dkt. Kalemani kwa umahiri, kwa maelekezo na rasilimali fedha zinazoiwezesha
TPDC sasa kuingia katika biashara hii, pia Serikali ya Mkoa wa Mara kwa
ushirikiano waliotupatia kwa muda wote tangu enzi za COPEC hadi sasa tunapokuwa
TANOIL na kufungua ukurasa mpya wa mafanikio ya uzinduzi wa biashara ya
mafuta”, Alisema Dkt. Mataragio.
Naye Mkuu
wa Mkoa, Adam Malima, aliwaasa wakazi wa wafanyabiashara na watumia wa mafuta
ya Petroli na Dizeli kuunga mkono juhudi za serikali za kuanzisha bishara ya
mafuta kwa kununua mafuta katika vituo vya serikali.
Sambamba
hilo alisema kuwa kutokana mikakati iliyowekwa na serikali kupitia TPDC na
TANOIL kufikisha huduma ya mafuta hayo karibu na wananchi,kutaweka katika
mazingiza salama na rafiki watumiaji wa mafuta hayo hasa waendesha bodaboda na
wafanyabiashara wadogo.
“Wafanyabiashara
wadogo wanaowauzia waendesha bodabora na vyombo vingine vidogo vinavyotumia
mafuta hayo, wamekuwa wakihifadhi bidhaa hiyo katika hatari kubwa ya kupoteza
maisha na mali zao, wanatumia vifungashio duni kama Galoni na chupa za maji,
kiukweli hii itaondoa kabisa hatari hii iliyopo katika jamii yetu hasa
vijijini”, Alisema Malima.
Historia
inatuonesha kwamba katika miaka ya 80 hadi kufikia Mwaka 2000, TPDC licha ya
biashara yake kuu ya utafutaji, uchimbaji, uendelezaji na usambazaji wa gesi
asilia ilikuwa muagizaji, muingizaji na msambazaji mkuu wa mafuta yote
yaliyotumika nchini.
TPDC
iliingiza mafuta ghafi nchini na kuyasafisha, na pia uingizaji wa ziada ya
mafuta yaliyosafishwa na kutosheleza mahitaji ya mafuta nchini.
Pia TPDC
ilibeba jukumu hilo kwa ufanisi na uzalendo wa hali ya juu, ikiwemo kuwa
msambazaji pekee aliyesambaza mafuta mstari wa mbele wakati wa vita vya Kagera
kati ya Mwaka 1977/78 baada ya makampuni ya binafsi kugoma kupeleka mafuta
Kagera.
0 comments:
Post a Comment