METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, June 8, 2020

MRADI WA MAJI LONGIDO NI MIUJIZA – DKT. MHINA


Tanki la maji lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido, ambalo linakusanya maji kutoka Mto Simba uliopo wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro.

“Tangu Longido kuwa  Wilaya mwaka 2007 haijawahi  kuwa na  huduma maji yanayotiririka kwenye  nyumba za watu, yamekuwepo maji ya visima miaka yote, nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alitupatia fedha kiasi cha shilingi bilioni 15. 89 ambazo zimetekeleza mradi maarufu  unaoitwa mto Simba, ambapo maji yanatoka Mlima Kilimanjaro  sehemu ya  umbali wa kilomita 63 hadi kufika hapa Longido”.


Hayo yanasemwa  na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Longido, Dkt. Jumaa Mhina wakati akizungumza na Afisa Habari kutoka Idara ya Habari – MAELEZO na mwandishi wa makala hii, Immaculate Makilika alipokuwa ziarani huko mkoani Arusha hivi karibuni.

Dkt. Mhina anaendelea kusema kuwa maji yanapofika Longido kutoka Mlima Kilimanjaro yanahifadhiwa kwenye tanki  kubwa  na kusambazwa ndani ya mji wa Longido kwenye mtandao wa Km 44.7 kisha yanaenda katika Kata ya Engikaret umbali wa km 31kwa hiyo huu ni mradi mkubwa kuwahi kutokea na wa kihistoria.

“Hivi sasa tunavyozungumza, wananchi wanachota maji  ya bomba  kwenye nyumba zao, hiyo ilikuwa miujiza hakuna mtu ambaye aliamini kuwa jambo hili linaweza kutokea, lakini jambo hili limetokea”, anasisiza Dkt. Mhina.

Ni dhahiri kuwa  mradi ulilenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji katika Mji wa Longido kutoka asilimia 15 ambayo ni sawa na wakazi 2,510 hadi kufikia asilimia 100 sawa na wakazi 16,712 kwa sasa. Kiasi hicho cha maji kimetosheleza mahitaji kwa asilimia 100 hadi kufikia idadi ya wakazi 26,145 kwa mwaka 2024.

Bi.Winnie Sangau mkazi wa Longido, anasema hapo awali kulikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji, kwani iliwalazimu kwenda kuchota maji sehemu yenye umbali mrefu ambapo ni kwenye kituo kikubwa kilichokuwa kikitoa huduma ya maji mara moja tu kwa wiki tena ambayo hukatika saa nane alasiri, baada ya mradi wa mto Simba kuanza kutoa huduma ya maji hali hiyo imebaki historia ambayo hawatakaa kuisahau maishani mwao kwani yalikuwa mateso makubwa kwa akina mama ambao ndio walionekana na ndoo za maji kila uchao wakihaha kutafuta maji kama swala aliyenusurika kujeruhiwa na nyoka mkubwa!

“Ahaa! hivi sasa upatikanaji wa huduma ya maji ni rahisi, tunapata maji kwenye nyumba zetu na ambao hawajavuta mabomba katika nyumba zao wanachota kwenye vituo vilivyopo karibu na makazi ya watu na maji yanatoka kila siku, kwa kweli tunamshukuru sana Rais Magufuli kwani amebadilisha maisha yetu wakazi wa Longido”, anaongeza Sangau.

Mradi huu wenye uwezo wa kuzalisha maji kiasi cha mita za ujazo 2,160 kwa siku wakati mahitaji ni mita za ujazo 1,462, umefungua fursa mpya za biashara katika wilaya hiyo  muhimu ya Longido ambapo kwa upande wa kaskazini inapakana na nchi jirani ya Kenya, na hivyo suala la maji ni nyenzo muhimu kwa matumizi mbalimbali hasa wakati huu ambao ulimwengu unapamba na virusi vya Corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu huku wengine wakisema hii ni “vita ya tatu ya dunia”.

Akielezea namna ambavyo mradi huo wa maji ya mto Simba umebadilisha maisha ya wanalongido, mwalimu mstaafu, Bw.Charles Msangi anasema  “Kwa sasa maji yanapatikana wakati  wote usipohitaji unafunga, na hivyo sipati shida ya huduma ya maji hapa kwenye biashara yangu ya nyumba ya kulala wageni, namshukuru sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kutukubalia huu mradi amefanya kitu kikubwa sana ambacho watu wa Longido hatutasahau. Wafugaji huko nyuma walipata shida sana kwani walikuwa wakienda kunywesha mifugo siku nzima na mara nyingine ng’ombe hulala huko huko , lakini kwa sasa  hawaendi tena huko kwani watu wengi wana mabomba katika nyumba zao na sehemu za kunyweshea zimewekwa karibu  na makazi ya watu”.

Halikadhalika miujiza ya Longido haikuishia kwenye maji tu, bali hata kwenye mifugo na ukusanyaji wa mapato, hali iliyobadilisha maisha ya wakazi wengi ambao ni wa jamii ya kimasai.

Awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa mnada wa mifugo ulipata fedha za utekelezaji kupitia ufadhali wa programu ya kuendeleza Miundombinu ya Masoko, Ongezeko la Thamani na Huduma za Fedha Vijijini (MIVARF) kwa  asilimia 95 na  Halmashauri ya Wilaya ya Longido ilichangia asilimia 5 ya gharama za mradi kwa awamu ya kwanza.

Utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya mnada wa mifugo ulianza rasmi Novemba 2016 na kugharimu shilingi 782,743,085.59/= ambapo MIVARF imechangia 95% sawa na shilingi 743,605,931.30 na Halmashauri ilichangia asilimia 5 sawa na shilingi 39,137,154.30.

Katika awamu ya pili ya ujenzi wa miundombinu ya mnada huu, Wizara ya Mifugo na Kazi hii ilitoa jumla ya shilingi 150,000,000/= ili kukamilisha ujenzi wake kazi. Hivyo jumla kuu ya gharama za mradi (awamu ya kwanza na awamu ya pili) ni shilingi 932,743,085.59.

Licha ya mradi huo kuwa na manufaa mbalimbali kama vile kuongeza uzalishaji wa mifugo na mazao ya mifugo kutokana na uwepo wa soko la uhakika la mifugo,  kuboresha na kuinua kipato cha wananchi wa Wilaya ya Longido kwa kuuza mifugo ndani ya Tanzania na nchi jirani.

Faida nyingine ni ajira kwa vijana na wanawake, kurahisisha upatikanaji wa mifugo kwa ajili ya kiwanda cha nyama kinachojengwa upande wa pili wa eneo la mnada ambacho kitasindika mbuzi au kondoo 2,000 na ng’ombe 500 kwa siku, ikiwa ni pamoja na na kijiji cha Eworendeke kunufaika na mapato asilimia 10 kutoka eneo la mradi.

Dkt. Mhina anasema kuwa kwa mara ya kwanza katika nchi hii, Serikali imepata mapato makubwa kupitia mnada wa kuuza mifugo kwenda nchi jirani ya Kenya.

“Katika mnada huo tuna mifugo takribani 3,000 hadi 6,000 kulingana na msimu inavuka kwenda nchi ya Kenya, na mifugo hiyo imekuwa ikivuka bila Serikali kupata ushuru wa aina yoyote yaani export permit kwa miaka yote, lakini tulivyoanzisha mnada huu kwa kipindi cha mwaka huu  pekee tayari Serikali imekusanya shilingi bilioni 1.2, na hivyo kiasi ambacho halmashauri inapata kwa mwaka kutokana na mnada huu ni shilingi milioni 400 na hivyo kuongeza mapato ya halmashauri ambapo inatusaidia kupeleka fedha katika miradi ya maendeleo pamoja na kulipa stahili“ anasema Dkt. Mhina.

Dkt. Mhina anaendelea kusema kuwa ili kuongeza mnyororo wa thamani licha ya kuwa na soko la kimataifa la mifugo, wilaya yake tayari imepata muwekezaji anayejenga kiwanda kikubwa kuchakata nyama katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambacho ambacho ujenzi wake utakamilika mwezi Julai mwaka huu.

Aidha, anaongeza, “Tunaamini kuwa kiwanda hicho kitakapoanza kufanya kazi,  kitakuza uchumi wa wilaya yetu, na watu watafuga kwa tija, tumeshaongea na benki mbalimbali pamoja na vikundi zaidi ya 100  vya wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo na hivi sasa tumeanzisha SACCOS ya kununua na kuuza mifugo ili kiwanda kitakapoanza kazi watanzania wasibaki kuwa watazamaji“

Mmoja wa wawekezaji wa kiwanda hicho cha Eliya Food Overseas Ltd, Alshabir Mohamed anasema kuwa gharama za mradi huu ni jumla ya Dola za Kimarekani 5,000,000.

Ujenzi wa kiwanda hicho umefikia asilimia 80, na wanatarajia kiwanda hicho kuanza kazi ifikapo mwezi Julai mwaka huu, ambapo watapeleka nyama yao kwenye hoteli mbalimbali za hapa nchini pamoja na kusafirisha nje ya nchi.

“Kiwanda hiki kitatumia kila kitu kinachotoka kwa mnyama ili kutengeneza malighafi mbalimbali, ngozi zote zitapelekwa katika kiwanda cha ngozi Mororgoro, pia tutatengeneza chakula cha mifugo, mafuta yanayotoka kwenye wanyama yatatumika kutengeneza sabuni. Aidha, tutaajiri watu 3,000 ambao wengi wao watakuwa vijana“, anasema Mohamed.

Hakika mapinduzi yanayoendelea katika Wilaya ya Longido, ni dhahiri kuwa Serikali imedhamiria kuboresha maisha ya watanzania na kufikia azma yake ya nchi ya  uchumi wa kati ifikapo 2025, sambamba na Tanzania ya viwanda.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com