📍 DODOMA
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema Serikali ipo katika mashauriano ya kufanya marekebisho ya baadhi ya vifungu vya Sheria ya Ndoa, hususan vinavyohusiana na masuala ya elimu.
Ameyasema hayo Septemba 25, 2026, Mtumba jijini Dodoma, wakati akizungumza katika Programu Maalumu ya Sema na Waziri, ambapo amesema kuwa Serikali inaendelea kushughulikia suala la ndoa za utotoni.
Amesema kuwa Serikali haiwezi kubadilisha vifungu vyote vya Sheria ya Ndoa, bali kuna baadhi ya vifungu vinavyofanyiwa mashauriano kwa ajili ya marekebisho, ikiwemo kuangalia suala la elimu ya awali, msingi, sekondari hadi kidato cha sita.
Aidha, amebainisha kuwa Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kushirikiana na Plan International katika kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki na fursa ya kutimiza ndoto zake, huku akiwataka kuendelea kushirikiana katika kuwasaidia mabinti wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali.
Pia ameongeza kuwa kuna umuhimu wa kwenda katika maeneo mbalimbali kujifunza changamoto zinazowakabili wanawake na mabinti wadogo, wakiwemo wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia, huku akisema kuwa mabinti wanaokumbwa na changamoto wanapaswa kuwezeshwa mitaji ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Naye, Mkurugenzi wa Plan International Tanzania, Jane Sembuche, amesema asilimia 29.1 ya wanawake wenye umri wa miaka 20–24 walioolewa waliingia kwenye ndoa kabla ya kufikisha miaka 18, hali inayoweza kuathiri elimu, afya na fursa za kiuchumi za wasichana. Amesisitiza umuhimu wa kufanyia marekebisho Sheria ya Ndoa ili kuweka miaka 18 kuwa umri wa chini wa ndoa kwa wote, hatua muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Tanzania 2050.
Kwa upande wake, Mkuu wa Sera, Mkakati na Ubora wa Plan International Tanzania, Christina Ruhinda, amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria, huku mabinti wakiendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na wizara hiyo ili kujifunza uongozi, sheria na haki.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CAMFED Tanzania, Anna Sawaki, amepongeza hatua ya Serikali kuanza mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa, akisema kwa pamoja wanaweza kumwezesha mtoto wa kike. Amesema CAMFED inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo Plan International na mashirika ya kimataifa, kuhakikisha watoto wa kike wanaotolewa katika mazingira hatarishi wanapata elimu na kuwezeshwa kutimiza ndoto zao, ikiwemo kuwa viongozi. Aidha, amesema amefurahishwa na ushiriki wao katika kampeni ya Girls Takeover inayohamasisha wasichana kushiriki katika uongozi na kujenga uwezo wa kufikia matarajio yao.
Naye Veronica Kalenga, mnufaika wa Plan International Tanzania, amesema amefurahi kushiriki katika programu ya Girls Takeover 2026, ambapo alipata fursa ya kuchukua nafasi ya Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kujifunza masuala ya uongozi, utendaji wa Serikali pamoja na namna ya kusikiliza na kushughulikia kero za wananchi.
Aidha, Jenipha Lucas, mkazi wa Geita na mnufaika wa Plan International Tanzania, amesema programu hiyo imempa fursa ya kujifunza na kushiriki katika masuala ya uongozi, huku akiishukuru Plan International Tanzania kwa kuwawezesha wasichana kupata nafasi za kujenga uwezo na kujiamini. Ameomba shirika hilo kuendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili wasichana, ikiwemo ndoa za utotoni na mimba katika maeneo ya vijijini.













0 comments:
Post a Comment