Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana
Gerald Kusaya amewaambia Wananchi wa kijiji cha Mtanana B kwenye Halmashauri ya
wilaya ya Kongwa kuwa ametumwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli kuwaletea zawadi ya ujenzi wa Kituo Mahiri (Centre of
Excellence) kwa ajili Udhibiti wa Sumukuvu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo
aliyasema hayo wakati alipotembelea eneo ambalo Kituo Mahili (Centre of
Excellence) cha Ujenzi wa Mradi huo kinataraji kujengwa na kuongeza kuwa tayari
fedha kwa ajili ya ujenzi huo ilishatolewa na Mhe. Rais na kwamba
kinachosubiriwa ni Wananchi kuridhia na kutoa eneo la ekari 150 na baada ya
hapo kesho tarehe 18 Juni, 2020. Serikali itasaini makubaliano na Kampuni ya
ujenzi ya B.J. Amuli ambayo itajenga majengo ya mradi huo.
Ujenzi wa Mradi wa Kituo Mahili cha
Udhibiti wa Sumukuvu unaenda sambamba na ujenzi wa Maabara Maalum itakayotumika
kupima sampuli na kuendesha majaribio mbalimbali yenye lengo la kuongeza
mapambano ya udhibiti wa changamoto ya sumukuvu.
Baada ya maelezo hayo ya Katibu Mkuu;
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtanana B Bwana Zakaria James amesema Wanakijiji
wamekubali mradi huo kujengwa katika eneo lao na kwamba watajitolea kuhakikisha
mradi unalindwa na unafanikiwa kama ilivyopangwa.
“Katibu Mkuu; naomba tufikishie salama
zetu kwa Mhe. Rais Magufuli. Tumekubali mradi huu uanze na tunaahidi kuulinda
ili ufanikiwe sawa sawa na malengo yake.” Amekaririwa Mwenyekiti wa kijiji cha
Mtanana B.
Naye Afisa Mtendaji wa kijiji cha
Mtanana B amesema Wananchi wameunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea
maendeleo na kwa kauli moja wamekubali kutoa eneo la ekari 150 ili kuhakikisha
ujenzi unaanza na kukamilika kwa wakati.
Akiongea mbele ya Katibu Mkuu;
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kongwa Bwana Omary Nkullo amesema kwa
niaba ya Wananchi wa Wilaya ya Kongwa, anamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Joseph Magufuli na kuongeza kuwa Kongwa
imekuwa ikipata fursa ya kutekeleza miradi mingi na kwamba Viongozi watahakikisha
wanashirikiana na Mkandalasi ili ikamilike kwa wakati.
Awali Katibu Mkuu Bwana Gerald Kusaya
alitembelea ili kuona eneo itakapojengwa mradi wa pili wa ujenzi wa maabara
maalum katika eneo la Mahoma Makulu njia ya kuelekea Hombolo katika Halmashauri
ya Jiji la Dodoma.
Baada ya kufika na kukagua eneo la
ujenzi wa maabala hiyo maalum kwa ajili ya kufanyia majaribio ya sampuli za
sumukuvu Bwana Kusaya amesema eneo lipo sehemu nzuri na kuongeza kuwa ni vyema
Mjenzi atakayejenga maabara hiyo pamoja na majengo mengine kuhakikisha kuwa
anajenga majengo yenye viwango na kulitumia eneo vizuri huku msisitizo ni
kufanya usafi wa eneo husika kwa kutokata miti yote ya asili ili kulinda uasili
na kutunza mazingira.
“Mkandalasi (Kampuni ya K & M
Architect) napenda kusisitiza kuwa matumizi mazuri ya nafasi wakati wa ujenzi
ili kama Wizara itakuwa na mahitaji mengine basi eneo litumike kwa ufanisi”
Amekaririwa Katibu Mkuu.
“Jambo lingine, ni vyema eneo hili
lisafishwe vizuri bila kuleta uhalibifu wa mazingira, kuna miti ya asili ambayo
si vyema ikikatwa yote; Sisi Wizara ya Kilimo ni Wadau wa mazingira, lazima
tuonyeshe kwa vitendo dhana ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira”. Amesisitiza
Bwana Kusaya.
Katibu Mkuu baada ya kufanya ukaguzi wa
eneo la ujenzi wa maabara hiyo ametoa maagizo ya kuanza mara moja kwa
usafishaji wa eneo husika kwa kuzingatia maelekezo hayo na kuahidi kuwa usafi
utakapokamilika, atakuja kutembelea ili kujionea maendeleo ya kazi hiyo.
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo
ilizindua rasmi Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu (TANPAC) mapema mwezi Julai 2019
ambapo, utekelezaji wa Mradi huo ni pamoja na ujenzi wa Kituo Mahili cha
Udhibiti na mafunzo ya sumukuvu pamoja na maabara kwa ajili ya kupimia sampuli
pamoja na kuendesha utafiti huku msisitizo ukiwa ni mikoa inayoathirika mara
kwa mara. Mikoa hiyo ni pamoja na Dodoma na Manyara.
0 comments:
Post a Comment