Wakurugenzi wa kampuni ya TanzaniteOne Mining Limited iliyopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Manyara kwa kosa la Uhujumu Uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni tatu ( 3.)
Wakisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Manyara, Simon Kobelo tarehe 22 Mei, 2020, Mwendesha Mashtaka ambaye pia ni Wakili wa Serikali Tarsila Asenga aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Hussein Gonga (Mkurugenzi), Faisal Shabhai (Mkurugenzi), Abubakar Lombe ambaye ni Mlinzi wa kampuni hiyo na Anthony Maswi Mhandisi wa kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka Tarsila Asenga amesema watuhumiwa hao waliisababishia Serikali hasara ya shilingi bilioni 3,558,086,418.80 kwa kufanya makosa saba ambayo ni 1. Kuongoza genge la uhalifu; 2. Kushindwa kufuata amri halali za Mkaguzi wa Migodi; 3. Kukaidi amri halali ya Mamlaka; 4. Kushindwa kufuata Kanuni za Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira; 5. Kukwepa kodi ya Serikali; 6. Kuzisababishia hasara mamlaka za Serikali na 7. Utakatishaji fedha.
Watuhumiwa hao walikuwa wakifanya hujuma hizo katika eneo la leseni namba ML 490/2013 ambalo awali lilikuwa likimilikiwa na Kampuni ya TanzaniteOne Mining Ltd lakini lilirejeshwa Serikalini mwezi Desemba, 2019.
Amesema watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwakuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo kwa sasa hadi jalada la kesi hiyo litakaporudi kutoka kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP)
Washtakiwa hao wamepelekwa Rumande kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana mpaka itakapotajwa tena tarehe 22 June, 2020.
0 comments:
Post a Comment