Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres ameisifu Serikali ya
Tanzania kwa jitihada zake za kutafuta amani nchini Burundi.
Guterres
alitoa pongezi hizo wakati aliposimama kwa muda katika Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wa jijini Dar es Salaam akitokea
Kenya.
Katibu
Mkuu huyo mpya wa UN alisimama kwa ajili ya kufanya mazunguzmo na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk
Augustine Mahiga.
Pamoja
na mambo mengine Guterres alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa
serikali kwa juhudi zake za kutafuta amani nchini Burundi kupitia kwa
Msuluhishi wa mgogoro huo, Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu,
Benjamin Mkapa.
“Tanzania
imekuwa kinara wa amani Afrika na duniani na naipongeza kwa dhati
katika jitihada zake inazozifanya za kutafuta amani ya Burundi na katika
nchi nyinge za ukanda huu,” alisema Guterres.
Aidha
alisema anatambua mzigo mkubwa inaoupata kama nchi kutokana na
kuendelea kupokea wakimbizi kutoka Burundi, na kuahidi UN kuendelea
kuunga mkono jitihada za kutafuta suluhu ya kisiasa nchini humo.
Kwa
upande wake; Balozi Mahiga aliwasilisha salamu maalum kutoka kwa Rais
John Magufuli kuhusiana na hatua iliyofikiwa ya usuluhishi wa mgogoro wa
Burundi na ushiriki wa Tanzania katika vikosi vya Umoja wa Mataifa vya
ulinzi wa amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Balozi Mahiga pia alisema Tanzania imefurahishwa na ujio wake na Rais amempa mwaliko rasmi wa kufanya ziara nchini.
Aidha
alimweleza kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za
Kusini mwa Afrika (SADC), katika mkutano wao ujao wana mpango wa
kuwasilisha hoja maalum kuhusu hali ya kisiasa nchini DRC.
Mbali
na kufanya ziara nchini Kenya, Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa
alitembelea Somalia na kukutana na Rais mpya wa nchi hiyo, Hassan Sheikh
Mohamud, ambapo aliagiza Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua kuepusha
balaa la njaa nchini humo, kutokana na hali mbaya ya ukame.
0 comments:
Post a Comment