METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, May 24, 2020

KAMATI YA UFUNDI TUME YA MADINI YATAKIWA KUPITIA UPYA LESENI MWABOMBA


Waziri wa Madini akizungumza na Wachimbaji Wadogo wa Madini katika Kijiji cha Mwabomba, Wilayani Kahama wakati wa ziara yake ya kutembelea shughuli za uchimbaji wa Madini nchini.
Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Mwabomba Wilayani Kahama wakifuatilia hotuba ya Waziri (hayupo pichani) wakati wa mkutano wa hadhara.

Tume ya Madini imeagizwa kuitisha Kikao cha Kamati ya Ufundi ili kupitia Upya Mchakato wa Leseni  Nne (4) za Uchimbaji Madini za Balafuma, Namba 1, Namba 2, na Namba 6 katika Kijiji cha Mwabomba Kata ya Idahina Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga ili kupatiwa wachimbaji Wadogo badala ya Kampuni ya Calton Miyabi (T) Ltd.


Uamuzi huo umefikiwa baada ya kuwepo kwa  mgogoro wa Leseni ya uchimbaji  katika maeneo hayo kati ya Wachimbaji wadogo wa Madini na kampuni za uchimbaji uliodumu kwa miaka 20.

Waziri wa Madini Doto Biteko ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake kijijini hapo ya kukagua shughuli za uchimbaji madini, kuzungumza na wananchi na kampuni hiyo na kueleza kwamba, wachimbaji hao wanayo haki ya kumiliki eneo husika kutokana na aina ya makubaliano yaliyofanyika awali  kati ya Wachimbaji na Kampuni ya Tanzania  Minerals Liquefied  Gas and Petroleum  Limited .

Biteko ameongeza kuwa, anafahamu mchakato wa leseni hizo kupatiwa kampuni ya Calton Miyabi (T) Ltd  ulifika mbali lakini hauna budi kupitiwa upya  na kamati husika na maombi ya leseni hizo asipewe mtu mwingine isipokuwa wachimbaji wadogo wa eneo hilo.

Hata hivyo, ameishauri kampuni husika kufanya mazungumzo na wachimbaji hao endapo kuna shughuli za uchimbaji mkubwa uliopangwa kufanyika, huku ikitakiwa kukumbuka kuwa wachimbaji hao ndiyo wamiliki halali wa maeneo husika.

Waziri Biteko amewapongeza wachimbaji wa Mwabomba na kusema kuwa, kwa kipindi kifupi wameweza  kulipa kodi za Serikali zaidi ya Shilingi Milioni 500 huku wakichangia huduma za kijamii zenye thamani ya shilingi milioni 500.

Aidha, ametumia fursa hiyo kuwaasa wachimbaji kuhakikisha wanaanzisha vitega uchumi vingine kutokana na faida wanazopata kufuatia  shughuli za uchimbaji madini wanazozifanya na kueleza kuwa, kuna wakati madini yanakwisha.

‘’lakini pia , wale wachimbaji wanaochimba kwa midomo waache kuwachanganya wachimbaji na kutafuta migogoro. Heshima ya Sekta hii ni kutokuwepo migogoro, lakini pia Mhe. Rais anataka kutengeneza mamilionea siyo migogoro,’’ amesema Waziri Biteko

Vilevile, Waziri Biteko ameendelea kuwakumbusha wachimbaji nchini hususan katika kipindi hiki cha Ugonjwa wa Covid-19, kuhakikisha wanafanya shughuli zao kwa kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huo huku wakiwalinda wengine.

“ Jitahidini kuishi salama, jilinde wewe na uwalinde na wengine na hakikisha muda wote upo salama. Usipokuwa salama hata madini hayo hutochimba na waziri hawezi kuja,’’ amesisitiza Waziri Biteko.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Wilaya ya Kahama Timoth Ndanya amemshukuru waziri Biteko kwa kumaliza mgogoro huo na kuchukua nafasi hiyo kuendelea kuwasisitiza wachimbaji hao kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya kuhusu ugonjwa wa Covid -19.

Naye, Diwani wa Kata ya Idaiya , Yuda Majonjozi amesema amemongeza Waziri Biteo kwa kutambua uwepo wa wachimbaji wadogo katika eneo lake na kueleza kuwa, wachimbaji wamekuwa wakichangia katika maendeleo ya kijiji kwa kuchangia huduma za kijamii.
“ Mhe. Waziri, Mhe, Rais alitwambia katika eneo hili hatutafukuzwa tena, tunashukuru sana leo tumefikia suluhisho ya mgogoro huu.

Waziri Biteko ameelezea kwa kifupi mazingira yaliyosababisha kuwepo kwa mgogoro huo ambapo ameeleza kuwa, awali, kabla ya Kampuni ya Calton Miyabi (T) Limited, kampuni ya Tanzania  Minerals Liquidfied  Gas and petroleum  Limited iliingia makubaliano  na wachimbaji na kutoa maeneo Manne  baadaye ikachukua leseni kwa jina la Tanzania Minerals bila kujumuishwa wachimbaji hao na baada  ya mwaka mmoja leseni ikafutwa na kupewa kampuni ya kigeni na hatimaye kampuni ya Australia iliyoomba leseni ya utafiti.

Awali, Waziri Biteko amezitaja juhudi za Serikali zilizofanywa katika Awamu ya Tano za kuhakikisha inawafanya watanzania kuwa sehemu ya wamiliki wa uchumi wa madini, wachimbaji nchini kufanya shughuli zao vizuri ikiwemo biashara ya madini kwa kuanzisha Masoko ya Madini mikoa mbalimbali nchini suala ambalo limewezesha wachimbaji kupata maeneo maalum ya kuuza madini yao.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com