METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, May 26, 2020

SERIKALI YAWATAKA MAAFISA MADINI KUTHIBITISHA USHURU MIGODINI


Waziri wa Madini Doto Biteko akikagua shughuli za uchimbaji madini katika eneo la Lusu, wilayani Nzenga Mkoa wa Tabora.
Baadhi ya wananchi wakiponda mawe yenye dhahabu katika moja ya mgodi wa wachimbaji wadogo.

Baadhi ya Wachimbaji wakimwangalia Waziri Biteko (hayupo pichani) wakati wa ziara yake katika migodi ya Lusu Wilayani Nzega. 
Baadhi ya wachimbaji wakimsikiliza Waziri Biteko wakati akizungumza nao katika mkutano wa hadhara baada ya kutembelea migodi.

Serikali imesema Ushuru wowote unaotolewa kwenye Maeneo ya Migodi Nchini ni lazima uthibitishwe na Maafisa Madini walioko kwenye maeneo husika.

Tamko hilo lilitolewa Mei 24, 2020  na Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akizungumza na Wachimbaji  Wadogo wa Madini ya Dhahabu eneo la Lusu Wilayani Nzega  Mkoa wa Tabora alipotembelea eneo hilo kuangalia shughuli za uchimbaji madini.

Aidha, tamko hilo linafuatia kuwepo kwa malalamiko toka kwa wachimbaji wanaofanyakazi kwenye Leseni za baadhi ya Wachimbaji ambao walimlalamikia Waziri Biteko kutozwa kodi na wenye leseni hizo na hivyo kuomba ufafanuzi juu ya suala hilo.

Waziri Biteko alisisitiza kwa kuwataka Maafisa hao kuhakikisha  Ushuru unaotolewa ni ule tu uliopo Kisheria na kuhakikisha wanasimamia jambo hilo.

Akifafanua kuhusu suala la mrabaha wa mawe  unaotozwa na Serikali alieleza kuwa,  wachimbaji wasio rasmi  wanalazimika kulipia mrabaha wa mawe isipokuwa wenye Leseni wanatakiwa kulipia mrabaha wa dhahabu baada ya kukamilisha hatua zote.

" Wale msio rasmi mjue mkigawana mawe na  Serikali  itakuwepo mnagawana nayo isipokuwa mwenye Leseni  yeye tutamwomba mrabaha wetu mwishoni. Ukitaka kulipa mrabaha mara moja chimba kwenye Leseni, mkichimba bila utaratibu tutagawana kwenye mawe na kwingine," alisisitiza Waziri Biteko.

Pia, aliendelea kuwasisitiza wachimbaji nchini kuyatumia Masoko ya Madini yaliyoanzishwa katika maeneo mbalimbali kufanya biashara ya madini.

Akijibu ombi la wachimbaji hao kupelekewa Wataalam wa masuala ya Utafiti ili kuwawezesha kujua  mwelekeo wa miamba na hivyo kuchimba kwa tija, alisema Wizara itaangalia namna ya kufikisha Mtambo wa  Kuchoronga katika eneo hilo baada ya Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO) kukamilisha kazi za kandarasi za uchorongaji zinazoendelea  katika maeneo mengine.

Katika hatua nyingine, alipongeza wachimbaji kwa kulipa mrabaha wa Serikali na hivyo kuwezesha makusanyo ya  shilingi Bilioni 2.7 hadi  kufikia Aprili 30, sawa na asilimia 122 na hivyo  kuvuka lengo la makusanyo ya shilingi bilioni 2.2 zilizopangwa kukusanywa Mwaka wa fedha 2019/2020.

Aidha, aliongeza kuwa, baada ya serikali kutoa eneo hilo kwa wachimbaji  wadogo, kwa kipindi cha kuanzia  mwezi Desemba  hadi sasa  madini ya dhahabu ya thamani ya shilingi Bilioni 3 na Milioni 500 yalizalishwa katika eneo hilo la Lusu.

" Watanzania changamkieni Rasilimali hii Ni zenu, chapeni kazi mlipe Kodi," amesema Biteko.

Aidha, alimpongeza Mkuu wa Wilaya hiyo Godfrey Ngupula kwa kusimamia vizuri Sekta ya Madini na kuwa karibu na wachimbaji wadogo.

Awali, katika eneo la Chuo Cha Madini Tawi la Nzega, Mkuu wa Wilaya hiyo Godfrey Ngupula alimweleza Waziri kuwas shughuli ya uchukuaji mchanga wa Dhahabu ulioachwa na  Kampuni ya Resolute  unaofanywa na Kampuni ya Ashery Construction & Matinje unaendelea vizuri na kuongeza kwamba ifikapo Juni 1   wakati Chuo kitakapofunguliwa zoezi hilo litakuwa limekamilika ns kuongeza kwamba eneo lililotumika linatarajiwa kutengenezwa ujwanj wa mprira.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Nzega Amos Kanunda  ameipongeza Serikali kwa kutoa maeneo 10 kwa ajili ya wachimbaji wadogo Wilayani humo na kusema hivi sasa wachimbaji wanachimba na kuwahimiza kulipa kodi za serikali   huku akisisitiza suala la wataalam wa Utafiti ili kuwawezesha wachimbaji kuchimba kwa  tija na Serikali inufaike kwa mapato.

Naye, Mwenyekiti wa Wachimbaji Mkoa wa Tabora (TABOREMA) Joseph Mabondo amesisitiza suala la Watalaam wa  kupima mwelekeo wa miamba kuwawezesha wachimbaji kuchimba bila kubahatisha. Pia ameipongeza Serikali kuwapatia wachimbaji Mkoani humo maeneo ya kuchimba

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com