METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, May 12, 2020

HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO, MHESHIMIWA JAPHET NGAILONGA HASUNGA (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA KILIMO KWA MWAKA 2020/2021

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb) akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Matumizi ya kawaida ya wizara hiyo ya mwaka 2020/2021. Leo tarehe 12 Mei 2020 (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb) akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Matumizi ya kawaida ya wizara hiyo ya mwaka 2020/2021. Leo tarehe 12 Mei 2020 

1. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji iliyochambua Bajeti ya Wizara ya Kilimo (Fungu 43), Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (Fungu 05) na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (Fungu 24) mnamo tarehe 25 na 26 Machi, 2020 Jijini Dodoma, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 na makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2020/2021.
2. Mheshimiwa Spika, kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwa na afya njema na kuendelea kuijaalia nchi yetu amani, utulivu na mshikamano na kutuwezesha kushiriki katika mkutano huu wa Bunge la 19 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni mkutano wa mwisho katika uhai wa Bunge la 11.
3. Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuniamini kusimamia Kilimo ambacho ndio tegemeo la Watanzania walio wengi. Vilevile, niwashukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa wanayofanya kusukuma maendeleo ya nchi hii, ikiwemo Sekta ya Kilimo. Aidha, binafsi ninawashukuru viongozi wangu wote kwa maelekezo, ushauri na miongozo wanayonipatia ambayo imenisaidia kutekeleza majukumu yangu kwa ufanisi mkubwa.   
4. Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine naomba kumpongeza Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) kwa hotuba  yake nzuri aliyoitoa hapa Bungeni tarehe 1 Aprili, 2020. Hotuba hiyo iligusa maeneo mengi ikiwemo Sekta ya Kilimo ambapo alisisitiza uimarishaji wa huduma za ugani, kilimo cha umwagiliaji, ushirika, upatikanaji wa pembejeo sahihi na miundombinu ya masoko.
 Aidha, napenda kumpongeza Mhe. Hussein Mohammed Bashe (Mb.) kwa kuteuliwa kwake kuwa Naibu Waziri na Ndugu Gerald M. Kusaya kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Kilimo na kuungana na viongozi wengine wa wizara kusukuma kilimo hapa nchini.
5. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kukupongeza wewe binafsi, na Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb.) pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa namna mnavyolisimamia na kuliendesha Bunge letu tukufu kwa weledi na umahiri mkubwa. Aidha, niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla kwa kazi nzuri walizozifanya katika miaka hii mitano ya kuwawakilisha wananchi katika Bunge hili. Nimpongeze pia Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu Mbunge wa Singida Mashariki kwa kuchaguliwa kujiunga na Bunge lako Tukufu.
6. Mheshimiwa Spika, naomba kuwapongeza Mawaziri walioteuliwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020, Mheshimiwa George Boniface Simbachawene Mbunge wa jimbo la Kibakwe kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu Mbunge wa jimbo la Ilala kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Mbunge wa Iramba Magharibi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
7. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 Bunge lako Tukufu limewapoteza Wawakilishi wenzetu wanne ambao ni Mheshimiwa Rashid Ajali Akbar aliyekuwa Mbunge wa Newala Vijijini aliyefariki tarehe 15 Januari 2020, Mheshimiwa Mchungaji Dkt. Getrude Pangalile Rwakatare Mbunge wa Viti Maalum aliyefariki tarehe 20 Aprili, 2020, Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa Mbunge wa Sumve aliyefariki tarehe 29 Aprili, 2020 na Mheshimiwa Balozi Dkt Augustine Philip Mahiga (Mb) aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria aliyefariki tarehe 1 Mei, 2020. Nitumie fursa hii kutoa pole kwako, Bunge lako Tukufu, Chama cha Mapinduzi, familia za marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa majimbo ya Newala Vijijini na Sumve.
8. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma Mbunge wa Viti Maalum kwa ushirikiano na  ushauri mzuri walioutoa katika kipindi chote cha mwaka 2019/2020 pamoja na kuipitia taarifa ya utekelezaji ya mwaka 2019/2020 na Mpango wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2020/2021. Naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, ushauri wao umezingatiwa na tutaendelea kushirikiana na Kamati ili kuleta mageuzi ya kilimo na kufikia matarajio ya wananchi katika kufikia uchumi wa kati.
9. Mheshimiwa Spika, natoa shukrani zangu za pekee kwa Wananchi wa Jimbo la Vwawa kwa ushirikiano wanaoendelea kunipa katika kipindi chote cha kuwawakilisha hapa Bungeni. Napenda kuwahimiza kuendelea kuniamini na kuiamini Serikali ya Awamu ya Tano na kwamba maendeleo ya Jimbo letu yanategemea sana kufanya kazi kwa pamoja. Aidha kwa namna ya pekee ninawapongeza sana Naibu mawaziri Mh. Omary Tebweta Mgumba (Mb) na Hussein Mohamed Bashe (Mb) kwa jinsi wanavyonisaidia katika kusimamia na kutekeleza majukumu ya Wizara ya Kilimo. Vile nawapongeza Katibu mkuu Ndugu Gerald Kusaya,  Naibu katibu Mkuu. Prof. Siza Tumbo,  wakurugenzi na vitengo, wakuu wa Taasisi, Bodi na wakala zilizo chini ya wizara kwa ushirikiano na kazi nzuri wanazoendeleza kuzitekeleza ili kufanikisha malengo ya kilimo nchini.
10. Mheshimiwa Spika, Awali ya yote nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa msukumo wa kuendeleza Sekta ya Kilimo. Aidha, katika hotuba yake aliyoitoa tarehe 20 Novemba, 2015 akifungua rasmi Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Dodoma alisisitiza kutekeleza ahadi alizozitoa kwa wakulima kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2015-2020. Wizara imetekeleza ahadi hizo kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) na kuwezesha kilimo kuchangia katika uchumi na maendeleo ya Taifa letu, hususan katika maeneo ya usalama wa chakula na lishe, ajira, upatikanaji wa malighafi za viwanda na kuchangia katika kupunguza umaskini na kuongeza kipato cha wakulima.
11. Mheshimiwa Spika, baadhi ya ahadi alizotoa ni pamoja na kuimarisha huduma za ugani, upatikanaji na usambazaji wa pembejeo, zana za kisasa za kilimo, masoko ya uhakika ya mazao, kuimarisha upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya kilimo na kuondoa ushuru, kodi na tozo ambazo ni kero kwa ajili ya maendeleo ya kilimo.
2. MCHANGO WA SEKTA YA KILIMO KATIKA UCHUMI
12. Mheshimiwa Spika, kilimo kimeendelea kuwa ni mhimili muhimu katika maendeleo ya uchumi wa taifa letu. Katika kipindi cha miaka mitano, Pato la Taifa linalotokana na kilimo, kwa kutumia bei za Mwaka 2015 limeongezeka kwa asilimia 17 kutoka shilingi trilioni 25.2 Mwaka 2015 hadi shilingi trilioni 29.5 Mwaka 2019. Vilevile, sekta imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 58 Mwaka 2018, imechangia asilimia 28.2 ya Pato la Taifa ambapo sekta ndogo ya mazao imechangia asilimia 16.2. Hii imetokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo vyakula vinavyotokana na mazao ya kilimo. Aidha, kati ya mwaka 2015 hadi 2019 sekta ya kilimo imeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 5.2 ambapo sekta ndogo ya mazao imeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 5.8.

3. MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2019/2020

3.1 Fedha Zilizoidhinishwa

13. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo kupitia Fungu 43, Fungu 05 na Fungu 24 iliidhinishiwa na Bunge lako tukufu jumla ya Shilingi bilioni 253.86 ili kutekeleza majukumu yake. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 77.78 ni kwa matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 176.08 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
4. HOMA KALI YA MAPAFU (COVID-19)
14. Mheshimiwa Spika, mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID-19) unaosababishwa na virusi vya Corona umeathiri sekta mbalimbali za kiuchumi nchini ikiwemo sekta ndogo ya mazao. Tathmini imefanyika na kubaini kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2019/2020 haujaathirika kwa kuwa pembejeo zimeshawasili nchini.
 Aidha, katika kukabiliana na uhaba wa mbolea unaoweza kutokea kutokana na kuendelea kuwepo kwa tatizo la COVID-19, Wizara imeiagiza TFRA kuhakikisha mbolea zote zinaagizwa mapema kipindi hiki kabla ya msimu ujao kuanza.
15. Mheshimiwa Spika, mazao ya asili ya biashara ambayo ni pamba, korosho na kahawa misimu yake ya mauzo imeishia mwezi Machi, 2020 na hivyo kutoathirika na ugonjwa huo. Aidha, kwa zao la tumbaku wakulima wameshafunga mikataba na wanunuzi kwa ajili ya msimu 2020/21 na hivyo kutoathiriwa na Covid-19. Mazao ambayo yameonesha dalili za kuathirika ni chai na mazao ya bustani ambayo masoko na usafirishaji wake nje ya nchi umeathiriwa. Vilevile, ugonjwa wa COVID-19 iwapo utaendelea kwa muda mrefu unaweza ukaathiri soko la pamba, korosho, kahawa, na mazao mengine yanategemea minada ya moja kwa moja.  
16. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na ugonjwa wa COVID-19, serikali imepanga kununua tani 300,000 za chakula kupitia NFRA, kuhakikisha sekta binafsi zinahifadhi kwenye maghala, kutumia mfumo wa Soko la Bidhaa (TMX) kwa mazao ambayo hutegemea zaidi wanunuzi kutoka nje ya nchi kama vile zao la korosho, kahawa, pamba, n.k., kutumia balozi zetu nje ya nchi kutafuta manunuzi na masoko, na kutumia soko la moja kwa moja, n.k. hivyo kwenye upande wa mazao ya chakula hii ni fursa ya kuweza kuuza Zaidi kuliko muda mwingine.

Utekelezaji wa Maeneo ya Kipaumbele kwa Mwaka 2019/2020

17. Mheshimiwa Spika,  katika mwaka 2019/2020, Wizara imeendelea kutekeleza maeneo ya kipaumbele ya kuongeza uzalishaji na tija kwenye kilimo kwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, udhibiti wa visumbufu, matumizi ya zana bora za kilimo na huduma za ugani; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji; ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi mazao ya kilimo na masoko; kufanya utafiti wa kilimo na kuzalisha teknolojia kwa mazao ya mahindi, muhogo, ngano, michikichi, ufuta, alizeti, pamba na mpunga.

5. MAFANIKIO YA WIZARA YA KILIMO KATIKA KIPINDI CHA SERIKALI YA AWAMU YA TANO
18. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka minne Wizara imepata mafanikio makubwa katika maeneo ya usalama wa chakula na lishe; uzalishaji wa mazao makuu ya biashara; upatikanaji wa pembejeo za kilimo; viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na masoko; utafiti, huduma za ugani na mafunzo; hifadhi ya mazao; uzalishaji wa mazao ya bustani; kuimarika kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko; kuimarika kwa ushirika; kuimarika kwa kilimo cha umwagiliaji; ongezeko la ushiriki wa vijana katika kilimo; matumizi bora ya ardhi; kuhuisha mifumo na sera za kilimo na kuanzishwa kwa kanzidata ya wakulima na wadau mbalimbali wa kilimo.


5.1 Usalama wa Chakula na Lishe

19. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka minne (4) upatikanaji wa chakula umeendelea kuimarika na hivyo kuwezesha nchi yetu kujitosheleza kwa chakula kwa wastani wa asilimia 121 na kuwa na wastani wa ziada ya tani 2,798,700.60. Aidha katika mwaka 2019/2020 upatikanaji wa chakula ulifikia tani milioni 16.2 ukilinganisha na mahitaji ya chakula ya tani milioni 13.8. Hivyo ziada ya chakula ilikuwa tani 2,473,774 na kuwa na kiwango cha utoshelevu cha asilimia 118.
Hali ya Lishe nchini
20. Mheshimiwa Spika, kulingana na taarifa ya mapitio ya kati (Mid Term Review) ya hali ya lishe nchini katika utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa lishe wa mwaka 2016-2021) uliyofanyika mwaka 2019, inaonesha kuwa udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano umepungua kutoka asilimia 34 mwaka 2015 kufikia asilimia 32 mwaka 2018. Aidha, Kiwango cha ukondefu kwa watoto chini ya miaka mitano kitaifa kimeendelea kushuka kutoka asilimia 3.8 hadi asilimia 3.5 na pia upungufu wa damu kwa akina mama umepungua kutoka asilimi 44.7 hadi kufikia asilimia 28.7 kwa kipindi hicho.
21. Mheshimiwa Spika, jukumu la serikali ni kuhakikisha kuwa mazao mbalimbali ya chakula yenye virutubishi kwa wingi yanazalishwa yakiwemo viazi lishe” na maharagwe yaliyoongezewa madini chuma na zinki.  Uzalishaji na utumiaji wa mazao haya unachangia kupunguza tatizo la upungufu wa damu unaosababishwa na ukosefu wa madini chuma na tatizo la upungufu wa vitamin A hususan kwa akina mama walio katika umri wa kuzaa na watoto chini ya miaka mitano (Mheshimiwa Spika maelezo ya kina yametolewa Uk. 12 hadi 15 wa kitabu cha Hotuba).
5.2 Uzalishaji wa Mazao Makuu ya Biashara

22. Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mazao makuu ya biashara yakiwemo pamba, kahawa, chai, pareto, tumbaku, korosho, mkonge na miwa umeongezeka kutoka jumla ya tani 796,502 Mwaka 2015/2016 hadi jumla ya tani 1,144,631 Mwaka 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia 43.7. Aidha zao la miwa limeongoza likifuatiwa na korosho na Pamba.
23. Mheshimiwa Spika, vilevile katika kipindi hicho cha miaka minne kiasi cha tani 1,613,000 za mazao ya kahawa, pamba, katani, chai, tumbaku na korosho kiliuzwa nje ya nchi na kuliingizia Taifa jumla ya Dola za Marekani Milioni 3,419.77 sawa na Shilingi trilioni 6.9. Aidha, Wizara kupitia Bodi ya Tumbaku imeuza jumla ya tani 500 za tumbaku ya daraja la chini (Reject) ambayo mapato yake yamesaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima na kuwaongezea kipato. (Mheshimiwa Spika maelezo ya kina yametolewa Uk. 15 hadi 16 wa kitabu cha Hotuba)

5.3 Uzalishaji wa Miwa na Sukari
24. Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Spika, Mahitaji ya sukari nchini ni takribani tani 420,000 ikiwa ni wastani wa tani 35,000 kwa mwezi. Uzalishaji wa Sukari kwa mwaka 2019/2020 ulikadiliwa kuwa tani 380,000, kulingana na matarajio ya uzalishaji huo upungufu wa Sukari ulikadiliwa kuwa wastani wa tani 40,000 kwa matarajio kwamba viwanda vingeweza kuzalisha kiasi chote cha Sukari cha tani 380,000 kilichokadiliwa mwanzoni mwa msimu. Aidha, kutokana na mvua kunyesha kupita kiasi viwanda  havikufikia Malengo ya uzalishaji ambapo vilizalisha tani 310,000 hivyo pengo la mahitaji kuongezeka kutoka tani 40,000 hadi kufikia tani 110,000. Hata hivyo, kwa vile viwanda vya ndani vinatarajia kuanza uzalisha mwezi Juni, 2020 ni matarajio ya serikali upatikanaji wa Sukari utarejea katika hali yake ya kawaida.
25. Mheshimiwa Spika, Ili kukabiliana na upungufu huo, Serikali ilichukua hatua ya kutoa vibali vya tani 40,000 kwa wazalishaji wa ndani wanne (4) kuingiza Sukari ambapo kila mzalishaji alipewa kibali cha kuingiza tani 10,000. Hadi sasa kiasi cha tani 14,398 kimekwisha ingizwa na kusambazwa nchini, kiasi cha tani 3,920 kipo katika hatua mbalimbali za kutolewa bandarini na kiasi cha tani 21,166 kinatarajiwa kuingizwa nchini kabla ya mwisho wa mwezi Mei, 2020. Kutokana na tatizo la mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 wafanyabiashara wachache wasio waadilifu wamekuwa wakihodhi Sukari na kusababisha kupanda bei. Hata hivyo, serikali inafuatilia mwenendo wa uingizwaji wa Sukari na kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha kunakuwa na utulivu wa soko.
26. Mheshimiwa Spika, Serikali inalenga kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 320,000 za sasa hadi 630,000 ifikapo mwaka 2024/2025 kutokana na uwekezaji mpya na upanuzi wa viwanda vilivyopo na hivyo  kujitosheleza kwa mahitaji ya Sukari nchini. Hata hivyo, serikali itaendelea kutoa vibali vya kuziba pengo la uzalishaji Sukari nchini kwa wakati ilikuhakikisha Sukari inapatikana nchini kwa wakati wote.
5.4 Mazao ya Bustani

27. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka minne, uzalishaji wa mazao ya bustani umeongezeka kutoka tani 5,931,900 mwaka 2015/2016 hadi tani 6,556,102 mwaka 2018/2019. Thamani ya mauzo ya mazao ya bustani yakiwemo mbogamboga na maua nje ya nchi yameongezeka toka Dola za Marekani milioni 412 mwaka 2015 hadi Dola za Marekani milioni 779 mwaka 2018/2019. Ongezeko hilo la mauzo linaifanya Tasnia ya mazao ya bustani kuchangia asilimia 38 ya fedha za kigeni zinazotokana na sekta ya kilimo.
28. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi hicho, uwekezaji katika mazao ya bustani kupitia sekta binafsi chini ya mwamvuli wa TAHA umefikia Dola za Marekani milioni 30. Aidha zao la parachichi limeonesha mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka minne ambapo uzalishaji umeongezeka kutoka tani 20,000 Mwaka 2015 hadi kufikia tani 190,000 Mwaka 2018. Mauzo yenye thamani ya Dola za marekani Milioni 8.5 yamefanyika katika soko la ulaya hususan nchi za Ufaransa, Uholanzi na Uingereza. (Mheshimiwa Spika maelezo ya kina yametolewa Uk. 17 hadi 20 wa kitabu cha Hotuba) 
5.5 Upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo
5.5.1 Mbegu
29. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka minne upatikanaji wa mbegu bora umeongezeka kutoka tani 36,614.28 mwaka 2015/2016 hadi tani 76,725.52 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 110. Aidha, uzalishaji wa ndani wa mbegu bora umeongezeka kutoka tani 20,604.97 mwaka 2015/2016 hadi tani 69,173.17 mwaka 2019/2020. Vilevile, uzalishaji wa miche umeongezeka kutoka miche 5,000,000 mwaka 2015/16 hadi kufikia miche 25,285,859 mwaka 2019/20. Pamoja na mambo mengine, mafanikio hayo yametokana na kuongezeka kwa eneo la uzalishaji wa mbegu na miche kutoka hekta 10,887 hadi hekta 94,368. Vile vile serikali imeimarisha maabara ya TOSCI na hivyo kupata ithibati ya Shirika la Kimataifa la Uthibiti wa Ubora wa Mbegu (International Seeds Testing Association – ISTA) pamoja na kujiunga na Skimu za Mbegu za Shirika la Kimataifa (OECD Seed Schemes) ambayo itaiwezesha nchi kufanya biashara ya mbegu kimataifa.
5.5.2 Mbolea
30. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho Wizara imeimarisha upatikanaji wa mbolea nchini kwa kuanzisha mfumo wa ununuzi wa pamoja (Bulk Procurement System - BPS) ambao umewezesha kuongeza upatikanaji wa mbolea kutoka tani 302,482 mwaka 2015/2016 hadi 633,197 mwaka 2019/2020.  Mfumo huo umewezesha wakulima kupata mbolea kwa wakati na bei nafuu. Aidha, idadi ya viwanda vinavyotengeneza mbolea na visaidizi vya mbolea (fertilizer suppliment) vimeongezeka kutoka viwanda vinne (4) mwaka 2015 hadi viwanda 13 mwaka 2019. Kati ya viwanda hivyo, viwanda viwili (2) ni vya visaidizi na 11 ni vya mbolea.
5.5.3 Viuatilifu
31. Mheshimiwa Spika, Upatikanaji wa viuatilifu kwa ajili ya kudhibiti visumbufu vya milipuko kama vile panya, nzige, kweleakwelea na viwavijeshi vamizi umeongezeka kutoka tani 4,111.50 mwaka 2015 hadi tani 16,869.10 mwaka 2019. (Mheshimiwa Spika maelezo ya kina yametolewa Uk. 21 hadi 26 wa kitabu cha Hotuba)
5.6 Mazingira ya Uwekezaji na Uanzishaji wa Viwanda vya Kuchakata Mazao ya Kilimo
32. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2015/16 hadi 2019/20, Serikali imefuta ushuru, tozo na ada 105 na kupunguza tozo nne (4) kati ya 146 zilizokuwa zinatozwa katika mazao ya kilimo. Hatua hiyo imevutia Sekta binafsi kuwekeza takribani Shilingi Trilioni 3.7 kwenye mnyororo wa thamani wa kuendeleza mazao ya chai, kahawa, mkonge, ngano, shayiri na mpunga. Aidha, ajira katika mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo zimeongezeka kutoka wastani wa ajira 3,880,262 Mwaka 2015/16 hadi kufikia wastani wa ajira 5,204,607 Mwaka 2018/19.
33. Mheshimiwa Spika, Wizara imehamasisha ujenzi wa viwanda ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kutengeneza ajira kwa watanzania. Katika kipindi cha miaka minne, jumla ya viwanda vipya 189 vya kuchakata mazao vimeanzishwa vikiwemo vya korosho 9, chai 3, kahawa 59, pamba 36, mkonge 81 na pareto 1. (Mheshimiwa Spika maelezo ya kina yametolewa Uk. 29 hadi 31 wa kitabu cha Hotuba)
5.7 Upatikanaji wa Masoko ya Mazao ya Kilimo
34. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka minne (4) Wizara imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya kilimo ndani na nje ya nchi. Katika kufikia azma hiyo, Wizara imeanzisha kitengo cha Masoko (Agricultural Marketing Division) katika Idara ya Maendeleo ya Mazao inayosimamia utafutaji wa masoko, kufanya tafiti za masoko na bei za mazao pamoja na kufuatilia mifumo ya uuzaji wa mazao. (Mheshimiwa Spika maelezo ya kina yametolewa Uk. 33 hadi 36 wa kitabu cha Hotuba) 
5.8 Utafiti, Huduma za Ugani na Mafunzo ya Kilimo
35. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi hicho TARI kwa kushirikiana na sekta binafsi imegundua aina 124 za mbegu bora. Aidha, kati ya hizo kampuni binafsi zimegundua aina 35 za mbegu bora za mazao ya kilimo. Vilevile, utafiti wa kupima afya ya udongo na kuandaa ramani zinazoonesha mtawanyiko na viwango vya mboji (Organic carbon) pamoja na uchachu (pH) wa udongo katika mikoa yote nchini umefanyika.
36. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia vyuo vyake 14 imetoa wataalam wa kilimo 7,530 na 6,146 wamehitimu katika vyuo binafsi 12 ngazi ya Astashahada na Stashahada za kilimo. Aidha, jumla ya maafisa ugani 902 na wakulima 42,192 wamepatiwa mafunzo kuhusu kanuni za kilimo bora, teknolojia mbalimbali za uzalishaji, jinsia na masoko. (Mheshimiwa Spika maelezo ya kina yametolewa Uk. 37 hadi 40 wa kitabu cha Hotuba)
5.9 Hifadhi ya mazao
37. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2015 nchi ilikuwa na jumla ya maghala 3,400 yenye uwezo wa kuhifadhi tani 2,774,106 za mazao ya chakula. ujenzi na kukarabati miundombinu ya hifadhi yavihenge 57 na ghala 118 zenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya tani 203,000 na tani 100,700 mtawalia na hivyo kuongeza uwezo wa kuhifadhi kutoka tani 2,774,106 mwaka 2015/2016 hadi tani 3,077,806 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 11. (Mheshimiwa Spika maelezo ya kina yametolewa Uk. 40 hadi 46 wa kitabu cha Hotuba)
5.10 Kuimarisha Ushirika
38. Mheshimiwa Spika, Ushirika umeendelea kuimarika ambapo Vyama vya Ushirika vimeongezeka kutoka 7,394 mwaka 2015 hadi 11,626 mwaka 2019 sawa na ongezeko la asilimia 57. Vilevile, idadi ya wanachama wa Vyama vya Ushirika imeongezeka kutoka 2,390,593 mwaka 2015 hadi 5,880,736 mwaka 2019 sawa na ongezeko la asilimia 146. Hata hivyo, Wizara imechukua hatua ya kuvifuta jumla ya Vyama 3,348 ambavyo vilibainika kuwa ni hewa na hivyo kubaki na jumla ya Vyama vya ushirika 8,611 kwenye daftari/rejista ya Vyama vya ushirika nchini.
(Mheshimiwa Spika maelezo ya kina yametolewa Uk. 46 hadi 48 wa kitabu cha Hotuba)
39. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, thamani ya mikopo inayotolewa na Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 899.2 mwaka 2015 hadi Shilingi trilioni 1.5 mwezi Machi, 2020. Aidha, idadi ya viwanda vinavyomilikiwa na Vyama vya Ushirika imeongezeka kutoka viwanda 304 mwaka 2015 hadi viwanda 379 mwaka 2019.
5.11 Kilimo cha Umwagiliaji
40. Mheshimiwa Spika, eneo la kilimo cha umwagiliaji limeongezeka  kutoka hekta 461,326 mwaka 2015/2016 hadi hekta 694,715 mwaka 2019/20 sawa na ongezeko la asilimia 33.6. Aidha, tija ya uzalishaji katika skimu za umwagiliaji zilizoendelezwa imeongezeka kutoka wastani wa tani 1.8 – 2.0 kwa hekta mwaka 2015/2016 hadi kufikia wastani wa tani 4.0 – 5.0 kwa hekta 2019/2020 kwa zao la mpunga.
41. Mheshimiwa Spika, aidha miradi 179 iliyogharimu shilingi 96,188,597,689.55 imetekelezwa. Kati ya miradi hiyo, miradi 56 inasubiri kuzinduliwa.  Miradi iliyokamilika ni pamoja na mradi wa uboreshaji miundombinu ya skimu ya umwagiliaji ya Dakawa yenye ukubwa wa hekta 2,000 iliyogharimu Shilingi 21,156,050,278; Skimu 9 kati ya skimu 16 zenye ukubwa wa hekta 2,547 za Mradi wa Kuendeleza Skimu za Umwagiliaji za Wakulima Wadogo (SSIDP); ukarabati wa miradi 4 ya skimu za umwagiliaji zenye jumla ya ukubwa wa hekta 2,000 iliyogharimu shilingi 1,166,220,000. (Mheshimiwa Spika maelezo ya kina yametolewa Uk. 48 hadi 50 wa kitabu cha Hotuba)
5.12 Mfumo wa Vibali kwa Njia ya Kielektroniki (ATMIS)
42. Mheshimiwa Spika, mfumo wa vibali kwa njia ya kielektroniki (ATMIS) unaolenga kutoa huduma za utoaji vyeti vya usafi wa mazao ya mimea na vibali vya kuingiza na kuuza mazao nje ya nchi umeanzishwa. Mfumo huo umepunguza muda wa kupata kibali kutoka siku saba (7) za awali hadi siku moja (1) kwa wafanyabiashara. Vilevile, umechangia kudhibiti mianya ya udanganyifu wa nyaraka na kuongeza ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.
5.13 Uanzishwaji wa Kanzidata ya Wakulima
43. Mheshimiwa Spika, Mfumo wa Usajili wa Wakulima (Farmers Registration System-FRS) na kutengeneza kanzidata ya wakulima ambayo itasaidia kuwatambua na kuwapatia vitambulisho, kuainisha mahitaji yao ikiwemo pembejeo za kilimo, huduma za kifedha na masoko na hatimae kuweka mipango ya kuwahudumia umeanzishwa. Hadi Aprili, 2020 jumla ya wakulima 1,275,220 (88.1%) katika mazao nane makuu ya kibiashara ambayo ni korosho, pamba, kahawa, chai, mkonge, pareto, tumbaku na sukari wamesajiliwa kupitia mfumo huo.
5.14 Bima ya mazao
44. Mheshimiwa Spika, serikali kwa kushirikiana na wadau wa huduma za Bima ikiwemo Mamlaka ya Kudhibiti Shughuli za Bima nchini (TIRA), Shirika la Bima la Taifa (NIC), kampuni binafsi tano (5) za bima zimeanzisha Bima ya Mazao kwa lengo la kumsadia mkulima kujikinga na athari za majanga ya asili na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kupata dhamana ya mkopo.
45. Mheshimiwa Spika, Wizara imekamilisha mfumo wa kuwasajili wadau wote wa sekta ya kilimo ikiwemo Sekta Binafsi (Stakeholders mapping). Hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2020, jumla ya wadau wa sekta binafsi 564 wamesajiliwa ambapo Wazalishaji na wasambazaji wa pembejeo ni 198, Wazalishaji wa bidhaa za kilimo 103 na wasindikaji 363. Aidha, jumla ya miradi 105 inayofadhiliwa na Washirika wa Maendeleo yenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.3 imesajiliwa kwenye mfumo. Mfumo huo utaiwezesha Serikali kutambua juhudi na uwekezaji wa wadau wote na kuimarisha ushirikiano kati yao na Serikali katika kuendeleza sekta ya kilimo. (Mheshimiwa Spika maelezo ya kina yametolewa Uk. 55 hadi 58 wa kitabu cha Hotuba)
46. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itaendelea kutekeleza Maeneo 10 ya vipaumbele  kupitia Fungu 43, 24 na 05 katika Idara, Vitengo, Tume na Taasisi za Wizara. Mpango wa bajeti umeweka msisitizo kwenye kilimo kitakachohakikisha upatikanji wa chakula cha kutosha, upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda na kufanya kilimo cha kibiashara.
47. Mheshimiwa Spika, Maeneo ya kipaumbele ni pamoja na Kuendelea na utekelezaji wa Progamu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II); Kuboresha mifumo ya kitaasisi, Bodi na Sheria za Kilimo, kupata ujuzi na maarifa ya kilimo chenye tija, kurahisisha upatikanaji wa huduma za pembejeo na masoko; Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji, maghala, masoko na  miundombinu ya kuhifadhi mazao ya kilimo; na Kuimarisha uzalishaji wa mbegu bora za mazao na upatikanaji wa pembejeo nyingine za kilimo na kuzisambaza kwa wakulima.
48. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara imepanga kutekeleza malengo na shabaha zifuatazo; kuzalisha tani 18,000,000 za mazao ya chakula; kuzalisha jumla ya tani 5,269,858 za mazao ya asili ya biashara yakiwemo pamba (400,000), korosho (300,000), chai (40,000), kahawa (90,000), miwa (4,246,630), pareto (2,800), mkonge (125,428) na tumbaku (65,000); Kuhakikisha upatikanaji wa mbolea tani 760,000; Kuhakikisha upatikanaji wa Mbegu tani 115,000; Kuhakikisha upatikanaji wa Viuatilifu tani 22,000; Kuzalisha tani 8,500,000 za mazao ya bustani; Kuhifadhi chakula kiasi cha tani 300,000; Kusimamia utafutaji na upatikanaji wa masoko ya mazao ya wakulima; Kununua na kuuza tani 500,000 za nafaka na tani 1,200,000 za muhogo mkavu kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB). Aidha, wanafunzi 2,600 kupitia vyuo 14 vya mafunzo ya kilimo watadahiliwa (MATIs); Kukarabati vyuo tisa (9) vya mafunzo ya Kilimo na Vituo vya utafiti wa kilimo vinne (5) na Kuendelea na zoezi la usajili wa Wakulima katika mazao mengine pamoja na usajili wa wadau wa kilimo.
49. Mheshimiwa Spika pia wizara itakamilisha ujenzi na ukarabati wa skimu 17 za umwagiliaji zenye ukubwa wa hekta 8,536; kukamilisha usanifu na upembuzi wa skimu ya Mkombozi-Iringa (hekta 10,000), mabwawa na skimu za Luiche-Kigoma (hekta 3,000) na Ibanda-Sengerema/Geita (hekta 1,200), skimu za Ilemba (Sumbawanga – hekta 800) na Makwale (Kyela – hekta 3,500) pamoja na mabwawa ya Nyisanzi (Chato – hekta 260), Kisese (Kondoa-hekta 2,000), Msia (Mbozi – hekta 100), Idudumo (Nzega-hekta 200) na Masasi (Chato – hekta 530);
na Kujenga maghala 12 yenye uwezo wa kuhifadhi tani 2,000 na kufundisha vijana 400 kuhusu teknolojia ya vihenge vya kisasa kupitia mradi wa TANIPAC. (Mheshimiwa Spika maelezo ya kina yametolewa Uk. 89 hadi 123 wa kitabu cha Hotuba)

7. SHUKRANI

50. Mheshimiwa Spika, kabla sijamaliza hotuba yangu naomba nitoe shukrani za dhati kwa taasisi, makundi, na wadau  mbalimbali tunaoshirikiana katika kuendeleza kilimo cha Tanzania. Kwanza, ninawashukuru kwa dhati  watumishi wote wa Wizara; na wadau wa Sekta ya Kilimo kwa juhudi, ushirikiano na ushauri uliowezesha kutekelezwa kwa majukumu ya Wizara kwa mwaka 2019/2020 pamoja na kuandaa Hotuba hii. Ni matarajio yangu kwamba, nitaendelea kupata ushirikiano wao katika mwaka 2020/2021.
51. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuzishukuru Nchi na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa ambayo yamesaidia katika juhudi za kuendeleza kilimo. Nachukua fursa hii kutaja baadhi yao kama ifuatavyo: Serikali za Japan, Marekani, Uingereza, Ireland, Malaysia, China, Indonesia, Korea ya Kusini, India, Misri, Israel, Ubelgiji, Ujerumani, Finland, Norway, Brazil, Uholanzi, Vietnam, Canada na Poland.  Ninayashukuru pia Mashirika na Taasisi za Kimataifa zifuatazo: Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, AU, IFAD, DFID, UNDP, FAO, JICA, EU, ENABEL, GIZ, UNICEF, WFP, CIMMYT, ICRISAT, ASARECA, USAID, KOICA, ICRAF, IITA, IRRI, ILRI na CABI. Nyingine ni EAC, SADC, AVRDC, AGRA, KILIMO TRUST, CIP, CIAT/PABRA, UNEP, WARDA, Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani (DLCO-EA) na HELVETAS.  Wadau wengine ni Shirika la Kudhibiti Nzige Wekundu (IRLCO-CSA),Bill and Melinda Gates Foundation, Gatsby Trust, Rockfeller Foundation, Clinton Foundation, Aga Khan Foundation, Unilever, Kampuni za TAHA fresh Limited, Africado na Rugwe Avocado Companyna Asasi zisizo za kiserikali nyingi ambazo hatuwezi kuzitaja zote hapa.
52. Mheshimiwa Spika,natoa shukrani za wakulima wote nchi nzima kwa kazi kubwa wanazofanya kuendeleza kilimo nchini. Ni wazi kuwa mafanikio haya makubwa ya kilimo yanatokana na jududi na ushirikiano mkubwa na serikali. Kipeke nirudie kuwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Vwawa kwa namna wanavyoniunga mkono na kunipa ushirikiano. Naomba wote watumbue kuwa kilimo ni chakula, maisha, uchumi, biashara, viwanda na ajira. 8. MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2020/2021

8. MAOMBI YA FEDHA ZA BAJETI KWA MWAKA 2020/2021

8.1 Makusanyo ya Maduhuli

53. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara inatarajia kukusanya Shilingi 5,793,400,000 kutokana na ada za ukaguzi wa mazao yanayouzwa nje ya nchi au kuingizwa nchini, uuzaji wa nyaraka za zabuni, ukodishaji wa mitambo ya Tume ya Umwagiliaji.

8.2 Fedha kwa Mafungu yote (43, 24 na 05)

54. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara ya Kilimo inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe  jumla ya Shilingi 229,839,808,000 kupitia Fungu 43, Fungu 05 na Fungu 24 kama ifuatavyo;

8.2.1 Fedha kwa Fungu 43

55. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 202,504,117,000 kupitiaFungu 43 kwa ajili ya matumizi ya Kawaida na Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi 137,273,144,000 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maendeleo. Aidha, Shilingi 65,230,973,000 ni kwa ajili yamatumizi ya kawaida, ambapo Shilingi 43,599,187,000 ni kwa ajili ya mishahara na Shilingi 21,631,786,450 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.

8.2.2 Fedha kwa Fungu 05

56. MheshimiwaNaibu Spika, jumla ya Shilingi 17,726,845,000 zinaombwa. Kati ya fedha hizo, Shilingi 12,801,180,000 ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo na, Shilingi 4,925,665,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Shilingi 4,040,481,000 ni kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi wa Tume na Shilingi 885,184,000 ni kwa ajili ya Matumizi mengineyo.

8.2.3 Fedha kwa Fungu 24

57. Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi 9,608,846,000 zinaombwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapo Shilingi 7,059,837,000ni kwa ajili ya mishahara na Shilingi 2,549,009,000ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.
58. Mheshimiwa  Naibu Spika, hotuba hii pia inapatikana katika tovuti ya Wizara: www.kilimo.go.tz 
Mheshimiwa Spika, NAOMBA KUTOA HOJA
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com