Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb) akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Matumizi ya kawaida ya wizara hiyo ya mwaka 2020/2021. Leo tarehe 12 Mei 2020 (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha jumla ya Shilingi 229,839,808,000 kwa ajili ya Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kugharamia matumizi ya kawaida na miradi mbalimbali ya maendeleo ya Sekta ya Kilimo kwa mwaka wa Fedha wa 2020/2021
Waziri Hasunga amesema kuwa kilimo kimeendelea kuwa ni mhimili muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania Katika kipindi cha miaka mitano, Pato la Taifa linalotokana na kilimo, kwa kutumia bei za Mwaka 2015 limeongezeka kwa asilimia 17 kutoka shilingi trilioni 25.2 Mwaka 2015 hadi shilingi trilioni 29.5 Mwaka 2019.
Vilevile, sekta imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 58 Mwaka 2018, imechangia asilimia 28.2 ya Pato la Taifa ambapo sekta ndogo ya mazao imechangia asilimia 16.2. Hii imetokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo vyakula vinavyotokana na mazao ya kilimo. Aidha, kati ya mwaka 2015 hadi 2019 sekta ya kilimo imeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 5.2 ambapo sekta ndogo ya mazao imeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 5.8
Waziri Hasunga amesema kuwa katika mwaka 2019/2020, Wizara imeendelea kutekeleza maeneo ya kipaumbele ya kuongeza uzalishaji na tija kwenye kilimo kwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, udhibiti wa visumbufu, matumizi ya zana bora za kilimo na huduma za ugani; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji; ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi mazao ya kilimo na masoko; kufanya utafiti wa kilimo na kuzalisha teknolojia kwa mazao ya mahindi, muhogo, ngano, michikichi, ufuta, alizeti, pamba na mpunga.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka minne Wizara imepata mafanikio makubwa katika maeneo ya usalama wa chakula na lishe; uzalishaji wa mazao makuu ya biashara; upatikanaji wa pembejeo za kilimo; viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na masoko; utafiti, huduma za ugani na mafunzo; hifadhi ya mazao; uzalishaji wa mazao ya bustani; kuimarika kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko; kuimarika kwa ushirika; kuimarika kwa kilimo cha umwagiliaji; ongezeko la ushiriki wa vijana katika kilimo; matumizi bora ya ardhi; kuhuisha mifumo na sera za kilimo na kuanzishwa kwa kanzidata ya wakulima na wadau mbalimbali wa kilimo.
Mhe Hasunga amesema kuwa kulingana na taarifa ya mapitio ya kati (Mid Term Review) ya hali ya lishe nchini katika utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa lishe wa mwaka 2016-2021) uliyofanyika mwaka 2019, inaonesha kuwa udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano umepungua kutoka asilimia 34 mwaka 2015 kufikia asilimia 32 mwaka 2018.
Aidha, Kiwango cha ukondefu kwa watoto chini ya miaka mitano kitaifa kimeendelea kushuka kutoka asilimia 3.8 hadi asilimia 3.5 na pia upungufu wa damu kwa akina mama umepungua kutoka asilimi 44.7 hadi kufikia asilimia 28.7 kwa kipindi hicho.
Amesema kuwa uzalishaji wa mazao makuu ya biashara yakiwemo pamba, kahawa, chai, pareto, tumbaku, korosho, mkonge na miwa umeongezeka kutoka jumla ya tani 796,502 Mwaka 2015/2016 hadi jumla ya tani 1,144,631 Mwaka 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia 43.7. Aidha zao la miwa limeongoza likifuatiwa na korosho na Pamba.
Vilevile katika kipindi hicho cha miaka minne kiasi cha tani 1,613,000 za mazao ya kahawa, pamba, katani, chai, tumbaku na korosho kiliuzwa nje ya nchi na kuliingizia Taifa jumla ya Dola za Marekani Milioni 3,419.77 sawa na Shilingi trilioni 6.9. Aidha, Wizara kupitia Bodi ya Tumbaku imeuza jumla ya tani 500 za tumbaku ya daraja la chini (Reject) ambayo mapato yake yamesaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima na kuwaongezea kipato.
Waziri Hasunga amesema kuwa Mahitaji ya sukari nchini ni takribani tani 420,000 ikiwa ni wastani wa tani 35,000 kwa mwezi, Uzalishaji wa Sukari kwa mwaka 2019/2020 ulikadiliwa kuwa tani 380,000, kulingana na matarajio ya uzalishaji huo upungufu wa Sukari ulikadiliwa kuwa wastani wa tani 40,000 kwa matarajio kwamba viwanda vingeweza kuzalisha kiasi chote cha Sukari cha tani 380,000 kilichokadiliwa mwanzoni mwa msimu.
Aidha, amesema kuwa kutokana na mvua kunyesha kupita kiasi viwanda havikufikia Malengo ya uzalishaji ambapo vilizalisha tani 310,000 hivyo pengo la mahitaji kuongezeka kutoka tani 40,000 hadi kufikia tani 110,000.
“Hata hivyo, kwa vile viwanda vya ndani vinatarajia kuanza uzalisha mwezi Juni, 2020 ni matarajio ya serikali upatikanaji wa Sukari utarejea katika hali yake ya kawaida” Alikaririwa Mhe Hasunga
Ameongeza kuwa ili kukabiliana na upungufu huo, Serikali ilichukua hatua ya kutoa vibali vya tani 40,000 kwa wazalishaji wa ndani wanne (4) kuingiza Sukari ambapo kila mzalishaji alipewa kibali cha kuingiza tani 10,000.
Hadi sasa kiasi cha tani 14,398 kimekwisha ingizwa na kusambazwa nchini, kiasi cha tani 3,920 kipo katika hatua mbalimbali za kutolewa bandarini na kiasi cha tani 21,166 kinatarajiwa kuingizwa nchini kabla ya mwisho wa mwezi Mei, 2020. Kutokana na tatizo la mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 wafanyabiashara wachache wasio waadilifu wamekuwa wakihodhi Sukari na kusababisha kupanda bei.
Hata hivyo, serikali inafuatilia mwenendo wa uingizwaji wa Sukari na kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha kunakuwa na utulivu wa soko.
Serikali inalenga kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 320,000 za sasa hadi 630,000 ifikapo mwaka 2024/2025 kutokana na uwekezaji mpya na upanuzi wa viwanda vilivyopo na hivyo kujitosheleza kwa mahitaji ya Sukari nchini. Hata hivyo, serikali itaendelea kutoa vibali vya kuziba pengo la uzalishaji Sukari nchini kwa wakati ilikuhakikisha Sukari inapatikana nchini kwa wakati wote.
Kuhusu mazao ya bustani waziri Hasunga amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne, uzalishaji wa mazao ya bustani umeongezeka kutoka tani 5,931,900 mwaka 2015/2016 hadi tani 6,556,102 mwaka 2018/2019.
Amesisitiza kwua Thamani ya mauzo ya mazao ya bustani yakiwemo mbogamboga na maua nje ya nchi yameongezeka toka Dola za Marekani milioni 412 mwaka 2015 hadi Dola za Marekani milioni 779 mwaka 2018/2019. Ongezeko hilo la mauzo linaifanya Tasnia ya mazao ya bustani kuchangia asilimia 38 ya fedha za kigeni zinazotokana na sekta ya kilimo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment