METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, April 30, 2020

SERIKALI HAITOPANGA BEI ZA MAZAO YA WAKULIMA-MHE MGUMBA

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akisisitiza jambo leo tarehe 30 Aprili 2020 wakati akizungumza na viongozi wa TADCOs Co ltd kuhusu hatua iliyofikiwa ya uagizaji wa mbolea katika ukumbi wa KILIMO IV Jijini Dodoma.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Serikali imesisitiza kuwa haitopanga wala kuingilia bei za mazao ya wakulima nchini badala yake wakulima watajipangia bei na kuuza wenyewe ilihali serikali ikisalia kama msimamizi.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 30 Aprili 2020 wakati akizungumza na viongozi wa TADCOs Co ltd kuhusu hatua iliyofikiwa ya uagizaji wa mbolea katika ukumbi wa KILIMO IV Jijini Dodoma.

Mhe Mgumba amesema kuwa mfumo wa biashara ulivyo unategemea zaidi ujazo wa mazao sokoni, hivyo bei haitolewi kutokana na gharama alizotumia mkulima wakati wa uzalishaji badala yake bei inaendana na soko.

Amesema kuwa wakulima kama wanavyoruhusiwa kuzalisha kadhalika wakulima hao watauza mazao yao popote watakapotaka wao lakini kwa kufuata taratibu na sheria za nchi.

Kuhusu Mfumo wa stakabadhi ghalani Naibu Waziri Mhe Mgumba amesema kuwa mfumo huo ulianzishwa kwa lengo la kumrahisishia huduma za biashara mkulima hivyo utaendelea kutumika kwa mujibu wa matakwa ya kuanzishwa kwake.

Amesema kuwa zipo changamoto nyingi katika utekelezaji wa mfumo huo unaochagizwa na viongozi wanaosimamia hususani wa vyama vya Ushirika kutotekeleza kwa mujibu wa sheria.

“Mtu akipeleka mazao yake ghalani lengo la serikali kwa sababu mazao yote tunategemea msimu wa mvua na upatikanaji wake ni wa wakati mmoja hivyo kuhifadhi kwa pamoja na kupewa stakabadhi itakayomrahisishia kupata mkopo kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake wakati akisubiri gharama za mazao zikipanda aweze kuuza kwa bei nzuri” Alikaririwa Mhe Mgumba

Mhe Mgumba ameongeza kuwa mfumo huo ni mzuri endapo utaendelea kusimamiwa vizuri ikiwa ni pamoja na kuendelea kuuboresha zaidi ili uwanufaishe wakulima kote nchini kwani mfumo huo unapunguza gharama za uendeshaji.

Ameeleza kuwa miongoni mwa changamoto waliyokuwa nayo wakulima ilikuwa ni Tija ndogo katika mavuno yao yaliyosababishwa na matumizi madogo ya mbolea hivyo serikali ilitoa elimu ya kutosha kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea hivyo katika kipindi cha serikali ya awamu ya tano tija imeongezeka.

Mgumba amesema kuwa matumizi sahihi ya mbolea yameongeza tija katika sekta ya kilimo kwani uzalishaji umeongezeka na wakulima wamekuwa na kipato kikubwa.

Katika kikao kazi hicho Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba amesema kuwa nchi ina mbolea ya kutosha ambapo ina akiba ya zaidi ya Tani 203,000 iliyotokana na uagizaji wa mbolea uliofanywa kwa mwaka mzima wa kiasi cha mbolea Tani 633,197

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com