Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya
Michezo wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bw.Yusuph Singo akifafanua kuhusu usajili wa
wanamichezo wa kigeni hapa nchini leo Aprili 29,2020 Jijini Dodoma.
Serikali haijatoa ukomo wa
wachezaji kutoka nje kushiriki michezo hapa nchini bali imeibua mjadala kwa
wadau ili watoe maoni yao.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma
na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw.Yusuph Singo kutoka Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiwa ni hatua ya kuboresha na kuimarisha
sekta ya michezo nchini.
Ili kutekeleza mjadala huo,
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limepewa jukumu la kuendelea kuandaaa mwongozo
utakaotumika kukusanya maoni kutoka kwa wadau kuhusu ukomo wa wanamichezo wa
nje hapa nchini.
“Katika Hotuba ya Bajeti
iliyosomwa hivi karibuni Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe, hakuongolea idadi ya wachezaji
kutoka nje wanaotakiwa kucheza nchini, bali aliagiza BMT kuandaa mjadala mpana
katika kukusanya maoni kwa wadau wa michezo kuhusu namna bora ya kusajili
wachezaji wa kigeni katika michezo yote hapa nchini” alisema Bw. Singo.
Pamoja na hayo, Mkurugenzi huyo
ambainisha kuwa Mhe.Waziri Dkt. Mwakyembe alisisitiza kuwa wanamichezo wote
kutoka nje ya nchi wanaosajiliwa hapa nchini ni lazima wawe na ubora pamoja na
viwango vinavyotakiwa.
Akifafanua suala hilo Bw. Singo
amesema kuwa michezo yote ya kulipwa kwa sasa imeendelea kukua duniani kote na
nchi yetu pia inayo wachezaji wengi wanaocheza michezo hii ikiwemo Mpira wa
Kikapu (Basketball), Kriketi, Mpira wa Miguu na michezo mingine, hivyo,
Serikali haijatoa maelekezo ya ukomo wa usajili wa idadi ya wachezaji bali
inataka kuwepo kwa mjadala wa wazi utakaotoa mwongozo wa ukomo wa idadi ya
usajili wa wachezaji wa kigeni.
Aidha, Mkurugenzi huyo alitoa rai
kwa wadau wa michezo nchini watakapopata fursa ya kuchangia au kutoa maoni katika
mjadala huo wasiegemee katika timu wanazoshabikia, bali watoe maoni ambayo
yatasaidia kuendeleza michezo na kuendeleza vipaji vya wanamichezo wetu pamoja
na kukuza michezo nchini.
0 comments:
Post a Comment