Mwenyekiti wa Bodi ya Bodi ya
Utalii Tanzania (TTB), Jaji Mstaafu Thomas Mihayo akizungumza na Waandishi wa
Habari katika Mkutano wa Bodi uliofanyika Jijini Dar es Salaam Aprili,
29, 2020.
BODI ya Utalii Tanzania (TTB)
imeainisha mikakati 10 ya muda mrefu inayolenga kuinua soko la utalii nchini
ambalo kwa sasa limeathirika na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu
(CORONA) unaosababishwa na kirusi cha (COVID-19) na kuenea katika nchi
mbalimbali duniani.
Hayo yamesemwa leo Jumatano
(Aprili 29, 2020) Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya (TTB) Jaji
Mstaafu Thomas Mihayo wakati wa mkutano na Waandishi wa vyombo vya habari
kuelezea athari za mlipuko ugonjwa wa CORONA na tathimini ya sekta ya Utalii
nchini.
Alisema kuwa kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa na Shirika la Utalii Duniani (UNWTO), inaonesha kuwa
mlipuko wa ugonjwa wa CORONA utasababisha kushuka kwa kiwango cha kati ya
asilimia 20-30 ya idadi ya watalii kwa mwaka 2020 pamoja na kusababisha ukosefu
wa mapato kiasi cha Dola za Marekani 300-450 Bilioni duniani.
Akifafanua zaidi Jaji Mihayo
alisema pia utabiri wa awali uliofanywa na Shirika lisilo la kiserikali
linaloshauri nchi na taasisi za kimataifa la DEFC unaonesha kuwa mwenendo wa
uchumi duniani umebadilika na utaendelea kubadilika ambapo sekta za utalii na
usafiri wa anga ziilizokuwa zimeshamiri, kwa sasa zitakuwa za mwisho kwenye
uchangiaji wa ukuaji wa uchumi duniani.
‘’Sekta ya Utalii nchini Tanzania
inachangia takribani asilimia 17-17.5 ya mapato ya Serikali (GDP) ambapo kwa
mwaka 2018 Tanzania ilitembelewa na watalii wapatao 1,505,702 kutoka watalii
1,327,143 wa mwaka 2017, hivyo janga la
virusi vya CORONA limeleta athari kwenye soko la utalii duniani na hapa nchini
pia kwenye sekta zinazowezesha sekta ya utalii’’ alisema Jaji Mihayo.
Aidha Jaji Mihayo aliitaja
mikakati endelevu iliyowekwa na TTB katika kuendeleza na kukuza sekta ya utalii
nchini ni pamoja na kushirikiana na wadau wa utalii kuandaa mkakati wa pamoja
wa kukabiliana na janga la COVID-19 kwenye sekta ya utalii, kuandaa mkakati
mpya wa mauzo wa kimataifa kupitia ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani
(USAID) na kushirikisha watu mashuhuri na mabalozi wa utalii Tanzania kwa ajili
ya kutangaza utalii.
Aliitaja mikakati mingine ni
pamoja na kuimarisha timu ya mauzo kubuni mbinu za kisasa na kitaalamu zenye
ubunifu wa kuandaa mikakati ya mauzo ya
mtandao, kutangaza utalii wa ndani kupitia programu maalum za mashule na
vyuo vya elimu pamoja na kushirikiana na Balozi za Tanzania nje ya nchi kuweka
mikakati bayana ya kuwapata mabalozi wa TTB.
Kwa mujibu wa Jaji Mihajo alisema
mara baada ya kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa CORONA, TTB ilianza kuchukua
tahadhari mbalimbali ikiwemo kuandaa na kurusha makala fupi ya dakika 1.5
iliyosambaa duniani kuhamasisha watalii kujikinga na COVID-19 na kuwakumbusha
wasifute safari zao za utalii nchini Tanzania.
‘’Makala hiyo fupi imezunguka
kwenye masoko yetu yote makubwa duniani na imevuka matarajio ya awali ya
kiwango cha watu waliyoiona na pia makala hiyo imeoneshwa kwenye vituo vyetu
vya Televisheni na kuwekewa lugha za kiarabu, kifaransa, kijerumani na
kidachi’’ alisema Jaji Mihayo.
Jaji Mihayo alisema TTB, Shirika
la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro (NCAA)
wameingia ubia na kampuni ya Great Migration Camp kwa pamoja wamebuni kipindi
maalum kinachoitwa ‘’Serengeti Live Show’’, kinachorushwa mubashara na vingine
kurekodiwa na kurushwa kwa awamu kwenye mitandao ya TTB na washirika wake
nchini na nje ya nchi kuonesha utalii wa Tanzania.
Aliongeza kuwa madhumuni ya
vipindi hivyo ni kukonga mioyo ya watalii ambao wameahirisha safari zao za kuja
Tanzania kwa kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa CORONA, ambapo kupitia
vipindi hivyo Tanzania itahakikisha kuwa Jina maalum la kutangaza utalii wa
Tanzania la Tanzania Unforgettable
linaendelea kutumia ili kuhamasisha sekta ya utalii nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa TTB, Devotha Mdhachi alisema mwezi Mei mwaka huu Ofisi yake
inatarajia kufanya kikao na wadau wa sekta ya utalii nchini ili kujadili
mikakati ya pamoja inayolenga kuimarisha soko la utalii nchini katika kipindi
hiki ambacho dunia inakabiriwa na mlipuko wa ugonjwa wa CORONA.
0 comments:
Post a Comment