Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe ( wa pili kutoka kulia) akipatiwa maelezo na mtaalam wa TBS kuhusu upimaji wa bidhaa mbalimbali unaofanyika katika maabara ya uhandisi mitambo,kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt Athuman Ngenya.
Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt Athuman Ngenya akisisitiza jambo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe wakati wa ziara yake katika Shirika hilo hivi karibuni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt Athuman Ngenya na watendaji wengine wa Shirika hilo mara baada ya ziara yake katika Shirika hilo hivi karibuni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe amewataka watumishi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS),kuepuka vishawishi katika utendaji kazi ili nchi iwe salama na kuvutia wawekezaji zaidi.
Prof. Shemdoe aliyasema hayo hivi karibuni alipotembelea TBS kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.
Prof. Shemdoe alisema ili kuwezesha biasharaTBS inapaswa kufanya kazi kwa uadilifu na kuepuka urasimu ambao unakwamisha biashara na kukatisha tamaa wawekezaji wapya.
“Tunapaswa kushirikiana katika utendaji kazi na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa manufaa ya taifa,” alisisitiza Prof. Shemdoe na kuongeza kuwa kwa sasa Tanzania iko nafasi ya 141 Duniani katika urahisi wa ufanyaji wa biashara hivyo jitihada zaidi zinahitajika ili luwa katika nafasi nzuri zaidi.
Alisema Wizara ya Viwanda na Biashara ndiyo inayotekeleza Blue Print kwa kuhakikisha kuwa vikwazo vyote vya kibiashara vinaondolewa na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya akimkaribisha Katibu Mkuu aliyeambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Ludovick Nduhiye, alimhakikishia Katibu Mkuu kuwa Shirika hilo litaendelea kufanyakazi katika kiwango kinachotakiwa licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa vifaa vya kisasa vya maabara ili kwenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Dkt. Ngenya alisema Shirika limeendelea kujizatiti katika kuhakikisha kuwa soko la Tanzania linakuwa na bidhaa bora pekee ikiwa ni pamoja na kuendelea kufungua ofisi mipakani na Kanda,ambazo zinatoa huduma kwaa haraka tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo huduma za TBS zilikuwa zinapatikana Dar es Salaam pekee.
Alisema mwezi Desemba 2019 Shirika lilifungua ofisi mpya ya Kanda ya Magharibi mkoani Kagera ambayo kwa sasa inahudumia mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa. Kufunguliwa kwa kanda ya Magharibi kumefanya idadi ya Kanda kwa sasa kufikia sita.
Alizitaja kanda zingine zilizopo ni ya Kati Dodoma (Dodoma, Singida na Tabora), Nyanda za Juu Kusini Mbeya (Mbeya, Iringa, Njombe, na Songwe), Kanda ya Kusini Mtwara (Mtwara,Lindi na Ruvuma) Kanda ya Kaskazini Arusha(Arusha,Kilimanjaro,Manyara na Tanga na Kanda ya Ziwa Mwanza (Mwanza,Kagera,Mara, Geita, Simiyu na Shinyanga).
Dkt. Ngenya pia alisema TBS imefungua ofisi katika viwanja vya ndege vya Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza na katika Bandari za Mwanza, Tanga, Dar es Salaam na Bagamoyo.
Alizitaja ofisi za mipakani ni pamoja na Rusumo, Kabanga, Kasumulo,Tunduma,Holili,Horohoro,Namanga, Sirari,Mutukula, Tarakea na Mtambaswala.
0 comments:
Post a Comment