Chama cha Ushirika cha Natta AMCOS LTD kiliopo Kata ya Natta Mbiso Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kimevunjwa bodi pamoja na menejimeti yake baada ya uchunguzi kubaini kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha wa kiasi cha shilingi milioni 29.
Katika taarifa yake Msimamizi Mkuu wa Vyama vya Ushirika Kija Maheda, ilibainisha Natta AMCOS LTD inaendeshwa bila kuzingatia sheria taratibu na kanuni japo kuwa ina miradi mingi ikiwemo mashamba zaidi ya ekari 100, vibanda, na jengo la ofisi lakini mapato yake hayawasaidii wanachama na jamii iliyopo Natta.
"Imekuwa ni jambo la kawaida kwa viongozi wa AMCOS hii kutumia fedha za Natta AMCOS kwa manufaa yao wenyewe pia kutumia fedha za ushuru wa pamba kujilipa posho kubwa bila kuzingatia bajeti ya Mrajis na kushindwa kupeleka hesabu kwa wakaguzi wa nje," amesema Mrajis Maheda.
Maheda amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatambua kuwa vyama vya Ushirika ni silaha ya wanyonge na nguzo kuu ya ujenzi wa uchumi wa nchi katika kufikia malengo na mipango ya maendeleo kwa wananchi.
Kwa upande wake Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Serengeti Emmanuel Liguda, amesema kuwa katika maelezo ya awali ya viongozi wa Natta AMCOS LTD tayari amebaini kuna matumizi mabaya ya fedha za fedha za washirika na mnyororo wa kutoa na kupokea rushwa na kuahidi kufikishwa juu ya sheria viongozi waliohusika pindi uchunguzi zaidi utakapokamilika.
Naye Bi. Petronia Joseph ni mmoja kati ya wanachama wa Natta AMCOS LTD, alimpongeza Mrajis kwa uamuzi wa alioufanya kutokana na chama hicho kutoitisha mikutano mikuu ya kila mwaka na kushindwa kuwasilisha makisio ya mapato na matumizi kwa wakati jambo linalopelekea kutopata haki yao ikiwemo fedha za gawio litolewalo na ushirika kwa mwanachama anayetambulika na aliyefikia hatua ya kupewa.
Aidha Bi. Joseph, ameongeza kuwa mali zote za chama hicho walitafuta wao wakiwa vijana ili ziwatunze uzeeni cha kushangaza wamekuwa wakidharauliwa na viongozi wanapodai fedha za kujikwamua na kuambiwa umri wao kwa sasa hauchangii chochote katika chama hivyo hawapaswi kudai fedha za chama.
0 comments:
Post a Comment