METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, March 7, 2020

ILEMELA WATUMISHI BONANZA KUIMARISHA AFYA ZA WAFANYAKAZI.

Bonanza la Michezo kwa Watumishi wa halmashauri ya manispaa ya Ilemela litakuwa likitumika kwaajili ya kuimarisha afya za watumishi wote wanaofanya kazi katika manispaa hiyo na kuongeza ufanisi wa kuwahudumia wananchi wanaoishi ndani ya wilaya ya Ilemela.

Kauli hiyo imetolewa na afisa utamaduni wa manispaa ya Ilemela ambae pia ndie mgeni rasmi wa Bonanza hilo ndugu Ernest Biseko ambapo amewataka watumishi wanaofanya kazi katika wilaya hiyo kuwa wanajitokeza kila robo ya mwaka yanapofanyika mashindano hayo na kuitumia fursa hiyo kuimarisha afya zao kwa kupambana na magonjwa yasiyoambukiza sanjari na kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi kwani michezo hiyo huifanya akili kukaa sawa kwa kupunguza msongo wa mawazo na wakati mwengine inaweza kutumika kama ajira mbadala 

' Niwapongeze kwa kujitokeza katika bonanza hili lakini nawaomba tutumie michezo hii kwa kuimarisha afya zetu dhidi ya magonjwa na itusaidie kuongeza ufanisi tunapohudumia wananachi katika maeneo yetu ya kazi ' Alisema

Aidha ameongeza kuwa bonanza la michezo katika manispaa ya Ilemela linaenda sambamba na utekelezaji wa agizo la makamu wa rais ambae pia ndie mlezi wa manispaa ya Ilemela Mhe Samia Suluhu Hassan la kuwataka wananchi kujihusisha na mazoezi ili kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa upande wake afisa michezo wa manispaa ya Ilemela ndugu Kizito Bahati amefafanua kuwa bonanza hilo litakuwa likifanyika kila robo ya mwaka ya kiserikali kwa kukutanisha timu za watumishi wa kada tofauti kutoka maeneo yote ya manispaa hiyo kwa michezo ya mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa mikono na kuvuta kamba huku akiwashukuru wadau waliounga mkono bonanza hilo wakiwemo Mwanza 2020 Soap Industry  sambamba na kuwaomba wengine kujitokeza kwa kipindi kijacho.

Mpaka kuisha kwa bonanza hilo  katika mchezo wa mpira wa miguu timu ya watumishi kutoka kata ya pasiansi iliibuka kidedea kwa kuicharaza vikali timu ya watumishi wa kutoka kata ya kayenze kwa goli mbili kwa moja huku mpira wa pete timu ya watumishi kutoka makao makuu iliibuka mshindi dhidi ya timu ya watumishi kutoka kata ya nyakato wakati katika mpira wa wavu timu ya watumishi kutoka kata ya pasiansi iliyoungana na timu ya watumishi bugogwa waliibuka kidedea dhidi ya timu ya watumishi kutoka kata ya mecco walioungana na nyakato.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com