METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, March 4, 2020

TUTAWASAJILI NA KUWAPATIA VYETI VYA KUZALIWA WATOTO WOTE NDANI YA MIEZI MITATU


Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Christina  Mndeme ametoa maagizo kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo kuanza uhamasishaji na utoaji elimu kwa wananchi kuelekea maandaalizi ya utekelezaji wa mpango wa usajili kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano.

Akitoa maagizo hayo hii leo  manispaa ya songea wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku moja kwa viongozi wa Mkoa huo amesema kuwa kila kiongozi anawajibika kwa nafasi yake  kusimamia na kuhakikisha watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano na wale wanaozaliwa kila siku wanasajiliwa na kupatiwa vyeti vyaa kuzaliwa.

Ameongeza kuwa mpango huo ni wa Serikali na hivyo  utasaidia kupata takwimu sahihi zitakazotumika katika upangaji wa mipango ya maendeleo na kupeleka huduma za kijamii kwa wananchi kama vile afya na elimu.

‘’Naagiza viongozi wenzangu, hakikisheni tunasajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wote wa umri huo kwa asilimia mia moja ndani ya miezi mitatu’’.Alisema Mhe Mndeme.

Kwa upande wake kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA Bi Emmy Hudson amesema kuwa Kwa sasa Serikali imesogeza huduma ya usajili karibu na maeneo ya makazi ya wananchi hivyo kuwaondolea wananchi changamoto ya kusafiri umbali mrefu na kutumia gharama nyingi kuweza kupata huduma hii. 

Bi Hudson ameongeza kuwa watoto wote wa umri huo  wanasajiliwa na kupatiwa vyeti papo hapo tena bila malipo yoyote ya ada yaani ni (bure), pia huduma hiyo inapatikana katika vituo vya tiba vinavyotoa huduma ya mama na mtoto na Ofisi za watendaji kata ukilinganisha na awali ambapo walilazimika kwenda katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya aliyozaliwa mtoto. 

‘’Maboresho yaliyofanyika ya mfumo wa usajili yamewezesha mpaka sasa kusajili zaidi ya watoto 4,082,424 na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa kupitia mpango huu hivyo kupandisha wastani wa kitaifa wa watoto waliosajiliwa kutoka asilimia 13 na kufikia asilimia 49’’.Alisema Bi Hudson.

Mkoa wa Ruvuma umeanza kutekeleza mpango huo na utakuwa wa Mkoa wa kumi na sita miongono mwa Mikoa inayotekeleza mpango huo, mikoa mingine kumi na tano inayoendelea kutekeleza ni Mbeya, Songwe, Mwanza, Iringa, Njombe, Geita, Shinyanga, Mtwara, Lindi, Mara, Simiyu, Dodoma, Singida, Morogoro na Pwani.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com