Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati alipofungua kikao kazi cha Menejimenti ya wizara, taasisi na bodi za mazao zilizo chini ya wizara ya Kilimo tarehe 23 Januari 2020 jijini Dodoma. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza ulazima wa serikali kuzalisha mbegu za mazao ya kilimo nchini wakati alipofungua kikao kazi cha Menejimenti ya wizara, taasisi na bodi za mazao zilizo chini ya wizara ya Kilimo tarehe 23 Januari 2020 jijini Dodoma.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati alipofungua kikao kazi cha Menejimenti ya wizara, taasisi na bodi za mazao zilizo chini ya wizara ya Kilimo tarehe 23 Januari 2020 jijini Dodoma.
Na
Revocatus Kassimba, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Waziri wa Kilimo Japhet
Hasunga ameagiza wataalam wa wizara na taasisi za wizara ya Kilimo nchini
kutumia utaalamu na uwepo wa fursa nzuri ya umwagiliaji kuzalisha mbegu bora kwa
matumizi ya wakulima.
Amesema kauli hiyo tarehe 23 Januari 2020
jijini Dodoma wakati alipofungua kikao kazi cha Menejimenti ya wizara, taasisi
na bodi za mazao zilizo chini ya wizara
ya Kilimo.
Hasunga amesema Tanzania
haina haja ya kutegemea mbegu za mazao toka nje wakati ina eneo linalofaa kwa
uzalishaji la kutosha na wataalam wabobezi kwenye sekta ya uzalishaji mazao ya
kilimo.
“Tunataka mbegu zizalishwe
kipindi cha kiangazi kupitia kilimo cha umwagiliaji, ili wakati wa mvua wakulima
wapande wala sio muda wa kuzalisha mbegu” alisema Hasunga
Waziri Hasunga ametoa takwimu
kuwa kwa sasa Tanzania inatumia tani 186,000 za mbegu ambapo uzalishaji ndani
ya nchi ni chini ya tani 71,000 kwa mwaka hali inayosababisha kuendelea
kutegemea mbegu zinazozalishwa nje.
Ameitaja changamoto ya
upungufu wa mbegu za miche ya chai, korosho, michikichi, kahawa, mihogo na jamii ya mikunde hivyo kuchangia ukuaji
mdogo wa tasnia za mazao hayo.
Waziri huyo wa kilimo
aliwaambia watendaji na watalaam wa wizara yake kuwa tayari Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kuwa nchi iwe na mkakati
maalum wa kuongeza uzalishaji kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji.
Hasunga amesema katika
kutekeleza agizo la Rais Magufuli, wizara yake tayari imeagiza taasisi zake
kutumia fursa ya umwagiliaji kuongeza uzalishaji mbegu nchini.
Amesema Tanzania ina eneo
linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji hekta milioni 29.4 ambapo zinazomwagiliwa
hadi sasa ni hekta 475,000 tu hivyo wataalam wahakikishe mbegu zinazalishwa kwa
wingi muda wote wa mwaka.
Wakati huo huo Waziri Hasunga
ameonya dhidi ya kuongezeka kwa mbegu, mbolea na viuatilifu visivyo bora(fake)
hali inayowaumiza na kusababisha hasara kwa wakulima nchini.
“Madawa na viuatilifu ambayo
hayaruhusiwi kutumika yapo mengi sana. Hata mimi (Waziri) mwaka jana nilipigwa
madawa yasiyo na ubora katika shamba langu Songwe na magugu hayakufa “ alitoa
mfano Waziri Hasunga.
Kwa upande wake Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Kilimo Prof.Siza Tumbo amemhakikishia Waziri kuwa watendaji wa
wizara na taasisi zake wataendelea kutekeleza maagizo ya serikali muda wote ili
tija katika uzalishaji mazao nchini iongezeke.
Kikao hiki cha Menejimenti ni
cha nne tangu Waziri Hasunga alipoteuliwa kuongoza wizara hiyo mwaka 2018
ambapo taarifa za utendaji kazi hujadiliwa pamoja na kuweka mpango wa
utekelezaji kwa nusu ya pili ya mwaka 2020 iliyobakia.
Wizara ya kilimo ina bodi za
mazao na taasisi zinazojitegemea jumla 22 ambapo wakurugenzi wakuu na wenyeviti
wake wa bodi wote wanashiriki kikao hiki
cha Waziri wa Kilimo mwaka huu.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment