METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, March 2, 2018

MAVUNDE ATUA TANGA AWATAKA WAAJIRI KUWAPA MIKATABA WAFANYAKAZI KWA MUJIBU WA SHERIA, ATOZA FAINI VIWANDA

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Antony Mavunde amewataka waajiri kote nchini, kubadilika na kufuata Sheria ya ajira na mahusiano kazini vinginevyo mkono wa sheria utawafikia.

Katika kusimamia utekelezaji wa Sheria  za masuala hayo ya kazi,Mavunde ametoa siku thelathini(30) kwa Waajiri kuwapa mikataba wafanyakazi wao kwa mujibu wa Sheria na pia amekipiga faini  ya *Tsh 35,000,000* kiwanda cha *PEE PEE LTD* kwa kushindwa kuwapa wafanyakazi wake vifaa kinga na hivyo kuhatarisha usalama wao wakiwa kazini.

Sambamba na hilo, Mhe. Mavunde amesema, serikali haitabadili msimamo wake wa kuwafikisha mahakamani waajiri wote ambao bado hawajatekeelza takwa la kisheria la kujisajili na kupeleka michango kwenye Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF) kwani kwa kutofanya hivyo wanakabiliwa na adhabu mbalimbali ikiwemo kupelekwa mahakamani ambapo mwajiri atakayepatikana na hatia atalazimika kulipa faini ya kiasi kisichozidi Tsh 50,000,000(Milioni Hamsini), au kifungo kisichozidi miaka mitano (5) au vyote kwa pamoja.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kuwabaini waajiri ambao bado hawajajisajili na WCF na ambao hawafuati sheria ya ajira na mahusiano kazini, mkoani Tanga Ijumaa Machi 2, 2018, Mhe. Mavunde alisema.
“Si jambo zuri kwa waajiri kutekeleza matakwa hayo ya kisheria hadi wanapoona kiongozi wa serikali amewafikia, hii siyo sawa, na kuonya kuwa ni muhimu waajiri wakatambua kuwa zama zimebadilika, hakuna kichaka cha kujificha, vichaka vyote vinawaka moto hivi sasa.” Alisema.

Mhe. Mavunde pia aliwatahadharisha waajiri ambao wamejisajili kwa kupeleka taarifa za uongo kuhusu shughuli zao ikiwa ni pamoja na idadi ya wafanyakazi wao na viwango vya malipo ya mishahara ya wafanyakazi hao, kwani kwa kufanya hivyo ni kutenda kosa la jinai.

Naibu Waziri ambaye kwa sasa yuko katika ziara ya kukagua utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Aira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama alilotoa mwishoni mwa mwaka jana, la kuwataka waajiri kutoka sekta rasmi (umma na binafsi) Tanzania Bara, kutekeleza takwa la kisheria linalowataka kujisajili na kutoa michango Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF).

“Kama nilivyowaeleza wenzenu kwenye mikoa niliyotembelea ya Mwanza, Shinyanga, Kilimanjaro na leo hapa Tanga ninarudia tena, nia ya serikali ni kuwaondolea mzigo wa gharama waajiri, ya kuwahudumia wafanyakazi wao wanapopatwa na madhara wakati wakitekeelza majukumu yao ya kikazi, na badala yake wajibu huo uchukuliwe na serikali kupitia Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi”.

Tunataka ninyi waajiri mjikite zaidi kwenye shughuli zenu za msingi za kufanya biashara na uwekezaji, na jukumu la kuwahudumia wafanyakazi wanapodhurika kazini tuachieni sisi serikali, alisisitiza Mhe. Antony Mavunde.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw. Anselim Peter, Mkoa wa Tanga una jumla ya waajiri 769 na kati ya hao, ni waajiri 413 tu ndio wamejisajili, huku wengine 356, bado hawajatekeleza takwa la kisheria la kujisajili na kupeleka michango kwenye Mfuko.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com