METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, January 16, 2020

WADAU WAKUTANA KUHUISHA SERA YA WAZEE YA MWAKA 2003




Na Mwandishi Wetu Morogoro




Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya- Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu akitoa maelezo kuhusu Sera ya Wazee ya mwaka 2003 ambayo inafanyiwa mapitio ili kuiboresha wakati alipofungua kikao cha  wadau wanaoshughulikia huduma na haki za wazee kwenye ukumbi wa Chuo cha VETA jijini Dodoma. 


Baadhi ya wadau mbalimbali wanaoshiriki kikao kazi cha kuhuisha Sera ya Wazee wakifuatilia mwongozo wa utoaji maoni ili kuboresha sera hiyo  katika ukumbi wa VETA jijini Dodoma. 

Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na watoto Dkt. John Jingu amewataka wadau wa utoaji huduma kwa wazee kutoa maoni ya kuboresha Sera ya Taifa a Wazee ya Mwaka 2003 ili kukidhi mahitaji ya wazee ambao wamelitumika Taifa kwa bidii na maarifa pindi walipokuwa na nguvu na sasa wanapata huduma, fursa na kuenziwa.

Dkt. Jingu alisema hayo wakati wa kufungua Kikao cha wadau wa Kitaifa waliokutana jijini Dodoma kwa lengo la kuhuisha Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 ambayo inapitiwa, kujadiliwa na kupokea maoni kuhusu uhalali wa matamko na maelekezo ya kisera kwa ajiliya kuboreshwa ili kuwapa fursa ya kuendelea kutoa mchango katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.   

Aidha Dkt. Jingu amebainisha kuwa Mtaalam mwelekezi Dkt. Richard Sambaiga ameandaa rasimu ya awali ya Sera hiyo itatumika kuchochea fikra za wadau ili kupata maoni chanya yatakayojumuishwa katika Sera iliyoboreshwa maana itazingatia mazingira halisi ya afya, ulinzi, usalama, hifadhi ya kijamii, matunzo na ushirikishwaji katika masuala ya kijamii.

Katika kutkeleza Sera ya Wazee ya Mwaka 2003, Dkt. Jingu ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhudumia wazee ikiwa ni pamoja na kusimamia makao ya wazee 17 ya yanayomilikiwa na Serikali ambayo hivi sasa yamepunguzwa manne na kubaki  13 kwa ajili ya kuboresha huduma kwa wazee wasiojiweza wanaoishi katika makao hayo baada ya familia zao kushindwa kuwapa huduma za msingi. 

’’Katika mazingira ya kawaida Serikali inachukua jukumu la kuwalea wazee baada ya kuthibitika kuwa familia husika haina uwezo au haikujitokeza kutoa huduma’’. Aliongeza Dkt. Jingu.  

Aidha Dkt. Jingu amesisitiza kuwa wajibu wa kulea wazee wasio jiweza sio haukomei tu kwa familia bali ni jukumu linalohussha pia jamii kwa ujumla hivyo amewataka wadau wote kutambua kuwa kila mtu anamchango katika malezi  na matunzo ya wazee hapa nchini.

Kadhalika, Mpango wa utambuzi wa wazee katika Halmashauri hadi kufikia Desemba, 2019 umewezesha kuwatambua  jumla ya Wazee 1,837,162 (Me 834,595 na Ke 1,002,567). Kati yao wazee wasio na uwezo 684,383 (ME:348,171, KE:336,212) wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bila malipo.  
Naye Kamishina wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi ameeleza kuwa ni muhimu kuboresha Sara ya wazee ili kuakisi mahitaji na changamoto zinazowakabili wazee kwa kuatika mazingira ya sasa maana sera iliyopo ni ya miaka16 iliyopita.
Dkt. Ngondi ameongeza kuwa azma ya kikao cha wadau wanaosimamia na kushughulikia masuala ya huduma na haki za wazee watajadili kwa pamoja na na kupendekeza namna sera pendekezi itaweza kuzingatia maeneo ya msingi.

Aidha Mtaalam mwelekezi anayeandaa Sera ya Wazee Dkt. Richard Sambaiga aliwambia washiriki kuwa suala la uzee na kuzeeka sio suala la kupuuzwa tena bali ni jambo ambalo linahitaji kuzingatiwa katika mipango ya maendeleo ya kisekta maana idadi ya wazee hapanchini ambayo ni takriban asilimia 5.6 itaongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2050 maana uwekezaji unaofanyika unaongeza idadai ya wazee na kupunguza umasikini uliokithiri.   
Itakumbukwa kuwa wazee wanatambulika kuwa ni walinzi wa mila na desturi, washauri/wapatanishi, na walezi wa watoto wadogo hivyo Sera inayoboreshwa itaweka matamko ambayo yatahakikisha wazee wanathaminiwa katika jamii kwa kuwa, uwepo  wa Taifa la Tanzania ni kielelezo tosha cha mchango mkubwa wa utumishi wa wazee katika nyanja mbalimbali.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com