Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga (Mb)
Revocatus Kassimba,
Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali imewatoa hofu wakulima nchini kuwa
hakuna taarifa za uthibitisho wa uwepo wadudu hatari aina ya Nzige wa Jangwani
walioripotiwa katika nchi za jirani.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ametoa kauli
hiyo jana (29.01.2020) wakati alipozungumza na waandishi wa habari ofisini
kwake Dodoma na kusema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za
kufuatiliaji viashiria vya uwepo wa Nzige wa Jangwani (Locust Desert).
“Hadi sasa hakuna uthibitisho wa kitaalam
kuhusu uwepo wa Nzige wa Jangwani nchini Tanzania” alisisitiza Waziri Hasunga
Alibainisha wazi kuwa Serikali imejipanga
kuwadhibiti nzige hao endapo wataingia nchini na tayari ina lita 7,000 za
viuatilifu kwa ajili ya tahadhari ya kukabiliana na tishio hilo na ununuzi wa
viuatilifu vingine zaidi unaendelea kufanyika.
Alisema Wizara yake inaendelea kuchukua
tahadhali kuhakikisha visumbufu vya mazao ya kilimo kama Nzige Wekundu, Ndege
waharibifu wa nafaka aina ya Kwelea kwelea, panya na Kiwavijeshi Vamizi
zinaripotiwa na kudhibitiwa kwa haraka.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo tishio la Nzige
wa Jangwani limeripotiwa katika nchi za Eritrea, Ethiopia, Somalia, Sudan na
Kenya hivyo kuwepo uwezakano wa Tanzania kuvamiwa na Nzige hao.
“Tanzania
ni miongoni mwa nchi zinazoweza kuathirika na aina mbili za Nzige yaani Nzige
Wekundu na Nzige wa Jangwani hivyo tumejipanga kuwadhibiti wakitokea” alisema
Waziri wa Kilimo.
Waziri
wa Kilimo amewataka wataalam wa kilimo kwenye Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za
Mitaa kuwasimamia Maafisa Ugani waliopo kwenye maeneo yao ili kuhakikisha
kwamba wanawatembelea wakulima mashambani na kubaini endapo kuna viashiria vya
uwepo wa Nzige.
Serikali itaendelea kuhakikisha visumbufu vya
mimea na mazao vinadhibitiwa ili wakulima wavune mazao yao kwa wingi na nchi
kuendelea kuwa na uhakika wa chakula.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment