METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, December 20, 2019

NI MARUFUKU MADALALI KWENYE MAZAO - MHE HASUNGA

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua skimu ya Umwagiliaji  ya Makwale iliyopo katika kata ya Makwale Wilayani Kyela, leo tarehe 20 Disemba 2019 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
 Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua skimu ya Umwagiliaji  ya Makwale iliyopo katika kata ya Makwale Wilayani Kyela, leo tarehe 20 Disemba 2019 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akishuhudia mnada wa Kakao katika kijiji na kata ya Ikolo ambapo Kakao imeuzwa kwa bei ya shilingi 5042 kwa kilo moja, leo tarehe 20 Disemba 2019 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya. 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Kyela

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 20 Disemba 2019 amepiga marufuku madalali wa mazao ya kilimo ambao wanatumia nafasi hiyo kuwagalaliza wakulima.

Waziri Hasunga amepiga marufuku hiyo wakati akizungumza kwenye mnada wa Kakao uliofanyika kwenye kijiji na kata ya Ikolo iliyopo katika Wilaya ya Kyela wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya.

Amesema kuwa "kumekuwa na wananchi wasiokuwa waaminifu kwa serikali na wakulima wake ambao wanawaibia wakulima maarufu kama Njemke, Butura, na Kangomba hivyo napiga marufuku biashara hiyo na endapo tukiwakamata tutawachukulia hatua za kisheria"

Waziri Hasunga amewaagiza wanunuzi hao wa Kakao na mazao mengine kuhakikisha kuwa wanawalipa wakulima fedha zao mara baada ya kukamilika kwa minada ili waweze kupata fursa ya kuandaa mashamba katika kipindi hiki cha msimu wa kilimo.

Waziri Hasunga amesema kuwa zao hilo la Kakao litasalia kuuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwani kupitia mfumo huo ambao unasimamiwa chini ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika wakulima wataendelea kunufaika na mazao yao kwa kupata bei nzuri.

Amesema kuwa bado vyama vya ushirika vina matatizo makubwa lakini serikali itaendelea kusimamia kwa weledi vyama hivyo ikiwemo kuchukua hatua za haraka kwa viongozi wa vyama hivyo wanaotumia vibaya nafasi yao kwa kuwaibia wakulima.

Amevitaka Vyama vikuu vya ushirika wa Kakao kuwa pamoja na kusimamia ubora wa zao hilo lakini pia amesema kuwa vyama hivyo vinapaswa kuendelea kuhamasisha wadau mbalimbali kuanzisha viwanda vya kuchakata Kakao ikiwa ni sehemu muhimu ya kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kuhamasisha sekta ya viwanda.

Amesema kuwa Kakao inayolimwa wilayani kyela nchini Tanzania ni miongoni mwa Kakao bora Duniani ambayo ina ubora mzuri kuliko Kakao nyinyine zinazozalishwa katika nchi za Afrika Magharibi.

Waziri Hasunga ameshuhudia mnada wa Kakao katika kijiji na kata ya Ikolo ambapo imeuzwa kwa bei ya shilingi 5042 kwa kilo moja ambapo amesisitiza kuwa bei hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa wakulima.

Sambamba na hayo Mhe Hasunga amewasihi wakulima kuendelea kulima zao hilo huku akiahidi kuwa serikali kupitia wizara ya kilimo itaendelea kusimamia kwa weledi kuongeza tija na uzalishaji.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com