METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, July 9, 2018

Serikali yatakiwa kufanye tathmini ya viwanja vya ndege




Na Mwandishi Wetu

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imeitaka serikali kufanya tathmini ya viwanja vya ndege nchini, inavyojiendesha kwa faida na hasara, ili iweze kuvihudumia vyema.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Mchafu ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati kamati hiyo ilipofanya ziara kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), na kupata taarifa mbalimbali za uendeshaji.

Mhe. Hawa amesema tathmini hiyo itasaidia kupunguza viwanja ambavyo ni mzigo kwa kuwa havizalishi ipasavyo na kuwa tegemezi kwa vingine.
“Serikali ifanye tathmini upya ya viwanja vya ndege ili iweze kuangalia vile vinavyozalisha na kuviwekea mkazo hata ikiwezekana ivigawe kwa kanda,” amesema Mhe. Hawa.

Hata hivyo awali katika taarifa yake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela ameiambia Kamati hiyo kuwa moja ya changamoto TAA inakutana nayo ni pamoja na kujiendesha kwa taabu kutokana na kuhudumia viwanja vingi visivyozalisha na kuwa tegemezi kwa vingine vichache vinavyozalisha.

Bw. Mayongela amesema kati ya viwanja vyote 58 vya ndege vingi ni tegemezi kwa zaidi ya asilimia 90, ambapo mapato mengi yanatoka kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na viwanja vichache vinavyozalisha.

Amesema changamoto nyingine ni uchakavu wa miundombinu ya viwanja, maegesho ya ndege na ufinyu wa majengo ya abiria katika viwanja vya ndege vya Dodoma, Mwanza, Mafia, Arusha na Ziwa Manyara; kutokuwa na mfumo wa kuongozea ndege wakati wa kutua na kuruka, ambapo husababisha viwanja vingi kutumika kwa saa 12 pekee kwa kushindwa kutua nyakati za usiku.

“Tatizo jingine ni uchakavu wa magari ya zimamoto na uokoaji yaliyopo kwenye baadhi ya viwanja, hivyo kunahatarisha usalama wa abiria na ndege; hali kadhalika wapo wananhi wanaovamia maeneo ya viwanja nao husababisha tutumie gharama kubwa za kuwaondoa,” amesema Bw. Mayongela.

Hata hivyo, Bw. Mayonbgela amesema pamoja na TAA kukabiliwa na changamoto la kutokuwepo kwa uzio kwa baadhi ya viwanja vya ndege, sasa wapo mbioni kujenga uzio kwenye Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, ambapo itasaidia kupunguza wananchi na mifugo kukatiza kwenye barabara ya kutua na kuruka kwa ndege.

Akizungumzia suala la uvamizi Mweyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Suleiman Kakoso amewataka wananchi kuacha kuvamia maeneo ya viwanja vya ndege ambavyo yapo halali kisheria.

“Viwanja vyote ni vya serikali na hao wanaovamia wanaonekana, basi waondolewe kulingana na sheria kwani wapo kwenye mikoa ambayo viwanja vipo,” amesema Mhe. Kakoso.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa amesema TAA inafanya jitihada ya kununua magari ya zimamoto na kuboresha miundombinu mbalimbali ili kuviweka viwanja vyake katika hali bora.

MWISHO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com