METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, December 1, 2019

Mkoa wa Mara Wajivunia Mafanikio Miaka 4 ya Serikali ya Awamu ya Tano


*******************************
Na Mwandishi wetu
Serikali ya Awamu ya Tano imeuwezesha mkoa wa Mara kujenga Hospitali 4 za Wilaya, Vituo vya Afya 13 kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Akizungumza katika kipindi cha ‘TUNATEKELEZA’ Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam
Malima amesema mkoa huo umepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma
mbalimbali za jamii ikiwemo sekta ya afya kutokana na kutekelezwa kwa ujenzi wa miundombinu ya sekta hiyo kwa ufanisi.

“Mradi wa Hospitali ya Kanda ya Mwalimu Nyerere unaendelea vizuri na utawezesha wananchi kupata huduma za kibingwa ikiwemo za mifupa na nyingine hali itakayoondoa adha ya wananchi kusafiri hadi Hospitali ya Bugando kufuata huduma hizo” Alisisitiza Malima.

Akifafanua amesema kuwa mkoa huo umepata mafanikio makubwa katika sekta
nyingine kama vile elimu kwa kujenga miundombinu ya kisasa yakiwemo madarasa na maabara hali iliyochangia kukua kwa kiwango cha elimu katika mkoa huo ikilinganishwa na miaka iliyotangulia kabla ya uwekezaji huo.

Kwa upande wa sekta ya madini amesema kuwa kuwepo kwa sheria nzuri na taratibu zilizowekwa na Serikali ya Awamu ya Tano, mkoa huo umezalisha kilo 130 za dhahabu kufikia Septemba mwaka huu hali inayochangia kukuza sekta ya madini na uchumi kwa ujumla.

Akizungumzia mikakati yake ya kukuza kilimo na uvuvi, Mhe. Malima amesema kuwa dhamira ya mkoa huo ni kuona sekta hizo zinatoa mchango stahiki katika uchumi kutokana na hatua zilizochukuliwa katika kokomesha uvuvi haramu katika mkoa huo.

Aidha, Mhe. Malima amebainisha kuwa wamejipanga kukuza sekta ya utalii katika mkoa huo ili kuongeza pato la mkoa huo hatua itakayowasaidia kuwainua wananchi kiuchumi na Taifa kwa ujumla.

Kipindi cha ‘TUNATEKELEZA’ kinarushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kuratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO ambapo awamu hii inawashirikisha wakuu wa mikoa yote Tanzania Bara.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com