METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, December 13, 2019

BODI TISA ZA MAZAO KUUNGANISHWA ILI KUUNDA BODI TATU PEKEE-WAZIRI HASUNGA

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika katika ukumbi wa Wilaya ya Tandahimba akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mtwara, jana tarehe 13 Disemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Sehemu ya wakulima wa korosha wakifatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika katika ukumbi wa Wilaya ya Tandahimba akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mtwara, jana tarehe 13 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika katika ukumbi wa Wilaya ya Tandahimba akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mtwara, jana tarehe 13 Disemba 2019.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara

Serikali imedhamiria kuziunganisha Bodi sita za mazao zilizopo chini ya Wizara ya Kilimo na kuwa na Bodi tatu ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo jana tarehe 13 Disemba 2019 wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika katika ukumbi wa Wilaya ya Tandahimba akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mtwara.

Waziri Hasunga amesema kuwa kumekuwa na Bodi nyingi lakini matokeo ya kiutendaji hayaakisi wingi huo hivyo ili kuboresha majukumu yake na kuwa na weledi katika kazi Bodi hizo zitaunganishwa.

Amesema kuwa Bodi saba zitaunganishwa na kuunda Mamlaka moja ya kusimamia mazao ya kimkakati ambayo ni pamoja na Kahawa, Pamba, Mkonge, Tumbaku, Pareto, Korosho, Alizeti na zao la mchikichi.

Waziri Hasunga amesema kuwa mabadiliko hayo yatakayozihusisha Bodi hizo yatapelekea kuundwa kwa idara za kusimamia kila zao.

Bodi nyingine ya pili itasimamia mazao ya nafaka, mboga mboga na matunda (Cereal and Horticulture Authority) pamoja na Bodi ya Sukari itakayosalia kujitegemea.

Amesema, kuwa na Bodi nyingi kumepelekea usimamizi kuwa mgumu kadhalika kuwa na Bodi chache kutaimarisha ufanisi na uwezo wa kuwasimamia watendaji wake.

Sambamba na hayo Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa Wizara ya Kilimo ipo katika mchakato wa kupitia upya sheria ya Ushirika pamoja na Shirika la ukaguzi wa vyama vya Ushirika-COASCO ili kuimarisha sheria na kuwa na usimamizi madhubuti wa mali za wananchi kwenye Ushirika.

Waziri Hasunga yupo mkoani Mtwara kwa ajili ya ziara ya kikazi ambapo awali alitembelea mkoa wa Pwani na Lindi kwa ajili ya kukagua hali ya uuzaji wa korosho msimu wa 2019/2020, kukagua hatua zilizofikiwa za malipo ya wakulima wa korosho zilizonunuliwa na serikali msimu wa mwaka 2018/2019 na kukagua skimu za umwagiliaji.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com