Wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari
nchini wakiendelea na zoezi la upakiaji wa mbolea ya kupandia tani elfu
23 tayari kwenda kwa wakulima mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari
nchini wakiendelea na zoezi la kufunga mbolea ya kupandia katika mifuko
tayari kwa kupakiwa na kusafirishwa kwenda kwa wakulima.
Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya
Udhibiti wa Ubora wa Mbolea Tanzania(TFRA) Bw. Lazaro Kitandu (katikati)
akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari wakati zoezi la upakuaji wa
mbolea ya kupandia ukiendelea katika bandari ya Dar es Salaam mapema hii
leo.
Picha na Eliphace Marwa – Maelezo
……………………………………………….
Na. Eliphace Marwa – Maelezo
Serikali imeingiza nchini
jumla ya tani elfu 32 za mbolea ya kukuzia pamoja na tani elfu 23 za
mbolea ya kupandia kupitia mfumo mpya wa uagizaji wa mbolea kwa pamoja,
lengo likiwa ni kudhibiti bei kwa kuzingatia bei elekezi.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam wakati zoezi la upakuaji wa mbolea hiyo likiendelea Kaimu
Mkurugenzi Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea Tanzania(TFRA) Bw.
Lazaro Kitandu amesema kuwa mpaka sasa jumla ya tani elfu 55 za mbolea
zimewasili nchini.
Hii ni awamu ya kwanza ya
kuingiza mbolea nchini kupitia mfumo mpya ya uagizaji mbolea kwapamoja
ambapo kampuni ya OCP S.A ya nchini Morocco imeingiza jumla ya tani elfu
23 za mbolea ya kupandia na Kampuni ya Premium Agro Chem imeingiza tani
elfu 32 za mbolea ya kukuzia.
“Mpaka sasa zoezi la kupakua
mbolea ya kupandia (DAP) tani elfu 23 linaendelea vizuri na mara baada
ya kumaliza kupakua mbolea hii tutaanza zoezi la kupakua mbolea ya
kukuzia (UREA) ambayo ni tani elfu 32,” alisema Bw. Kitandu.
Kitandu aliongeza kuwa
Mheshimiwa Waziri wa kilimo juzi alipokuwa anaongea na waandishi wa
habari mjini Dodoma na akasisitiza bei ambazo zimetolewa zisimamiwe na
kila ngazi kwasababu taasisi peke yake haiwezi kuwa na watu kila mahali
hivyo Tawala za mikoa, Serikali za mitaa mpaka Kijiji zitasaidia
kusimamia bei ambazo zimetolewa.
Pia Kitandu aliongeza kuwa
kuhusiana suala la bei ya mbolea hiyo itatangazwa kupitia vyombo vya
habari kama vile magazeti na televisheni na hivyo kutoa onyo kwa
mawakala kujipangia bei kwa kuuza mbolea nje ya bei elekezi ya
Serikali kwamba watachukuliwa hatua za kisheria kama kunyang’anywa
leseni, kufungwa, faini au vyote kwa pamoja.
Aidha Kitandu alisisitiza kuwa
mbolea hizi siyo mbolea za ruzuku kwani wakulima wengi wamekuwa
wakichanganya mbolea hizi na mbolea za ruzuku na amefafanua kuwa mbolea
hii imefanyiwa utaratibu wa kudhibiti toka kule inapotoka na hivyo
serikali itahakikisha mbolea hii inauzwa kwa kulingana na bei ya soko la
dunia.
Aidha Bw. Kitandu aliwahakikishia
wakulima kuwa mbolea itasafirishwa mpaka vijijini kwa kutumia treni na
malori kwa sehemu ambapo treni haiwezi kufika, na amewatoa hofu
wakulima kuwa msimu unaoanza mwezi huu wameingiza tani 23,000 kwa mbolea
ya kupandia (DAP) na tani 32,000 kwa mbolea ya kukuzia (UREA) ambapo
watakuwa wanaagiza kwa awamu kwa miezi miwili miwili.
0 comments:
Post a Comment