METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, November 23, 2019

Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda Awataka Watumishi Rukwa kupambana na Udumavu


Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda akizungumza na watumishi wa Mkoa wa Rukwa (hawapo pichani)
Wakuu wa taasisi mbalimbali zinazohudumu katika mkoa wa Rukwa wakimsikiliza Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda (hayupo pichani)
Wakuu wa Idara na vitengo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa wakimsikiliza kwa makini Wazriri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda (hayupo pichani)
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa pongezi zake kwa Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda (aliyepo kushoto kwake) muda mfupi kabla ya kumkaribisha kuwasalimu watumishi wa mkoa wa Rukwa.
…………………

Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mizengo Pinda amewasisitiza watumishi mkoani Rukwa kuhakikisha kila mmoja katika nafasi yake anafanya kazi kwa uadilifu na kueleza kuwa utendaji kazi wa aina hiyo ndio njia pekee ya kupeleka maendeleo ya mkoa mbele na hatimae kuutoa mkoa katika umasikini.


Amesema kuwa amesikitishwa na taarifa iliyolewa hivi karibuni kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2018 ambapo mkoa wa rukwa umeonekana kushika mkia kwa kuwa na asilimia 45 ya umasikini nchini kwa mahitaji ya msingi huku mkoa wa Dar es Salaam ukiwa na asilimia 8 ya kiwango hicho huku mkoa wa Katavi uliozaliwa kutoka mkoa wa rukwa ukiwa na asilimia 29


Pia ameshtushwa kuwa mkoa wa Rukwa ambao ni miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini kuwa na kiwango kikubwa cha udumavu pamoja na kuongoza kuwa na kiwango kikubwa cha umasikini wa chakula kwa asilimia 19 wakati Katavi ukiwa na asilimia 9.


“Tukikaa sisi kama wataalamu, najua baadhi ya wilaya wameshapata maafisa lishe, tutawatengenezea mfumo tuwaonganishe na majukumu ya zahanati na vituo vya afya na hospitali zetu za wilaya, mama anapokuwa ametunga mimba lazima aambiwe aende kliniki, lakini kliniki si kupima tu uzito nakadhalika, hapana, kubwa ni kuona kwamba huyu mama mzazi anapata lishe stahiki?” Alihoji.


Amesema kuwa fikra zilizopo katika makabila yaliyopo mkoa wa Rukwa na Katavi wanaamini kuwa kula mboga za majani ni umasikini wa kutupwa kwahiyo kama mkoa una kazi kubwa ya kubadili fikra za watu hao na kuonyesha umuhimu wa kula mboga za majani.


Ameyasema hayo katika salamu zake kwa watumishi wa mkoa wa Rukwa hivi karibuni ambapo kikao hicho kiliwajumuisha wakuu wa taasisi, idara, wakala za serikali pamoja na watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa Wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mh. Joachim Wangabo.


Wakati akimkaribisha Waziri Mkuu Mstaafu, Mh. Joachim Wangabo alimpongeza Mh. Pinda kwa kuhakikisha anasogeza huduma muhimu kwa wananchi kwa kuugawa mkoa wa Rukwa na kuzaliwa Mkoa wa Katavi ambapo hivi sasa wananchi wa mkoa wa Katavi wanafaidika na maendeleo yanayopatikana kutokana na uwepo wa huduma muhimu za kijamii katika halmashauri tano za mkoa huo.


“ Wilaya ya Mpanda ilikuwa inapakana na Kaliua, Uvinza na inapakana na Sikonge Mkoa wa Tabora, Sasa fikiria huyo RC aliyekuwa anatoka Sumbawanga kwenda mpaka huko, huenda ukakaa miaka mitano usifike maeneo mingine, ilikuwa ni shida kweli na miundombinu yake ilikuwa ni matatizo makubwa sana kwahiyo kuugawa huu mkoa wa Rukwa kuwa mikoa miwili umetoa unafuu mkubwa sana wa kimaendeleo” Alisema.


Mkoa wa Rukwa ulianzishwa mwaka 1974 kwa kumega sehemu ya Mikoa ya Tabora na Mbeya. Mkoa una eneo la kilomita za mraba 27,765,  kati ya hizo Kilomita za mraba 22,844 (82.3%) ni za nchi kavu na Kilomita za mraba 4,921 (17.7%) ni za maji. Mkoa una jumla ya Wilaya tatu (3), zenye Halmashauri nne (4), Tarafa 16, Kata 97, Vijiji 339, Vitongoji 1,825, Mitaa 167 na Kaya 199,766. Mwaka 2010 mkoa uligawanywa na kuzaliwa mkoa wa Katavi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com